By Rabi Hume
Waliofariki ni dereva wa basi hilo Athumani Idd (47) mkazi wa Mabibo jijini Dares Salaam na mwalimu wa shule ya msingi Malunga aliyefahamika kwa jina moja la Janet (anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 29).
Habari zilizopatikana eneo la tukio, zimedai kuwa katika siku za hivi karibuni mwalimu Janet alimpeleka mama yake jijini Dar es salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Imedaiwa kuwa baada ya kufika Dar es Salaam, aligundua kuwa amesahau kuchukua kadi ya bima ya afya, na hivyo akalazimika kurudi Iramba.
Jana asubuhi Janet alichelewa basi la National Express katika kituo cha Kyengenge na kuamua kukodi bodaboda kulifukuzia basi hilo na kufanikiwa kulikuta kituo cha Malunga. Baada kupanda basi hilo, dakika chake baadae, basi hilo lilipata ajali na kulaliwa na basi kichwani.
Watu hao wamefariki dunia papo hapo na miili yao ipo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa mjini hapa. Basi hilo lilikuwa linatokea New Kiomboi, likielekea jijini Dar.
Akizungumza kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, ACP Debora Daudi Magiligimba, alisema ajali hiyo imetokea Desemba, 30 saa 12.45 asubuhi katika eneo la kijiji cha Tumuli.
Alisema ajali hiyo pia imesababisha majeruhi 26 ambao wamelazwa katika hosipitali ya mkoa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kamanda Magiligimba alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ajali hiyo kwa kiwango kikubwa imesababishwa na mwendo kasi na uzembe.
“Eneo hili ilipotokea ajali hii kuna mteremko na kona kali. Kutokana na mwendo kasi, dereva alishindwa kulimudu na hivyo kuacha barabara na kuingia kwenye korogo la mto, na kuruka juu kisha kupinduka mara tatu,” alisema.
Basi
la National Express lililopata ajali asubuhi ya leo katika kijiji cha
Tumuli, wilaya ya Mkalama mkoani Singida. (Picha na Nathaniel Limu,
Singida)
Kwa upande wake mganga mkuu mkoa wa
Singida, Dk. John Mwombeki, alikiri kupokea miili ya watu wawili
waliofariki dunia kwenye ajali ya basi la National Express, pamoja na
majeruhi 26.“Kati ya majeruhi hawa, mmoja dada Joyce tumempa rufaa kwenda hospitali ya taifa Muhimbili kutokana na sehemu yake ya mwili ya chini kutokufanya kazi. Majeruhi 10 wao tunaendelea kuwafanyia uchunguzi, lakini kuna uwezekano kuwapa ruhusa le oleo,” alisema Dk. Mwombeki.
Mmoja wa majeruhi hao mfanyakazi wa shirika la TBC jijini Dar es Salaam, Victor Elia, alisema pamoja na kupoteza kila kitu, anamshukuru Mungu kwa kupona kufa kwenye ajali hiyo mbaya.
“Kilichonisaidia ni kufunga mkanda … abiria wenzangu wote ambao hawakufunga mikanda ndio walioumia zaidi wakiwemo waliopoteza maisha. Ajali hii kwa vyovyote imechangiwa na mwendo kasi,” alisema Victor ambaye ni mtayarishaji na mtangazaji wa TBC.
Kondakta wa basi hiyo, Nicolaus Apolinari (23) mkazi wa jijini Dar es Salaam, alisema ajali hiyo imechangiwa na utelezi uliosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo.
Na Nathaniel Limu, Singida
No comments :
Post a Comment