Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Bunge la Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha muswada wa sheria ya marekebisho
ya sheria mbalimbali (Na. 4) wa mwaka 2016 [The written laws
miscellaneous Amendments (No. 4) Bill, 2016].
Akiwasilishwa muswada huo Bungeni,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema kuwa muswada huo
unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria Sita ambapo lengo la
marekebisho yanayopendekezwa ni kurahisisha utekelezaji wa Sheria hizo
kwa kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa kutumia masharti ya sheria
hizo.
Masaju alizitaja sheria
zilizopendekezwa kufanyiwa marekebisho kupitia muswada huo kuwa ni
Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana, Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu
ya Juu, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Sukari na
Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori.
“Ibara ya 21 ya muswada
inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 30 cha Sheria ambacho
kinaweka masharti kuhusu Waziri mwenye dhamana ya fedha kukasimu
madaraka yake chini ya Sheria hiyo. Sheria ilivyo sasa inaelekeza kuwa
Waziri anaweza kukasimu mamlaka yake ya kujadili mkopo (negotiating
loan), kuingia makubaliano ya kukopa mkopo na kutoa dhamana,” alifafanua
Masaju.
Aliendelea kwa kusema kuwa muswada
unapendekeza kuwa Waziri awe na uwezo wa kukasimu pia mamlaka ya
kujadili au kuingia makubaliano ya misaada kwa mamlaka au mtu mwingine.
Lengo la marekebisho hayo ni kurahisisha taratibu za upokeaji misaada
kwa kuwa sheria hiyo ilikuwa kimya kuhusu suala hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge la Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa
alipokuwa akitoa maoni na ushauri wa kamati hiyo alisema kuwa, kamati
hiyo inaunga mkono marekebisho ya Sheria ya Mkopo wa Elimu ya Juu kwa
sababu itatoa nafasi kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini kupata
nafasi ya kusoma katika Vyuo vya Elimu ya Juu.
Aidha ameeleza kuwa, kamati
inakubaliana na mtazamo wa Serikali kwamba utoaji wa Mikopo ya Elimu ya
Juu kwa ajili ya ngazi ya Diploma utazingatia vipaumbele vya Taifa
kulingana na wakati husika.
Nae, Mbunge wa Karagwe, Innocent
Bashungwa amesema kuwa muswada huo umelenga kusaidia Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupata mikopo yenye riba nafuu.
Vile vile muswada huo unapendekeza
marekebisho katika sheria ya Wanyamapori kuwa, katika hatua yoyote ya
kesi ya Mahakama inaweza kwa kuamua yenyewe au kwa maombi ya upande wa
mashtaka kutoa amri kuwa mnyama, nyara ya Serikali, silaha, gari au kitu
chochote kilichotolewa kama ushahidi ambacho kinaweza kuharibika au
kupoteza thamani kiuzwe au kiharibiwe na Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia muswada huo unapendekeza
kuongezwa kifungu kipya kitakachoweka masharti kuhusu bei elekezi ya
miwa, sukari na bidhaa nyingine zitokanazo na miwa.
Mwenyekiti, Mhe. Najma Giga
alitangaza rasmi kupitishwa kwa muswada huo na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania baada ya kupata kura nyingi za ndio. Aidha muswada
huo unasubiri kibali cha Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili uanze
kutumika kama sheria.
No comments :
Post a Comment