Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Taasisi ya Global Education Link
imeisaidia Serikali kuzalisha rasilimali watu wenye ujuzi na elimu ya
kutosha ili watumike katika kuinua viwanda na uchumi wa nchi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Abdulmaliki Mollel
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa maonesho
ya kwanza ya viwanda Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba
vilivyopo jijini humo.
Mollel amesema kuwa Tanzania
imeamua kuwa nchi ya viwanda lakini bila kuwa na rasilimali watu wenye
ujuzi na elimu ya kutosha kuhusu uzalishaji na uendelezaji wa viwanda
hakutakuwa na maendeleo kwani maendeleo yoyote mzizi wake ni elimu na
ujuzi.
“Kuna baadhi ya masomo ambayo ni
muhimu hayapatikani katika vyuo vya Tanzania na kama zinapatikana basi
nafasi ni chache hivyo,taasisi hii ni kama daraja la kutengeneza
rasilimali watu wenye ubora watakaoleta maendeleo ya nchi kupitia kusoma
nchi za nje,”alisema Mollel.
Ameongeza kuwa ili nchi ipate
maendeleo kwa haraka ni lazima isaidiwe na taasisi na mashirika binafsi
na ndio maana taasisi hiyo imeamua kuisaidia Serikali kwa kuwarahisishia
Watanzania kupata elimu nje ya nchi ambayo itasaidia Serikali kupunguza
matumizi pamoja na kuzuia wataalamu wa nchi za nje kufanya kazi nchini.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa
mpaka sasa chuo hicho kimeshatoa wanafunzi takribani 5400 ambao wengi
wao wameshika nyazfa mbalimbali kwenye taasisi za Umma na Binafsi.
Aidha, taasisi hiyo ina mpango wa
kuandaa programu za miezi 4 hadi 6 ambazo zitakuwa maalum kwa ajili ya
kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi kwa kupitia elimu ya vitendo kwenye
viwanda mbalimbali vilivyoko nchini India.
Taasisi hiyo imeanzishwa mnamo
mwaka 2006 ikiwa na lengo la kurahisisha mchakato na kuwaondolea
usumbufu wanafunzi wanaohitaji kwenda kusoma nje ya nchi pamoja na
kuwasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao.
No comments :
Post a Comment