Tuesday, January 31, 2017

Bil. 2,570.1 Zalipia Madeni ya Ndani na Nje


indexNa;  Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia Desemba, 2016 Serikali imetumia jumla ya shilingi Bil. 2,570.1 kulipia madeni ya ndani na nje yaliyoiva.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango aliyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi wa Taifa.

“Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia Desemba, 2016 Serikali ilitumia jumla ya shilingi Bil. 2,570.1 kulipia madeni ya ndani na nje yaliyoiva. Kati ya kiasi hicho malipo ya deni la ndani ni shilingi Bil. 1,822.3 na deni la nje ni shilingi Bil. 747.8 ,” alifafanua Dkt. Mpango.
Ameeleza kuwa katika malipo ya deni la ndani yanajumuisha malipo ya mtaji (rollover) ya shilingi Bil. 1,367.1 na malipo ya riba ya shilingi Bil. 455.2.
Aidha Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kupeleka fedha katika Halmashauri  kwa kuwa ndiko utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi yanapofanyika.
Hivyo basi, katika robo ya kwanza ya mwaka 2016/2017, Serikali ilipeleka jumla ya shilingi Bil. 114.7  kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Aidha, katika robo ya pili ya mwaka, Serikali iliongeza mgao wa fedha zilizoenda kwenye Halmashauri ambapo kiasi cha shilingi bilioni 203.4 zilipelekwa.
Dkt. Mpango alitaja madai mengine yaliyolipwa na Serikali katika kipindi cha kufikia Juni 30, 2016 kuwa ni kiasi cha Shilingi Bil. 3,113.7 ambazo ziliwasilishwa ikiwa ni madai ya wakandarasi, watumishi, wazabuni na watoa huduma mbalimbali.
Serikali ilifanya uhakiki kupitia kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ilibainika kuwa madai halali yalikuwa shilingi Bil. 2,934.2 na madai yaliyokosa vielelezo na hivyo kukosa uhalalli yalikuwa shilingi Bil. 179.5.
Vile vile katika kipindi cha nusu mwaka wa 2016/17, Serikali imelipa jumla ya shilingi Bil. 600.2 ambapo kati ya kiasi hicho, shilingi Bil. 42.35 zilikuwa kwa ajili ya madai ya watumishi, shilingi Bil. 49.46 kwa ajili ya wazabuni, shilingi Bil. 11.2 kwa ajili ya watoa huduma, shilingi Bil. 30.0 kwa ajili ya madai ya vyombo vya Ulinzi na Usalama, shilingi bil. 67.2 kwa ajili ya wakandarasi mbalimbali ikijumuisha shilingi Bil. 2.0 kwa ajili ya makandarasi wa maghala na skimu za maji.

No comments :

Post a Comment