Na Jovina Bujulu MAELEZO Dar es Salaam
TAASISI ya sekta binafsi nchini
(TPSF) imetoa wito kwa wahitimu na vijana waliopo vyuoni kuchangamkia
fursa ya mpango maalum uliobuniwa baina yake na Serikali ambao
umekusudia kuwajengea ujuzi kabla ya kuajiriwa ili waweze kufanya kazi
kwa weledi.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye wakati alipokuwa
akichangia mada kuhusu wahitimu wa vyuo vikuu kushindwa
kuonyesha ujuzi
baada ya kuajiriwa.
“Upo upungufu mkubwa wa mafunzo ya
vitendo kwa wahitimu wengi wanaomaliza vyuo vikuu nchini na
imedhihirika kuwa wahitimu hao hushindwa kufanya kazi kwa weledi
wanapokuwa wameajiriwa na sekta mbali mbali.
Alisema kuwa mpango huo maalum
umeanzishwa kwa lengo la kuwatayarisha wahitimu wa vyuo kupata mafunzo
ya muda mfupi ili kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo pindi
wanapoajiriwa au kutaka kujiajiri.
Simbeye alisema Mpango huo pia
umekusudia kuwapunguzia gharama waajiri, hasa wa sekta binafsi kwa kuwa
wengi wao wamekuwa wakitumia pesa nyingi kwa kuwapeleka waajiriwa wapya
katika mafunzo ili waweze kumudu kazi zao.
Akifafanua zaidi alisema katika
mpango huo waajiriwa wataweza kupata mafunzo mtambuka na gharama zote
za mafunzo zinagharimiwa na Serikali.
“Chini ya mpango huu, wahitimu na
vijana walioko vyuoni wanatakiwa kujiandikisha kwa hiari, na baada ya
mafunzo inakuwa rahisi kwao kupata ajira kupitia katika sekta binafsi au
makampuni” aliongeza Bwana Simbeye.
Aidha Bwana Simbeye alisema kuwa
mpango huo pia utawawezesha wahitimu kutengeneza mazingira ya kuanzisha
biashara nyingi na kupanua biashara zilizopo ili waweze kupata fursa
nyingi za kuajiriwa na kujiajiri hasa katika wakati huu ambao nchi
inaelekea katika uchumi wa viwanda.
Akizungumzia mpango huo, Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana, na Walemavu), Anthony
Mavunde alisema kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa kila chuo
kinajitengenezea mwongozo wake unaomwezesha kila mwanafunzi kupata
nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo.
Aidha aliongeza kuwa Serikali
itahakikisha kuwa mpango huo unakuwa endelevu na unafanya kazi kama
ilivyokusudiwa na kutoa wito kwa sekta binafsi na waajiri kutoa maoni
yao ili kuboresha mpango huo
No comments :
Post a Comment