Sunday, February 12, 2017

KATIBU TAWALA WA MKOA WA MOROGORO AAGIZWA KURATIBU VIKUNDI VYA MAZOEZI


chime1Mbunge wa Morogoro Mjini Mohamed Abood Azizi (mwenye mavazi mekundu mbele) akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe (kushoto kwake)  wakiongoza mamia ya watu waliofiki kushiriki mazoezi ya mwili.
chime2Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (mwenye Truck rangi ya bluu)  akiwa katika mazoezi  mepesi Uwanja wa Jamhuri  Mjini Morogoro siku ya Jumamosi  ya Februari 11,2017. Kushoto kwake ni Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini  Mohamed Abood Azizi, na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo.
chime3Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Urich Matei (katikati) akiwa na viongozi wengine wa majeshi ya magereza Mkoani humo wakitembea kwa ukakamavu wakati wa mazoezi ya pamoja Februari 11 mwaka huu.
……………………………………………………………………….
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Dkt. John Ndunguru kuratibu vikundi vingine vya mazoezi na wananchi wengine
Mkoani Morogoro kujiunga na mazoezi ya viungo yanayofanyika kila Jumamosi ya pili ya kila mwezi kwa lengo la kuimarisha Afya zao.
Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki hii muda mfupi kabla Mkuu huyo kuongoa mamia ya watu kutoka Taasisi za Umma na watu binafsi waliofika kushiriki mazoezi hayo na Mkuu huyo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kufanya pamoja mazoezi ili kulinda Afya zao.
Dkt. Kebwe alisema, mazoezi hayo hayakuanzishwa kwa ajili ya watumishi wa umma pekee bali kwa ajili ya wananchi wote na lengo lake ni kupunguza magonjwa yasiyoambukizwa kwa wanannchi wote  na kumuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kuendelea kuratibu ili kuvipata vikundi au watu wengine kujiunga na mazoezi hayo.
“Lakini RAS, suala hili lifuatiliwe, kwa mujibu wa waraka kutoka kwa Makamu wa Rais Makatibu Tawala wa Mikoa ndio wenyeviti wa shughuli hii ya michezo kwa Mkoa mzima”, Dkt. Kebwe alisema. “kwa hiyo Mwenyekiti, tafadhali simamia ili watu wengine waendelee kuratibiwa kwa kuwa mazoezi haya siyo kwa ajili ya watumishi wa umma tu bali kwa watu wote” alisisitiza
Pamoja na wito huo Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro ameitahadhalisha jamii kuwa magonjwa yasiyoambukizwa yanapanda kwa kasi hapa nchini na dawa pekee ya kutibu magonjwa hayo ni kufanya mazoezi. Ameyataja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, kiharusi, magonjwa ya moyo saratani n.k.
Awali kabla ya kuanza mazoezi hayo Mkuu wa Mkoa aliwashukuru wote waliofika kushiriki michezo na kwamba ameridhika na mwitikio huo huku akitaka watu wengi zaidi waendelee kuitikia wito wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kuungana kufanya mazoezi ya pamoja kila Jumamosi ya pili ya kila mwezi.
Mazoezi hayo yaliyoanzia katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kuishia Uwanja wa Jamhuri uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoroa yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa huo akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa Mhandisi Daktari John Nunguru, Kamanda wa Polisi wa  Mkoa Urich Onesphori Matei, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo na Mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Mohamed Abood Azizi.

No comments :

Post a Comment