Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
SERIKALI kupitia Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi imesema kuwa imeandaa mikakati mbalimbali ili
kuhakikisha Sekta ya Kilimo inatoa mchango zaidi katika kufikia nchi ya
uchumi wa kati.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam
jana katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoandaliwa kwa ushirikiano wa
Idara ya Habari – MAELEZO na kituo cha televisheni cha TBC, aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ambaye sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya
Ulinzi Dkt. Florence Turuka alisema kuwa Serikali imeandaa mikakati hiyo
ili kuhakikisha kunakuwepo na uzalishaji wa mazao ya kilimo ili viwanda
viweze kupata malighafi, chakula cha kutosha pamoja na ajira kwa
wananchi.
“Serikali imeamua kuanzisha
viwanda vidogo vya kuchakata mazao kwa ajili ya soko, kushirikisha sekta
binafsi katika kuongeza thamani ya mazao, ili kuvutia wakekezaji katika
sekta ya kilimo nchini” alisema Dkt. Turuka.
Kwa mujibu wa Dkt. Turuka alisema
ili kuhakikisha huduma za ugani zinakua za kisasa Serikali
inadhamiria kutumia simu za mkononi zitakazorahisisha utoaji wa taarifa
kwa wataalamu wa kilimo, ikiwa ni pamoja na kusaidia wakulima kupata
huduma za kitaalamu kwa wakati.
Aidha Dkt. Turuka alisema
mikakati mingine inayotekelezwa na Serikali ni pamoja na kuongeza idadi
ya matrekta hadi kufikia 6,000 badala ya 400 yaliyokuwepo awali.
Aliongeza kuwa Serikali
imekusudia pia kujenga maghala karibu na maeneo yanayozalisha mazao ya
matunda na mbogamboga ili kuweza kuyahifadhi kwa muda kabla mazao hayo
hayajapekelekwa sokoni ili kupunguza uharibifu.
Naye Katibu Mkuu wa sasa wa
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Mathew Mtigumwe alisema
Serikali itaboresha mfumo wa takwimu wa wataalamu wa kilimo pamoja na
kuwajengea uwezo ili kusaidia utekelezaji wa maendeleo ya kilimo katika
maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali inawakaribisha
wawekezaji wa kilimo cha miwa ambapo imeandaa zaidi ya hekta 6000 kwa
ajili ya kilimo hicho nchini.
No comments :
Post a Comment