WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli hajawahi kutangaza ama kutoa kauli
ya kufutwa kwa vyama vya siasa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo (Februari, 2, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati
akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa
Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake Mheshimiwa Mbowe alisema Rais Dkt. Magufuli
alinukuliwa akisema atahakikisha anafuta vyama vyama vya upinzani na
ifikapo mwaka 2020 hakuna upinzani nchini.
Pia Mheshimiwa Mbowe alitaka kujua
nini kauli ya Serikali kuhusu kunyimwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha
Mjini, Mheshimiwa Godbless Lema ambaye anashikiliwa kwa muda miezi
mitatu.
Mbali na Mheshimiwa Lema, pia kiongozi
huyo alitaka kujua kuhusiana na kufungwa kwa Mbunge wa Kilombelo,
Mheshimiwa Peter Lijualikali pamoja na madiwani sita wa chama hicho
ambao wamefungwa na viongozi wengine 215 wanakabiliwa na kesi
mbalimbali.
“Kwanza nataka nikanushe kwamba
Mheshimiwa Rais hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya upinzani. Pia
Watanzania wote wanajua nchi hii inaongozwa kwa sheria, kanuni na
taratibu i,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “tunajua
katika kuendesha nchi tunaendesha kwa mihimili mitatu ipo Serikali,
Mahakama na Bunge na hakuna mhimili unaoweza kuuingilia mhimili
mwingine,”.
“Pia Watanzania wote wanajua kwamba
jambo lolote ambalo lipo Mahakamani haliwezi kuzungumzwa mahali pengine
popote, hivyo siwezi kutumia nafasi hii kuzungumzia mambo yote
yanayoendelea chini ya sheria na yaliyo mahakamani,” amesema.
Wakati huo huo; Waziri Mkuu
amewahakikishia Watanzania kwamba suala la upungufu wa sukari
halitatokea nchini kwa sababu viwanda vya ndani vinaendelea kuzalisha na
hadi mwishoni mwa Januari vilifikia asilimia 86 ya uzalishaji.
“Hadi kufikia mwishoni mwa msimu wa
uzalishaji ambao ni mwezi Machi, tunaweza kuwa tumefikia malengo na kama
itajitokeza upungufu Serikali itatafuta namna nzuri ya kupata sukari
kwa kushirikiana na wenye viwanda nchini,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati
akijibu swali la Mbunge wa Mvomero, Mheshimiwa Suleiman Sadiq aliyetaka
kujua hali ya sukari ilivyo nchini kwa sasa na hatua gani
zinazochukuliwa na Serikali ili kunusuru hali ya uhaba wa sukari
isijitokeze.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
- L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMIS, FEBRUARI 02, 2017
No comments :
Post a Comment