Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo kwa wananchi wa Kata
ya Mpata wilayani Busokelo mkoani Mbeya ambao wapo tayari kutoa maeneo
yao ili kupisha ujenzi wa barabara inayounganisha kata hiyo na eneo la
Mwakaleli.
Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS) Mkoa wa Mbeya Eng. Paul Lyakurwa akisisitiza namna
atakavyoshirikiana na wananachi wa kata ya Mpata katika ujenzi wa
barabara itakayofungua uchumi wa kata hiyo ambayo ni maarufu kwa
uzalishaji wa ndizi na viazi.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akijibu maswali ya wananchi wa
Mwakaleli waliotaka kujua hatma ya fidia zao katika mradi wa ujenzi wa
barabara ya Katumba-Mbambo hadi Tukuyu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akijibu maswali ya wananchi wa
Mwakaleli waliotaka kujua hatma ya fidia zao katika mradi wa ujenzi wa
barabara ya Katumba-Mbambo hadi Tukuyu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo kwa wakazi wa kata
ya Mpata wakati alipokagua miundombinu ya barabara katika kata hiyo.
Wakazi wa mwakaleli wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (hayupo pichani).
Mbunge wa Busokelo Mhe. Atupele
Mwakibete akiongea na wananchi wa jimbo lake wakati Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani alipotembelea
kukagua miundombinu ya barabara jimboni humo.
………………………………………………………………..
Serikali imesema itaijenga kwa
kiwango cha lami barabara ya Katumba-Mbambo hadi Tukuyu KM 79.4 ili
kuiunganisha kwa lami wilaya mpya ya Busekelo na Wilaya nyingine za mkoa
wa Mbeya na hivyo kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng.Edwin Ngonyani amesema hayo mara baada ya kukagua
ujenzi wa barabara hiyo unaendelea katika sehemu ya Lupaso hadi Bujesi
KM 10 na kumtaka mkandarasi anayejenga barabara hiyo kampuni ya
Chongqing International Construction Corporation (CICO) kuongeza kasi ya
ujenzi huo kwa kuzingatia makubaliano yaliyopo kwenye mkataba.
“Nawaomba wananchi wa Busokelo
msimcheleweshe mkandarasi kufanya kazi yake kwa kuepuka vitendo
vinavyoweza kuchelewesha ujenzi wa barabara hii kwa kufungua kesi za
kudai fidia kwani kwa kufanya hivyo kunachelewesha maaendeleo ya ujenzi
wa barabara hii”. amesema Eng. Ngonyani.
Eng. Ngonyani amewataka wananchi
wa Wilaya ya Busokelo kushirikina na viongozi wao na kutoa ushirikiano
unaostahili ili kasi ya ujenzi wa baraba za lami katika maeneo yao
isikwamishwe na wananchi wachache.
Akiwa wilayani Busekelo Naibu
Waziri huyo amekagua barabara za Kata ya Mpata na Luteba ambazo
zinasimamiwa na halmashauri na kuahaidi kushirikiana na Wizara nyingine
ili kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara katika wilaya hiyo inayozalisha
mazao mengi chakula na biashara yanayosafirishwa katika miji mikubwa
nchini.
Naibu Waziri Ngonyani
amezungumzia umuhimu wa kuziunganisha wilaya za Makete na Busokelo kwa
lami ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na kukuza utalii katika
hifadhi ya kitulo.
Amemuagiza Meneja wa wakala wa
barabara (TANROADS) mkoa wa Mbeya Eng. Paul Lyakurwa kushirikiana na
halmashauri ya Busokelo katika baadhi ya miradi ili kuongeza kasi ya
kuboresha barabara na hivyo kuhuisha uchumi wa wakazi wa wilaya hiyo.
Naye Mbunge wa Busokelo Mhe.
Atupele Mwakibete amemuomba Naibu waziri Ngonyani kuangalia namna ya
kuijenga barabara ya Kata ya Mpata ili kuwezesha magari mengi
yanayosafirisha gesi kufika kwa urahisi katika eneo hilo na hivyo
kurahisha usafirishaji wa gesi,kuongeza ajira kwa vijana na kuongeza
pato la halmashauri hiyo.
“Mhe. Waziri wananchi wa Mpata na
Luteba wako tayari kutoa maeneo yao bila fidia ili barabara ijengwe
katika eneo hilo ambalo ni muhimu kwa uzalishaji wa viazi na ndizi”.
Amesistiza Mwakibete.
Naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonuani yupo katika ziara mikoani ya nyanda
za juu kusini kukagua miradi ya ujenzi na kutoa maelekezo kwa taasisi
zilizopo chini ya Wizara hiyo
No comments :
Post a Comment