Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizindua jukwaa la uwezeshaji
wanawake kiuchumi Mkoani Singida, kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt. Angelina M. Lutambi na kushoto ni Mratibu wa Jukwaa la
uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida Daniel Munyi.
Baadhi ya wanawake wajasiriamali waliohudhuria uzinduzi wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida
Dkt. Angelina M. Lutambi akizungumza na wanawake wajasiriamali wa Mkoa
wa Singida na kushoto kwake ni Mratibu wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake
kiuchumi Mkoani Singida Daniel Munyi.
Mwenyekiti
wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida Bi Neema
Salumu akiwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumchagua nyuma yake ni
Makamu Mwenyekiti wa jukwaa hilo Happy Fransis.
Mwenyekiti
wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida Bi Neema
Salumu akiwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumchagua kushoto kwake ni
Makamu Mwenyekiti wa jukwaa hilo Happy Fransis na Kulia ni Katibu Tawala
Mkoa wa Singida Dkt. Angelina M. Lutambi.
………………………………………………………………………….
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi amewataka akina mama wajasiriamali wote kuacha kulalamika
na kutumia fursa zilizopo kujiinua kiuchumi kwakuwa wakati wa
kulalamika umeisha na sasa ni kuchapa kazi tu.
Dkt. Nchimbi ametoa rai hiyo
mapema leo wakati akizindua rasmi jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi
Mkoa wa Singida na kusisitiza kuwa wanawake sio dhaifu bali watu dhaifu
ni wale wanaofikiria mwanamke ni dhaifu.
Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa
jukwaa hilo alilolizindua liwe sehemu ya kuwafundisha akina mama mbinu
na fursa za uwekezaji pamoja na matumizi mazuri ya fedha wanazozipata
hasa mikopo.
Amesema ‘kukopa hakukwepeki
katika maisha ya sasa, ila akina mama wengine wanakopa na kuzitumia,
vibaya ukiona nguo inapita unanunua wakati haikuwa katika malengo ya
mkopo, eti ukishakopa ndio unatamani kula kuku ujionyeshe una pesa,
hapana….. kwa namna hii hautaweza kufika popote, hakikisha unabaki
katika malengo ya mkopo’.
Dkt. Nchimbi amesema jukwaa liwe
jicho la kuhakikisha kuna usalama wa chakula Mkoani Singida kwa kuanzia
ngazi ya kila kaya ambapo wanapaswa kuelimisha kaya kuhusu matumizi
mazuri ya chakula hasa kulima mazao yanayotumia maji kwa ufanisi na
kutunza akiba ya chakula.
Ameeleza kuwa majukumu ya jukwaa
hilo ni pamoja na kuangalia namna ya kurejesha maadili ya vijana na
kuwakemea ili wasijiingize katika matumizi ya madawa ya kulevya kwakuwa
limekuwa tatizo katika maeneo mengi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa
Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoa wa Singida Bi Neema Salumu
ambaye amechaguliwa mara baada ya jukwaa hilo kuzinduliwa amewashuruku
wajumbe kwa kumuamini na kumchagua huku akiahidi ushirikiano na kufanya
kazi kwa bidii katika kuhakikisha wanawake sehemu ya kukuza uchumi.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt. Angelina M Lutambi amewashukuru wanawake ambao wametoka
katika halmashauri zote saba za mkoa wa singida kwa kushiriki uzinduzi
wa jukwaa hilo.
Dkt. Lutambi ameongeza kuwa
anasimamia na kutekeleza mambo yote yanayohusu maendeleo hasa
yanayolenga kuboresha uchumi wa mwanamke Mkoani Singida kwakuwa anaamini
ukimuwezesha mwanamke unajenga uchumi wa taifa.
Wajumbe walioshiriki jukwaa la
uwezeshaji wanawake uchumi Mkoani Singida wamepewa elimu ya sheria ya
kodi na umuhimu wa kulipa kodi, elimu na upatikanaji wa mikopo pamoja na
uhusiano wa wanawake na uchumi wa Tanzania.
No comments :
Post a Comment