Judith Mhina – MAELEZO
- SERA YA VIWANDA ITATUKOMBOA
Katika kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa
Tanganyika Idara ya Habari – MAELEZO ilipata fursa ya kufanya mahojiano
na Mwanasiasa na mwana Diplomasia Balozi Christopher Liundi kuhusiana
na maadhimisho hayo. Yafuatayo ni maswali na majibu katika mahojiano
hayo:
SWALI: Mheshimiwa Balozi Tanzania imetimiza miaka 55 ya Uhuru una lipi la kuwaeleza Watanzania?
JIBU: Kwa mtazamo wangu nina mambo matatu
muhimu ninayoayaona katika hii miaka 55 ya Uhuru. Jambo la kwanza lazima
tutambue na tuone fahari kwa nchi yetu kufikisha miaka 55, bila kuwepo
na machafuko yalliyosababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Katika
miaka 55 tumeweza kujitawala kwa amani na utulivu kutokana na viongozi
wetu kuwa na busara na kutongangania madaraka kama ilivyo kwa nchi
nyingine barani Afrika.
Pili, tumeweza kupiga hatua kubwa
kimaendeleo katika nyanja mbalimbali kama vile elimu, afya, miundombinu ,
uchukuzi na viwanda. Katika elimu kwa mfano wakati wa ukoloni kulikuwa
na shule za Wazungu, Wahindi na Waafrika lakini sasa, watoto wote
wanasoma bila kujali kama ni Mzungu Mhindi au Mwafrika.
Mwisho, nakumbuka mara baada ya Uhuru
tukaja na sheria zetu, baraza letu la mawaziri na maamuzi yetu wenyewe.
Misingi hiyo tumeidumisha na kuridhisha kwa vizazi vya sasa na vizazi
vijavyo Yapo mambo mengi ambayo tunaweza kukumbuka ambayo hayakuwa
mazuri lakini la muhimu ni lazima ukisema uhuru umkumbuke Baba wa Taifa
Hayati Mwalimu Julius Kambarage. Nyerere ambaye alitumia muda wake
wote, uwezo wake wote pamoja na waasisi wa TANU kuhakikisha nchi hii
inakuwa huru.
SWALI: Mheshimiwa Balozi wewe ni kati ya
watu waliobobea katika siasa na Diplomasia za nchi na umefanya kazi na
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Unadhani muelekeo
tulionao mpaka sasa unaleta hali halisi ya nchi huru katika miaka 55 ya
Uhuru?
JIBU: Muelekeo ni mzuri tena madhubuti.
Umeleta matumaini makubwa mno kutokana na kuweza kuendelea na Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar, lakini pia huduma zinazotolewa na serikali
yetu kwa wananchi kukua, kuimarika na kuboreshwa zaidi.
Pili kuna hali ya amani inayowafanya watu
washiriki katika kujenga uchumi na kujiletea maendeleo. Mfano kuweka
miundombinu ili kukuza uchumi ambapo barabara zimejengwa nchi nzima kwa
kuunganisha Mikoa na Mkioa, Wilaya na Wilaya na sasa tunaelekea
kuunganisha Tarafa Kata na hatimaye vijiji. Hii ni dalili nzuri ya
maendeleo na kukua kwa uchumi.
Tatu , kuongezeka kwa wataalam wetu
wenyewe katika taaluma mbalimbali ambapo wakati tunapata uhuru tulikuwa
na wataalamu wachache sana, sina takwimu lakini sasa Mtanzania anaweza
kuongoza meli, ndege, kuchimba madini na kutengeneza barabara. Nani
alitegemea Mtanzania atatengeneza barabara hapa nchini? Nani alidhani
mtanzania anaweza kurusha ndege? Nani alidhani Mtanzania naweza kuchora
mchoro wa majengo marefu tuliyonayo hivi leo.
Haya yote yanaonyesha kwamba muelekeo wetu
unaleta matumaini na uko sahihi. Tumpe Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu
ya Tano ushirikiano ili aweze kutimiza ndoto zetu.
SWALI: NIni maoni yako kuhusu nchi muelekeo wa nchi kwenye uchumi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa?
JIBU: Tukubali kuwa uchumi ndio msingi wa
maendeleo wa Taifa lolote. Sera zinazoandaliwa ni lazima zilenge katika
kuleta maendeleo ya nchi kiuchumi. Rais anaposema anataka Taifa
liondokane na umasikinini ni kweli tutaondokana nao, kama tutakuwa na
viwanda vidogo vya kati na vikubwa. Kutokana na viwanda watu watapata
ajira Wakulima watapata sokola uhakika la mazao yao na bidhaa
zitakazozalishwa zitauzwa ndani na nje ya nchi kwa kuwa zimeongezewa
dhamani.
