Kwa mujibu wa kifungu cha 40 (6)
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ilipokea Rufaa moja
ya kupinga Uteuzi wa Mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) katika Uchaguzi
Mdogo wa Bunge Jimbo la Dimani – Zanzibar.
Rufaa hiyo ilikatwa na Mgombea wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bwana Juma Ali Juma akipinga Maamuzi ya
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dimani aliyemthibitisha Mgombea wa Chama
Cha Wananchi (CUF) Bwana Abdul Razak Khatib Ramadhani kuwa ni mgombea
halali.
Rufaa hiyo ilikuwa na sababu
mbili ambazo ni:- (i) Hakurudisha Fomu za Uteuzi kwa mujibu wa masharti
yaliyowekwa na sheria na (ii) Hakudhaminiwa na Chama cha Siasa kugombea
Ubunge. Katika kikao chake cha leo tarehe 30 Desemba, 2016, Tume
imepitia Rufaa hiyo na kuona sababu zilizotolewa na mkata Rufaa hazina
nguvu ya kisheria, kwa kuwa, Mgombea wa CUF amerudisha Fomu za Uteuzi
kwa mujibu wa sheria na taratibu. Pia, Fomu zake za Uteuzi zimesainiwa
na kugongwa muhuri wa Katibu wa Wilaya ya Magharibi B. Kwa mantiki hiyo,
Tume imekubaliana na Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dimani –
Zanzibar. Hivyo, Mgombea wa CUF amekidhi vigezo na uteuzi wake ni
halali na aendelee na kampeni za kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo
hilo.
Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha
44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume
imepokea Rufaa tatu; kutoka Kata ya Kijichi – Halmashauri ya Manispaa ya
Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, Kata ya Misugusugu – Halmashauri ya Mji
wa Kibaha, Mkoa wa Pwani na Kata ya Ihumwa – Halmashauri ya Manispaa ya
Dodoma, Mkoa wa Dodoma.
Kata ya Misugusugu Halmashauri ya
Mji Kibaha, Rufaa ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana Gasper Melkiory
Ndakidemi dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM Bwana Bogasi
Hussen Ramadhani.
Katika Kata ya Kijichi, Rufaa
ilikuwa ni ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah Shamas dhidi ya
mgombea wa CHADEMA Bwana Fredrick Felician Rugaimukamu.
Kata ya Ihumwa Rufaa ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana Magawa Edward Juma dhidi ya maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi.
Tume katika kikao chake cha leo tarehe 30 Desemba, 2016 imepitia Rufaa zote na imeamua ifuatavyo:
Rufaa ya mgombea wa CHADEMA Bwana
Gasper Melkiory Ndakidemi katika Kata ya Misugusugu Halmashauri ya Mji
Kibaha na ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah Shamas katika Kata ya
Kijichi, hazina mashiko ya kisheria na zimekataliwa. Hivyo, Tume
inakubaliana na Maamuzi ya Wasimamzi wa Uchaguzi wa Halmashauri hizo na
wagombea waendelee na Kampeni kwa mujibu wa Ratiba.
Kuhusu Rufaa ya Mgombea wa CHADEMA
kutoka Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Tume,
imepokea barua ya Msimamizi wa Uchaguzi, Manispaa ya Dodoma, ikiwa
imeambatishwa na barua ya Mgombea wa CHADEMA kuiondoa Rufaa yake na
kwamba anakubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi ambayo
yalimuengua. Pia, leo Tume imepokea barua za kujitoa Ugombea za wagombea
wa CHADEMA na ACT – WAZALENDO katika Kata ya Ihumwa. Kwa maana hiyo
Rufaa iliyokuwa imekatwa na mgombea wa CHADEMA Kata ya Ihumwa
imeondolewa kwa kuwa mkata Rufaa ameiondoa na amejitoa ugombea kabla
haijasikilizwa.
Mwisho, Tume inavisisitiza Vyama
vya Siasa, Wagombea na Wananchi wote wa maeneo yenye Uchaguzi Mdogo
kufanya Kampeni za kistaarabu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Maadili ya
Uchaguzi.
Imetolewa na:-
Jaji Mkuu (Mst. Znz) Hamid M. Hamid
MAKAMU MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
30/12/2016
No comments :
Post a Comment