Kulia Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu
wa Rais Profesa Faustin Kamuzora, akitoa Tamko la Siku ya Mazingira
Afrika kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. January Mkamba, Leo katika mkutano na waandishi wa Habari
Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya
Mazingira wa Ofisi hiyo Bw. Richard Muyungi.
TAMKO LA WN-OMR – MMZ BW. JANUARY Y. MAKAMBA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA AFRIKA TAREHE 3 MACHI, 2017
Ndugu Wananchi,
Tarehe 3 Machi kila mwaka
watanzania wote huungana na nchi nyingine za Afrika katika
kuadhimisha
Siku ya Mazingira Afrika, ambayo huadhimishwa barani Afrika kila mwaka.
Siku hii imetengwa kwa lengo la kukumbuka umuhimu wa kutunza na
kuhifadhi mazingira barani Afrika. Azimio la kuadhimisha Siku hii
lilipitishwa na kuamuliwa na Baraza la Mawaziri wanaosimamia Mazingira
wa nchi za Afrika kwenye mkutano uliofanyika Durban, Afrika Kusini Mwaka
2002. Siku hii iliamuliwa iwe kielelezo cha kukuza weledi kuhusu
kupambana na uharibifu wa mazingira pamoja na kuenea kwa hali ya jangwa
Afrika. Kuanzia wakati huo siku hii ilikuwa inaadhimishwa nchini
Ethiopia kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika.
Ndugu Wananchi,
Kikao cha 12 cha Baraza la
Mawaziri wa Mazingira (AMCEN) kiliamua kwamba maadhimisho ya siku hii
yawe yanafanyika kikanda. Hivyo kuanzia mwaka 2009 maadhimisho ya siku
ya Mazingira Afrika yalianza kufanyika kikanda katika nchi za Afrika na
ndipo, mwaka 2010 nchi yetu ikapata fursa ya kuwa mwenyeji wa
maadhimisho haya yaliyofanyika jijini Arusha.
Aidha, Umoja wa Afrika kwa
kutambua juhudi na kazi iliyofanywa na Prof. Wangari Maathai kutokana na
mchango wa mwanamke huyu katika hifadhi ya mazingira na kuwezesha
wanawake katika usimamizi endelevu wa maliasili na mazingira kwa ujumla
waliamua tarehe 3 Machi kila mwaka iwe pia ni siku ya kumkumbuka yake
iende sambamba na maadhimisho ya siku ya Mazingira Afrika. Hivyo tangu
mwaka 2012 maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika yamekuwa yakienda
sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wangari Maathai ili kutambua mchango
wake katika utunzaji wa Mazingira. Mwanamke huyu alipata Tuzo ya heshima
ya Nobel Laureate’s green legacy kutokana na juhudi alizofanya.
Ndugu Wananchi,
Tunapoadhimisha siku hii
tutafakari kwa kina changamoto mbalimbali zinazochangia uharibifu mkubwa
wa Mazingira. Changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi,
kuongezeka kwa hali ya jangwa na ukame, uchafuzi wa mazingira, ongezeko
kubwa la idadi ya watu, kuwepo kwa shughuli za kiuchumi zisizoendelevu
ambazo husababisha uharibifu wa mazingira. Hali hizo husababisha
ongezeko la joto, ongezeko la ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko,
ongezeko la magonjwa mbalimbali ya mlipuko, upotevu wa bioanuai, uhaba
wa chakula na hivyo kusababisha kuwepo kwa ongezeko la umaskini kwa
jamii.
Ndugu Wananchi,
Tunafahamu kabisa hali ilivyo sasa
katika maeneo mengi nchini kwamba majira ya mvua yamebadilika na
kusababisha ukame. Hivyo, inabidi tuhakikishe tunavilinda vyanzo vya
maji kwa gharama yoyote ile. Aidha, katika kuadhimisha maadhimisho haya,
kila mmoja awawajibike ipasavyo katika kukabiliana na uharibifu wa
mazingira unaosababishwa na matumizi yasiyoendelevu ya bioanuai na
rasilimali zake. Hivyo kila mtu afanye shughuli za kiuchumi zisizoharibu
mazingira ikiwa ni pamoja na kutumia nyenzo za uvuvi endelevu, kutumia
nishati jadidifu, majiko sanifu na banifu, nishati mbadala, kudhibiti
uchafuzi, kupunguza uzalishaji wa taka na kusimamia ukusanyaji wa taka
ili kuhakikisha miji yetu inakuwa safi.
Ndugu wananchi,
Natoa wito kwa watanzania
tuadhimishe Siku ya Mazingira ya Afrika kwa kuendeleza na kusisitiza
kampeni ya usafi katika maeneno yetu. Aidha, ninawagiza wananchi wote
kuanzia ngazi ya Kaya, Mitaa, vikiwemo vikundi vya watu binafsi
kushiriki kwenye shughuli za usafi ili kuhifadhi mazingira yetu. Nitumie
fursa hii kuwakumbusha viongozi kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa
kutumia fursa hii kuhuisha Kamati za Mazingira ili ziweze kusimamia
shughuli za utunzaji mazingira katika maeneo yao. Aidha, mikoa,
halmashauri za wilaya, sekta zote, pamoja na taasisi mbalimbali,
mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi wote kwa ujumla kushiriki
katika shughuli za hifadhi na usafi wa mazingira wakati wote.
Ndugu wananchi,
Katika kuadhimisha siku hii, natoa
wito pia kwa viongozi na watendaji katika ngazi zote kuelimisha na
kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingirakwa kuzingatia sheria ya
Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni zake.
Baada ya kusema hayo, nawatakieni maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika yenye ufanisi.
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments :
Post a Comment