RC akiwa na Mkuu wa Wilaya ya
Kilombero James Ihunyo (aliyevaa miwani) na nyingine akiwemo pia M/kiti
wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara (kulia ) Mashaka Mbilinyi wakiangalia
mbegu za Mpunga zinazofanyiwa utafiti katika kituo cha Utafiti na
mafunzo ya kilimo KATRIN alipokitembelea hapo Februari 21 mwaka huu.
Shamba la mpunga la Kituo cha Utafiti na mafunzo ya Kilimo KATRIN ambalo linalimwa kwa mbegu zinazofanyiwa utafiti.
(picha zote na Andrew Chimesela)
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt.
Kebwe Stephen Kebwe amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya
Kilombero James Ihunyo
kukaa na viongozi wa Halmashauri za Kilombero na Mji wa Ifakara ili
kutafuta njia ya kukitumia vema Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Kilimo
KATRIN kilichopo Wilayani humo ili kuleta mapinduzi ya Kilimo kwa
Halmashauri zake.
Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo
Februari 21 mwaka huu, wakati wa ziara yake Wilayani Kilombero baada ya
kutembelea Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Kilimo KATRIN na kuongea na
Uongozi wa kituo hicho.
Amesema, uwepo wa Kituo cha
Utafiti na Mafunzo ya Kilimo Wilayani humo ni fursa kubwa katika masuala
ya kilimo na hivyo Halmashauri zilizopo katika Wilaya hiyo zinatakiwa
kufanya kila jitihada na kutafuta njia za kufaidi matunda ya chuo hicho
hasa katika kilimo na hivyo kuonesha utofauti na maeneo mengine ambayo
hayana vituo vinavyojishughulisha na kilimo.
Kwa sababu hiyo, amemtaka Mkuu wa
Wilaya ya Kilombero James Ihunyo kuitisha Kongamano la wadau wa kilimo
ngazi ya Wilaya na kuona ni kwa namna gani kituo hicho kinaweza
kuboresha kilimo katika Halmashauri zake mbili za Kilombero na
Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
“DC mimi nakupa maagizo leo,
fuatilia huyo Mkurugezi ili kuona ni kwa vipi anatumia vyuo tulivyo
navyo hapa katika kuleta mapinduzi ya kilimo” Dkt. Kebwe alisema.
Aliongeza kuwa, Kongamano la wadau
wa Kilimo ngazi ya Mkoa limeshafanyika wiki moja iliyopita na kwamba
katika kongamano hilo aliagiza kila Wilaya ifanye Kongamano la wadau wa
Kilimo ngazi ya Wilaya, kwa lengo la kujadili namna ya kuinua uzalishaji
katika Sekta ya Kilimo. Hivyo amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya atumie fursa
hiyo kujadili pia suala la chuo hicho kitakavyoleta mapinduzi ya kilimo
Wilayani humo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa
alimuagiza Kaimu Mkuu wa Kituo hicho Bw. Jerome Mgase, kuwa anataka chuo
hicho kujipanga katika kusaidia Halmashauri za Kilombero na Mji wa
Ifakara na kujielekeza katika eneo la kuinua uzalishaji katika sekta ya
Kilimo.
Ameshauri kuwa wanafunzi wa mwaka
wa pili wanapokaribia kuhitimu na kufanya mazoezi yao wapangiwe Vijiji
au Vitongoji mbalimbali katika Halmashauri hizo ili kulea mashamba
darasa yaliyopo na kuwafundisha wananchi kilimo bora kwa Vitendo.
Dkt. Kebwe amesema, wananchi kwa
sasa wanataka kufundishwa kilimo bora kwa vitendo ili kuona utofauti wa
kilimo cha mazoea walichokuwa wanakitumia siku zote na kilimo bora kwa
kuona uzalishaji wake unaongezeka wakilinganisha na hapo awali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Kilombero James Ihunyo amesema, anayapokea maagizo ya Mhe. Mkuu wa Mkoa,
hata hivyo aefafanua kuwa alishawaagiza wakurugenzi wa Halmashauri
zote mbili kuangalia maeneo ambayo chuo hicho kingeweza kuwasaidia
katika kupata mbegu bora za Mpunga au kuongeza zaidi uzalishaji wa
mazao.
Pamoja na kutekeleza agizo hilo
anasema pia atajikita katika kutatua mgogoro wa muda mrefu uliopo baina
ya chuo hicho na Wananchi zaidi ya 200 ambao inasemekana wengine
wamevamia maeneo ya chuo katika maana ya makazi na wengine kwenye
mashamba ya chuo ili kukaa katika meza moja na kupata suluhisho la
kudumu.
Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya
Kilimo KATRIN (Kilombero Agricultural Training and Reseach Institute)
ambacho kipo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na maendeleo ya Uvuvi,
kipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Wilayani Kilombero,
kilianzishwa mwaka 1963 kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanganyika (kwa
wakati huo) na Ujerumani.
Kituo kilikuwa na jukumu la
kufanya tafiti za mazao mbalimbali yakiwemo ya mahindi, mtama, ulezi,
ufuta, alizeti, minazi na pamba. Mazao mengine ni mikunde, mazao ya
mafuta, mbogamboga na matunda. Mwanzoni mwa miaka ya themanini kituo
kilipewa jukumu la kuratibu utafiti wa mpunga Kitaifa.
Kwa matokeo mazuri yaliyotokana na
kituo hicho, mnamo mwaka 2010, KATRIN ilichaguliwa kuwa kituo mahiri
cha mpunga kwa nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika (Regional Rice
Centre of Excellence – RRCoE) na hadi sasa Kituo kimefanikiwa kufanya
utafiti na kupitishwa kwa mbegu kumi kitaifa.
No comments :
Post a Comment