Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Vyuo Vikuu hapa Nchini vimeagizwa kuacha mara moja kutoza ada kwa fedha za kigeni kwa wanafunzi ambao ni watanzania.
Agizo hilo limetolewa leo
Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge
Jaku Hashimu Ayoub kwamba kumekuwa na malalamiko ya wanafunzi wa Elimu
ya Juu Tanzania ambao ni wazawa kulipishwa ada ya masomo yao kwa fedha
za kigeni badala ya fedha za Kitanzania.
“Sarafu inayotakiwa kutumika
Tanzania ni shilingi ya Kitanzania kwa mujibu wa kifungu cha 25 na 26
cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya mwaka 2006. Aidha, kwa
Tanzania malipo ya kitu au huduma yoyote inapaswa kulipwa kwa shilingi
ya Kitanzania kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 28 cha Sheria ya
Benki Kuu ya Tanzania, 2006,” alifafanua Mhandisi Manyanya.
Aliendelea kwa kusema kuwa japo
Wizara haijapokea malalamiko yoyote ya kutozwa fedha za kigeni kwa
wanafunzi wa Elimu ya Juu tangu itoe agizo kama hilo kwa wamiliki wa
vyuo Septemba 07, 2016.
Hivyo basi kwa mara nyingine
Mhandisi Manyanya ameviagiza vyuo ambavyo bado vinatoza wanafunzi
Watanzania fedha za kigeni kuacha mara moja kwani vyuo hivyo
vimeelekezwa kutoza wananchi wa Kitanzania kwa pesa ya Kitanzania.
Aidha Mhandisi Manyanya
amewataka watanzania kutoa taarifa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia ikiwa kuna Chuo chochote kinachotoza ada kwa Watanzania kwa
fedha za Kigeni ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi ya
wahusika.
No comments :
Post a Comment