Dodoma, Jumatatu, Januari 30, 2017: Katika toleo la Jumatatu, Januari 30-Februari 5, 2017 gazeti la MwanaHALISI
linalochapishwa na kampuni ya Hali Halisi Publishers LTD kumechapisha
habari kuu katika ukurasa wa kwanza inayosomeka “Ufisadi ndani ya ofisi
ya JPM.”
Licha ya habari hiyo kujenga
dhana kuwa Rais John Pombe Magufuli anahusika na kilichoitwa ufisadi,
msingi wa taarifa husika ni tatizo la manunuzi katika Shirika la Elimu
Kibaha!
Kwa kuwa ni jambo lililodhahiri
kuwa Shirika la Elimu Kibaha si ofisi, idara wala kitengo “ndani ya
ofisi ya JPM” mwandishi na mhariri wa habari husika wamedhihirisha
malengo ya kumchafua Rais binafsi kwa jamii.
Aidha, katika siku za karibuni
Serikali imejitahidi kufanya mazungumzo na wahariri wa gazeti hili kwa
lengo la kukumbushana maadili ya uandishi wa habari, ni bahati mbaya
kwamba wamekuwa wakikaidi japo wito tu.
Kwa sababu hizi, Serikali inawaagiza wahariri wa gazeti hilo kujitathmini na kuchukua hatua kwa kutumia kifungu cha 40 cha Sheria ya Huduma za Habari, 2016 kinachowapa fursa ya kuomba radhi, kwa kumuomba radhi Rais ndani ya saa 24 kuanzia saa 10 jioni ya leo Januari 30, 2017.
Iwapo wahusika wataona muhali
kufanya hivyo, Serikali itachukua hatua kali kwa mujibu wa sheria na
masharti ya usajili ya gazeti husika. Tunaendelea kuwashukuru wanahabari
wanaofuata maadili ya taaluma.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO
No comments :
Post a Comment