Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwapungia wananchi wa Ruangwa wakati alipowasili kwenye uwanja wa
Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo kuhutubia mkutano wa hadhara Desemba 30,
2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia Mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Ofisi ya CCM ya wilaya ya Ruangwa Desemba 30, 2016.
Baadhi ya wananchi wa mji wa
Ruangwa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia
mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo mjini
Ruangwa Desemba 30, 2016.
Baadhi ya wananchi wa
kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa wakigalagala kuonyesha furaha
katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
kwenye uwanja wa Ofisi ya CCM ya wilaya ya Ruangwa, Desemba 30, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea zawadi ya mkeka kutoka kwa wananwake wa Ruangwa katika mkutano
wa hadhara aliouhutubia kwenye uwanja wa Ofisi ya CCM ya wilaya ya
Ruangwa Desemba 30, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amelazimika kuendesha harambee ya papo kwa papo ma kuchangisha
sh.milioni 138.26 ili kufanikisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari
wilayani Ruangwa.
Hatua hiyo hiyo inafuatia wingi
wa wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kuingia
kidato cha kwanza lakini hawakufanikiwa kupata nafasi katika mkupuo wa
kwanza.
“Katika kikao cha Halmashauri ya
Wilaya cha hivi karibuni ilionekana kuna haja ya kujenga shule mpya ya
sekondari ili kukabiliana na wingi wa watoto waliofaulu mtihani wa
darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza. Tunawashukuru
sana wenzetu ambao wametoa maeneo yao bure ili shule ijengwe haraka,”
amesema.
Katika harambee iliyofanyika
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ruangwa leo mchana (Ijumaa,
Desemba 30, 2016), Waziri Mkuu amefanikisha kupatikana kwa fedha kiasi
cha sh. milioni 120.65 na mifuko 550 ya saruji na mabati 360 (vyenye
thamani ya sh. milioni 17.61) ambavyo vitatumika kujenga madarasa manne
ya kidato cha kwanza yanayotakiwa kuwa yamekamilika ifikapo Januari 15,
2017.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue, jumla ya watoto 319
walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini walikosa nafasi
sababu ya ukosefu wa madarasa na walitakiwa kusubiri hadi chaguo la pili
ambalo kwa kawaida hufanyika Februari, kila mwaka.
“Wanafunzi waliofaulu na kukosa
nafasi jumla yao ni 319 lakini kwa hapa Ruangwa mjini ni 179 na
waliobakia 140 wanatoka kwenye kata za jirani za Nachingwea na
Mandarawe. Shule hii ya sekondari itahudumia kata tatu. Kwa hiyo
Halmashauri imepanga kujenga madarasa manne hapa mjini ili watoto wote
waweze kuanza mara moja,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema ili
kupunguza tatizo hilo mwakani, wataendeleza ujenzi wa madarasa manne
manne waweze kuwa na mikondo minne kwa kila kidato. “Halmashauri ya
Ruangwa imetenga sh. milioni 75, wananchi wa Kata ya Ruangwa wametoa sh.
milioni 1.2 na wananchi wa kata ya Nachingwea wametoa sh. milioni
2.25,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa
jimbo hilo, amechangia sh. milioni 33 kutoka kwenye mfuko wa jimbo ili
kuharakisha ujenzi wa madarasa mawili ya kuanzia. Wengine waliochangia
harambee hiyo ni kampuni ya Paco Gems Ltd, (sh. milioni 6), Baraka Solar
(sh. milioni moja), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (sh. milioni 1), Kampuni ya
Asamalema (sh. milioni 1) na mfanyabiashara wa Ruangwa, Bw. Abdallah
Namkudai (sh. 200,000).
Wengine ni kampuni ya wanyumbani
construction mifuko 100 ya saruji, kampuni ya Lindi Jumbo (mabati 100 na
mifuko 100 ya saruji), kampuni ya madini ya Nazareth (mifuko 150 ya
saruji), kampuni ya URANEX inayochimba madini ya Graphite (mabati 260),
mgodi wa dhahabu wa Namungo (mifuko 100 ya saruji) na Kampuni ya ujenzi
ya Nahungo Construction Ltd. (mifuko 100 ya saruji).
Waziri Mkuu amewashukuru wote waliojitolea kuchangia ujenzi wa shule hiyo. Amerejea jijini Dar es Salaam jioni hii
No comments :
Post a Comment