Friday, December 2, 2016

VIWANDA VYA UZALISHAJI VYATENGENEZA AJIRA 16000

picc
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage  akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu ongezeko la wawekezaji nchini katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
……………………………………..
             Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
JUMLA ya ajira 16,671 zimetengenezwa na viwanda vya uzalishaji nchini ambapo viwanda vya wawekezaji kutoka nje ya nchi vikiongoza kwa utoaji wa ajira hizo.
Takwimu hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu ongezeko la wawekezaji nchini kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Waziri Mwijage amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inafanya juhudi za kuwahamasisha wawekezaji ili waweze kushiriki katika kuchochea mageuzi ya kiuchumi hivyo imeanza kupunguza uuzaji wa malighafi nje ya nchi ikiwa ni njia mojawapo ya kuwavutia wawekezaji kuwekeza nchini.
”Katika kujenga uchumi wa viwanda, tunalenga kujenga uchumi shirikishi na ulio endelevu ambao utahusisha watu wengi hivyo utaratibu wa aina hiyo utawasaidia kuwainua wananchi kiuchumi pamoja na kukuza pato la taifa,” alisema Mwijage.
Kwa mujibu wa Mwijage ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, takwimu zinaonyesha kuwa kuna ongezeko la uwekezaji katika sekta za ujenzi wa majengo, maliasili, rasilimali watu, viwanda vya uchakataji bidhaa, sekta ya nishati, kilimo, huduma, usafiri pamoja na mawasiliano.
Aidha, amezitaja sekta zingine za uwekezaji ambazo zinaongoza kwa uzalishaji wa ajira kwa wingi kuwa ni majengo ya biashara ambayo yanazalisha ajira 5537, sekta ya utalii ajira 2011 pamoja na sekta ya huduma inayozalisha jumla ya ajira 680.
Akizungumzia kuhusu ubora wa makaa ya mawe, Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini, John Shija amesema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na makaa ya mawe ya kutosha ya kuweza kuchimbwa na kutumiwa kwa zaidi ya miaka 200.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhandisi wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda, Mhandisi Lugano Wilson amesisitiza kuwa kati ya nchi zinazozalisha makaa ya mawe zikiwemo za India, China na Afrika ya Kusini, nchi ya Tanzania ndiyo inayoongoza kwa kuwa na makaa ya mawe yenye ubora unaokubalika.
MWISHO

No comments :

Post a Comment