WAZIRI wa Biashara, Viwanda na
Masoko Balozi Amina Salum Ali ameutaka uongozi wa CocaCola kufikiria
kurejesha uzalishaji katika kiwanda cha Maruhubi na Serikali imeandaa
mikakati ya kuvilinda viwanda vya Zanzibar ili wananchi wafaidike kupata
ajira.
Amesema miongoni mwa mikakati
hiyo ni kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa Zanzibar kutoka nje
zinalipiwa ushuru unaostahiki na kudhibiti mbinu za wafanyabiashara za
kukwepa kulipa kodi.
Balozi Amina ameeleza hayo
alipofanya ziara ya kutembelea Kiwanda CocaCola Maruhubi ambacho
kinaendelea kusambaza soda zinazozalishwa Dar es salaam kufuatia kiwanda
hicho kusitisha uzalishaji kwa muda mrefu sasa.
Amesema kitendo cha kusitisha
uzalishaji wa soda katika Kiwanda cha Maruhubi kinawanyima fursa
wananchi wengi kutoa mchango wao na ni kinyume cha sera ya kuwa na
viwanda venye tija.
Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha
CocaCola Zanzibar na Tanzania Bara Ndugu Haji Ali amemueleza Waziri
Amina wamelazimika kusitisha uzalishaji Zanzibar kutokana na ushindani
uliopo wa bidhaa hiyo kutoka nje bei yake kuwa chini kutokana na
kuingizwa bila kulipiwa ushuru.
Ametaja sababu nyengine kuwa ni
uchakavu wa mitambo ya uzalishaji iliyokuwa ikitumika imepitwa na wakati
na haiendani na teknolojia ya usazalisha wa sasa.
Hata hivyo amesema Kiwanda cha
CocaCola Zanzibar kimeongeza mauzo ya bidhaa za aina tofauti za soda
zinazozalishwa Tanzania Bara kwa asilimia 40.
No comments :
Post a Comment