Washindi wa kwanza wa masuala
ya kodi katika mashindano ya vilabu vya kodi kutoka shule ya
Sekondari Loyola wakifurahia ushindi mara baada ya kutangazwa kuwa
washindi.
Washindi wa kipengele cha
uwasilishaji wa mada kutoka shule ya sekondari ya Shaaban Robert katika
picha ya pamoja na Mwalimu wao kutoka TRA Bw. Patrick Massawe (mwenye
tisheti ya njano) mara baada ya kutangazwa washindi katika mashindano
yaliyofanyika tarehe 2 Disemba 2016 jijini Dar es Salaam.
Mshindi bora katika kipengele
cha kujibu maswali kwa umahiri, Adamson Nsimba kutoka shule ya
sekondari St. Joseph mara baada ya kutangazwa mshindi. Adamson
amezawadiwa kompyuta mpakato (haipo pichani) .
Mwanafunzi Nabila Omary
(kulia) kutoka shule ya Sekondari Loyola akiwasilisha mada ya Kodi ya
Mapato Yatokanayo na Ajira (PAYE) wakati wa mashindano ya vilabu vya
kodi katika shule za Sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani
yaliyofanyika Tarehe 02 Disemba 2016 katika ukumbi wa shule ya Shaaban
Robert Jijini Dar es Salaam. Wapili kulia ni Devotha Aloyce pamoja na
Christina Mbawala walioshirikiana nae kutoa mada hiyo.
Meneja wa Huduma kwa
Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Honesta Ndunguru
ambaye ni Mratibu wa Vilabu vya Kodi Tanzania akitambulisha kwa mgeni
rasmi shule zilizoshiriki mashindano ya vilabu vya kodi kutoka Mkoa wa
Dar es Salaam na Pwani yaliyofanyika Tarehe 02 Disemba 2016 katika
shule ya Shaabani Robert Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya wanafunzi
walioshiriki shindano la vilabu vya kodi kutoka shule za sekondari za
Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wakiwasikiliza kwa makini wanafunzi
wenzao wakiwasilisha mada za kodi wakati wa mashindano ya vilabu vya
kodi kwa shule za Sekondari yaliyofanyika Tarehe 02 Disemba 2016 katika
shule ya Shaabani Robert Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya wanafunzi
walioshiriki shindano la vilabu vya kodi kutoka shule 47 za sekondari za
Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani lililofanyika Tarehe 02 Disemba 2016
katika ukumbi wa shule ya Shaabani Robert Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu
kwa Mlipakodi TRA Bw. Richard Kayombo akitoa ufafanuzi wa shindano la
vilabu vya kodi mashuleni kwa vyombo vya habari baada ya kufungua rasmi
shindano la vilabu vya kodi kwa shule za sekondari Mkoa wa Dar es Salaam
na Pwani.
……………………………………………………………………………….
Shule ya Sekondari Loyola
imeibuka mshindi wa mashindano ya vilabu vya kodi mwaka 2016 na
kujinyakulia zawadi ya Televisheni ya Inchi 40, Kompyuta ya mezani
pamoja na Printa moja baada kuonesha uwezo wa hali ya juu katika kujibu
maswali ya kodi wakati wa mashindano ya vilabu vya kodi yaliyofanyika
katika ukumbi wa shule ya Sekondari Shaaban Robert Jijini Dar es Salaam.
Nafasi ya pili katika mashindano
hayo imeshikwa na shule ya Sekondari Kibaha ambayo ilizawadiwa Kompyuta
ya mezani na Printa wakati shule ya Sekondari ya St. Joseph imekuwa
mshindi wa tatu na kupatiwa Kompyuta ya mezani.
Zawadi ya shule iliyowasilisha
mada bora ya kodi ilinyakuliwa na shule ya Sekondari Shaaban Robert
ambapo mwanafunzi Adamson Nsimba kutoka shule ya Sekondari St. Joseph
ameibuka mwanafunzi bora na kuzawadiwa Kompyuta mpakato.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na
kuratibiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalizishirikisha shule
za sekondari 47 kutoka katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa lengo
la kupima uelewa wa masuala ya kodi miongoni mwa wanafunzi ikiwa ni
mkakati wa kujenga uzalendo na uhiari wa kulipa kodi kupitia shule za
sekondari kwa kuwajengea uwezo wa kuwa walipakodi wa baadae.
Kati ya shule hizo zilizoshiriki,
jumla ya shule 18 zilishindana katika kuwasilisha mada mbalimbali za
kodi baada ya kuibuka washindi katika mashindano ya awali yaliyofanyika
Tarehe 26 Novemba 2016 katika Chuo cha Kodi (ITA) ambayo yalishirikisha
shule 46 za Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Mada ambazo ziliwasilishwa na
kushindanishwa katika shindano hilo ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT), Mashine za Kielektroniki za Kodi (EFD’s) na Utunzaji wa
Kumbukumbu za Biashara; Uingizaji wa Bidhaa Nchini na Uuzaji wa Bidhaa
Nje ya nchi; Mifumo ya Ulipaji Kodi na Kodi ya Mapato Yatokanayo na
Ajira (PAYE).
Mada nyingine zilizowasiliswa
katika mashindano hayo ni Uboreshaji wa Mifumo na Utawala wa Kodi
Tanzania, Kodi ya Mapato Yatokanayo na Rasilimali na Mapato yatokanayo
na Biashara.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa
mashindano hayo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA Bw.
Richard Kayombo alisema, mashindano hayo ya vilabu vya kodi kwa shule za
Sekondari yalianza kufanyika baada ya kuzinduliwa vilabu vya kodi
katika shule za Sekondari mwaka 2008 ili kukuza uelewa wa masuala ya
kodi kwa wanafunzi na kuongeza hamasa ya ushiriki wa mashindano hayo.
“Tayari TRA imezindua jumla ya
vilabu vya kodi katika shule za Sekondari 220 za Tanzania Bara na
Visiwani zikiwa na wananfunzi wanachama 16,620”. Alisema Bw. Kayombo
Bw. Kayombo amesema TRA
itaendelea kusaidia vilabu vya kodi kadri inavyoweza kwani kupitia
vilabu vya kodi Taifa linapata vijana wenye uelewa wa kodi ambao
wanakuwa mabalozi wazuri wa masuala ya kodi na hivyo kupata taifa lenye
uelewa wa masuala ya kodi na kujijengea utamaduni wa kulipa kodi.
Kwa upande wake Mratibu wa vilabu
vya kodi Tanzania ambaye ni Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi TRA Bi.
Honesta Ndunguru alisema pamoja na kuzindua vilabu vya kodi katika shule
za sekondari; TRA pia imepanua wigo wa vilabu hivyo kwa kuanzisha
Jumuiya za Kodi kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambao kwa pamoja na shule za
Sekondari watakuwa mabalozi wazuri wa masuala ya kodi mashuleni, vyuoni
na katika jamii kwa ujumla.
Mwanafunzi bora Adamson Nsimba
ametoa wito kwa wanafunzi wote kujiunga na vilabu vya kodi ili wapate
uelewa wa masuala ya kodi na hivyo kujijengea utamaduni wa kulipa kodi
kwa hiari.
No comments :
Post a Comment