Sunday, January 29, 2017

SERIKALI YALAANI VIKALI MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUENDELEA KUCHOCHEA MGOGORO WA PORI TENGEFU LA LOLIONDO 01

01
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Waandishi wa habari jana  mjini Dodoma,  kuhusiana na  uchochezi unaofanywa na Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Loliondo na Ngorongoro ya kuwahimiza wananchi kuchunga, kulima na kukata miti katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo hali inayochangia kukausha  vyanzo maji yanayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
02
Kundi la mifugo likiwa ndani ya Pori Tengefu la Loliondo, karibu kabisa na mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inalaani vikali uchochezi unaofanywa na Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Loliondo na Ngorongoro ya kuwahimiza wananchi kuchunga, kulima na kukata miti katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo hali inayochangia kukausha  vyanzo maji yanayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana  mjini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema maelfu ya mifugo  kutoka nchi jirani ya Kenya imekuwa ikiingizwa  ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti muda wa saa 11 jioni,
Amesema katika kukabiliana na changamoto ya uharibu wa chanzo kikuu cha maji ya Serengeti kwa asilimia 47.2 ya maji yote, tayari mifugo 1700 imeshakamatwa
Mbali na mifugo  hiyo, Waziri Maghembe alisema kuwa maelfu ya Matrekta ya kutoka nchini Kenya yameletwa kulima katika maeneo yanayopakana na Serengeti
Aliongeza kuwa  hivi karibuni kilimo kimeshamiri ambapo kipindi cha nyuma wakazi  walikuwa wanalima na ng’ombe (maksai) ila sasa matrekta ya Kenya yanalima na kufungua mashamba makubwa.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Maghembe ameagiza kuwa raia wa Kenya wenye  mifugo  Loliondo warudi makwao mara moja, Mkoa na Wilaya uchukue hatua kuwaondoa mara moja
Pia, Matrekta yote ya nchi ya Kenya yawe na usajili wa kodi (Tax Clearance) toka TRA au yarudi kwao mara moja
Aidha, ameagiza kuwa  eneo la 1,5002km liwekewe alama mara moja na uwekaji alama ukamilike ifikapo  tarehe 30 Machi, 2017.
Kwa upande wa Utalii, Ameziagiza kampuni zote za utalii ambazo hazina usajili wa kitaifa zinazofanya biashara kwa mikataba ya vijiji ziripoti Wizarani ndani ya siku saba, Ikiwa pamoja na kuonyesha usajili wao, kuonyesha vitalu walivyopewa na Serikali pamoja kuiridhisha Serikali kama wanalipa kodi.
Awali, akizungumzia kuhusu mgogoro huo wa Pori Tengefu la Loliondo, Waziri Maghemba alisema anatambua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo  anasimamia mazungumzo ya wadau wote ili kuleta utatuzi wa mgogoro huo.
‘’Nimeambiwa kuwa mwelekeo wa mazungumzo ni mzuri nahimiza mazungumzo yaendelee, lakini  nimeona  nikingoja hadi mazungumzo hayo  yaishe Hifadhi ya Taifa ya Serengeti  itakuwa haipo.’’ alisisitiza

No comments :

Post a Comment