Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Leornard Chamuriho kabla ya kuwaaga
watumishi wa Wizara hiyo wanaohamia Dodoma leo, jijini Dar es salaam.
Picha na Biseko Ibrahim
…………
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka watumishi wa Wizara hiyo
Sekta ya Uchukuzi kutumia vizuri fursa ya kuhamia Dodoma kwa kuwatumikia
watanzania kwa uadilifu na weledi.
Amesema hayo jijini Dar es
Salaam wakati akiwaaga watumishi wa Sekta ya uchukuzi wa awamu ya kwanza
ambao wameondoka leo kuelekea mjini Dodoma.
“Nawapongeza kwa kupata fursa
ya kuwa katika awamu ya kwanza katika Wizara hii kuhamia Dodoma fahamuni
hii ni fursa na si changamoto kwani hatua hii inasogeza huduma karibu
na wananchi hivyo watumikieni kwa moyo”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema kuwa nia
ya Serikali ni kuhakikisha watumishi wake wanahamia Dodoma na kuendelea
na utekelezaji wa majukumu yake kwa wananchi.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa
Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho amesema awamu ya kwanza ya
watumishi zaidi ya 45 inahamia Dodoma mwezi huu na Awamu ya pili itaanza
mwezi wa Machi na watumishi wote wa sekta ya uchukuzi watakuwa Dodoma
ifikapo Agosti mwaka huu.
“Watumishi wa Sekta ya
Uchukuzi wanaohamia Dodoma katika awamu ya kwanza ni pamoja na Katibu
Mkuu Sekta ya Uchukuzi, Wakurugenzi na Wakurugenzi wasaidizi, wakuu wa
vitengo na maafisa waandamizi”, amesisitiza Dkt. Chamuriho.
Stori na Biseko Ibrahim
No comments :
Post a Comment