BAADHI ya madiwani, watendaji na
wenyeviti wa Serikali za mitaa kutoka Wilaya Tatu za Mkoa wa Dar es
Salaam yaani Temeke, Ilala na Kinondoni wameviomba vyama vya siasa kutoa
fursa za uongozi kwa wanawake ili waongezeke katika nafasi za uongozi
ngazi mbalimbali.
Ombi hilo limetolewa na viongozi
hao katika maoni yao walipokuwa katika semina kuangalia usawa wa
kijinsia katika nafasi mbalimbali za uongozi iliyoandaliwa na Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP). Baadhi ya viongozi hao na watendaji walisema
kumekuwa na changamoto nyingi ndani ya vyama vya siasa ambazo
zinaendelea kuwa vikwazo kwa wanawake kushiriki katika nafasi za uongoni
katika vyama anuai, hivyo kama zikiangaliwa zinaweza ongeza hamasa kwa
wanawake kupata nafasi za uongozi.
Hata hivyo wamewataka wanawake
kuendelea kujitokeza, kujiunga na vyama mbalimbali vya siasa pia
kushiriki kugombea nafasi ili waweze kuonekana na kukwaa nafasi hizo.
“Mbali na
Vyama vya siasa kutakiwa kuregeza masharti na kutoa fursa kwa
kundi la wanawake, wao pia wanatakiwa kujitokeza kushiriki katika
siasa…na hata kugombea nafasi mbalimbali ili waonekane,” alisema mmoja
wa washiriki wa semina hiyo.
Kwa pamoja viongozi hao
walikubaliana kuendelea kuwaunga mkono kundi hilo katika ushiriki wa
siasa ili kujenga usawa wa kijinsia katika nafasi za maamuzi kuanzia
ngazi za chini na kuendelea.
Kwa upande wake Afisa Programu na
Uchambuzi wa TGNP, Deogratius Temba akiwasilisha mada katika semina hiyo
alisema wanawake ni wadau muhimu katika shughuli zote za kisiasa na
maendeleo ya jamii hivyo kuna kila sababu ya kupewa nafasi ili waingie
katika vyombo vya maamuzi. Alisema yapo matamko mbalimbali ya juu ya
umuhimu wa kundi hilo kushiriki katika uchaguzi, japokuwa utekelezaji
wake kivitendo umekuwa na changamoto kadhaa.
Aidha alitolea mfano matamko hayo
ni pamoja na Tamko la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (U 1948),
Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya
wanawake (CEDAW: 1979) na mpango kazi wa Beijing (1995). Pamoja na hayo
alisema licha ya kundi hilo kusahaulika lakini limekuwa likitumiwa na
vyama vya siasa kuhamasisha na kueneza sera zao ikiwemo kuongeza
wanachama jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umuhimu hivyo kupewa
fursa katika ushiriki.
No comments :
Post a Comment