Mkuu
wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,akizungumza na watumishi na
mahakimu wa mahakama ya hakimu mkazi Kibaha.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Watumishi,wanasheria
na mahakimu mbalimbali wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi
Evarist Ndikilo,siku ya sheria .(picha na Mwamvua Mwinyi).
………..
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi
Evarist Ndikilo,amezitaka mahakama,polisi na mawakili kutenda haki
kwenye majukumu yao ya kazi pasipo kujihusisha na vitendo vya rushwa
ambavyo vinasababisha mlundikano wa kesi.
Aidha amewataka wapelelezi na
mawakili wa serikali kuzipa kipaombele kikubwa kesi zinazohusisha
waliowapa mimba za utotoni wanafunzi wa kike na unyanyasaji wa watoto
kijumla kwa kutoa adhabu kali ili iwe fundisho.
Mhandisi Ndikilo,amewaasa pia
kuacha kupiga kalenda kesi bila sababu za msingi suala linalisababisha
mashauri na watuhumiwa mahabusu kuchukua muda.
Akizungumza kwenye siku ya sheria
nchini katika viwanja vya mahakama ya hakimu mkazi –Kibaha ,alisema
vitendo vya rushwa ni mwiba unaorudisha nyuma jitihada za serikali
katika kufikia ukuaji wa uchumi.
“Mchakato wa utoaji haki umekumbwa
na changamoto ya baadhi ya watumishi wa umma na wasio wa umma
kujihusisha na vitendo vya rushwa ,ninawasihi mahakimu,watumishi wa
mahakama na wananchi ,kuachana na vitendo hivyo”
Mhandisi Ndikilo,alisema haki ni
msingi mkubwa wa ustawi wa jamii na kwa umuhimu huo ,jamii isiyo
zingatia misingi ya haki kama ilivyoainishwa katika sura (3)ya katiba ya
mwaka 1977,itakumbwa na changamoto nyingi katika kukuza uchumi wake.
Alisema ni wajibu wao kuhakikisha
kuna kuwa na kizazi ambacho kinapata mahitaji muhimu yatakayowajenga na
kuwaandaa vijana kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Hata hivyo alieleza
kwamba,maandalizi hayo ni pamoja na kuhakikisha vijana wanapata fursa ya
kutimiza ndoto zao kwa kuwajengea mazingira rafiki ya kutimiza ndoto
zao kitaaluma.
“Changamoto kubwa kwasasa katika
eneo hili ni baadhi ya watoto wetu waliopo shuleni kupata mimba na hivyo
kukatisha dhamira na malengo yao kimasomo na kimaisha”alisema mkuu huyo
wa mkoa.
Mhandisi Ndikilo,aliviagiza vyombo
vyote vinavyohusika katika mchakato wa kushughulikia wanaowapa mimba
watoto wa shule kuwashughulikia ipasavyo kwa kufuata sheria ili
kukomesha watu wenye tabia za aina hiyo.
Alieleza ,licha ya kutekeleza
wajibu wao kimsingi wa kimahakama katika kutoa haki kwa wakati,lakini
anatambua kuna changamoto zinazowakabili ambazo serikali inazifanyia
kazi.
Alisema serikali ya mkoa
inaendelea kuelekeza wakurugenzi watendaji wa halmashauri kutenga maeneo
kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya mahakama na nyumba za watumishi wa
mahakama kila wanapofanya upimaji kwenye maeneo yao.
Nae hakimu mkazi mwandamizi
mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi,Kibaha Elizabeth Nyembele,alisema
ushiriki wa wadau ni muhimu ili haki itolewe kwa wakati.
Alielezea kuwa kwa ushirikiano
baina ya polisi,vitengo vya asasi zisizo za kiserikali,waendesha
mashtaka,mlalamikaji na mshtakiwa na mdai na mdaiwa unaweza kusaidia
kutoa haki bila ubaguzi na kwa wakati.
Elizabeth alisema itambuliwe
kwamba uwezeshaji wa utoaji haki kwa wakati si wa mahakama pekee bali
kwa wadau wanaohusika kushiriki kikamilifu.
No comments :
Post a Comment