Watanzania tumekuwa na tatizo la kuthamini
vitu vinavyotoka nje. Mfano mzuri ni China ambao viwanda vyao
vilianza kuzalisha bidhaa ambazo zilitumika nchini mwao hadi
kujitosheleza. Hivi sasa nchi hiyo imepata soko kubwa la nje na uchumi
wake umeendelea kukua.
SWALI : Suala la nidhamu kwa Watumishi wa
Umma, Taasisi, Mashirika na Idara za Serikali mara baada ya Uhuru na
sasa miaka 55 ya Uhuru?
JIBU: Nidhamu ni suala la msingi mahali
popote na sio mahali pa kazi tu hata nyumbani kwako. Watanzania walizoea
kufanya kazi kwa mazoea na hivyo kukosa nidhamu. Utendaji kazi mzuri
unatokana na nidhamu ambayo inamfanya mtu afanye kazi kwa uadilifu.
Nidhamu katika Utumishi wa Umma
inayosisistizwa na Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli Itaongeza bidii ya
kazi kwa wafanyakazi viwandani na hivyo kuongeza uzalishaji. Enzi za
Baba wa Taifa Wafanyakazi na Wakulima wote walikuwa na nidhamu na
uwajibikaji ulikuwa mkubwa zaidi ndi maana uchumi wa nchi ulikuwa wa
juu. Kila mtu aliwajibika mahali pake pa kazi.
Enzi za Baba wa Taifa unapokwenda popote
duniani, ukisema niketoka Tanzania kila mtu anajua Mtanzania ni mkweli,
muwazi na ana nidhamu ya hali ya juu. Mtanzania hawezi kupokea wala
kutoa rushwa, hashiriki kwenye masuala yoyote ya kuiharibia heshima nchi
yake, mwenye kutumia madaraka yake vizuri, na asiyefuja mali ya umma.
SWALI:: Msaada gani unaweza kumpa Mhe Rais katika vita dhidi ya wakwepaji kulipa Ushuru?
JIBU: Kwanza namshukuru sana Rais katika suala zima la ukusanyaji kodi kwani ameonyesha umuhimu kwa kulipa kodi
Pili, nampongeza kwa kuanzisha mfumo
unaomtaka kila mfanyabiashara kuwa na mashine za kulipa kodi. “Mpaka
sasa imefikia mahali nchi nyingine za nje wameanza kuiga utendaji wa
kazi wa Rais wetu hili ni jambo la kujivunia”. Hivyo tumuunge mkono
katika hii vita ya ukusanyaji kodi. Watanzania wakubali mpaka sasa
kwamba hatua alizochukua Mheshimiwa Rais za kukusanya kodi ni sahihi na
tuziunge mkono.
Tatu, Serikali haina namna itakayoweza
kupata fedha za kusaidia watu wake kupata huduma za msingi. Fedha
zinazokusanywa ndio zinazotumika kwenye barabara, kununulia madawa
kujenga Hospital na mabo kama hayo.
SWALI :Unaposikia siku ya Uhuru wa Tanganyika unakumbuka nini?
JIBU: Hii inanikumbusha kauli ya Mwalimu
Nyerere alisema: “UHURU NA KAZI”, ni kweli kabisa lazima tufanye kazi
kama anavyosisitiza Rais wetu Magufuli “HAPA KAZI TU”. Maendeleo hayaji
kwa kupiga hadithi ni lazima watu wafanye kazi na asiyefanya kazi na
asile.
Pili siku hii ya Uhuru inanikumbusha juu
ya elimu ambayo wakati huo inatolewa bure, lakini baadaye ilisitishwa na
kuwafanya vijana wengi kukosa fursa ya kuendelea na masomo . Rais wetu
ameamua elimu sasa itolewe bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari
ili kuwaondolea mizigo wazazi ambao walishindwa kuwasomesha watoto wao
kutokana na gharama kubwa.
SWALI: Una wito gani kwa Watanzania katika kusheherekea miaka 55 ya Uhuru?
JIBU: Wito wangu kwa Watanzania tusikilize
maelekezo yanayotolewa na serikali yetu ambayo ni sikivu, tuisipende
kusikiliza maneno ambayo sio rasmi na kujiamulia jambo bila kufuata
sheria.Watanzania tufanye kazi tuache uvivu tusipende kulaumu serikali
wakati sisi wenyewe tunakaa tu bila kufanya kazi. Tuunge mkono Serikali
yetu kwa kila jambo inayoelekeza kufanya.
Waandishi wa Habari wanafanya kazi nzuri
sana ya kuelimisha. Napenda kuwapongeza kwa hilo. Waaendelee kuelimisha
jamii kwa kuelezea masuala ya msingi na muhimu katika maendeleo yao na
hasa nchi kwa ujumla.
Mwisho tuendelee kulinda Muungano wetu Amani yetu, Upendo, Umoja na Mshikamano.
No comments :
Post a Comment