Thursday, November 24, 2016

RAIS MAGUFULI AWEKA BAYANA SABABU ZA KUITUMBUA BODI YA TRA

chuo9
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
RAIS John Magufuli,ameweka bayana sababu za kuivunja bodi ya mamlaka ya mapato Tanzania( TRA) kuwa ilikuwa ni baada ya kuidhinisha mabilioni ya fedha kiasi cha sh.bil 26,katika taasisi binafsi tatu za kifedha.
Amesema fedha hizo zilikuwa zimetolewa katika mamlaka hiyo kwa ajili ya matumizi ya TRA na bodi ikapitisha ndio sababu ya kuivunja ambapo fedha hizo ameshazichukua na zipo kwenye mikono salama.

Dk.Magufuli aliyasema hayo katika mahafali ya 31,ya chuo kikuu huria Tanzania(OUT)yaliyofanyika makao makuu ya chuo hicho Bungo wilayani Kibaha .
Alielezea kuwa pamekuwa na kamchezo hako ,kwa baadhi ya viongozi wa aina hiyo ambapo wanachukua fedha za miradi mbalimbali na kuziweka katika mabenki binafsi kwa mazungumzo baina ya mkuu wa taasisi na taasisi husika.
Aidha alisema TEA ambayo imeanzishwa kwa ajili ya makusudi maalum na kuchangiwa fedha kwa ajili ya kujengea madarasa na kusaidia masuala ya sekta ya elimu zaidi ya sh.bil 30  lakini fedha hizo wameweka kwenye Fixed Account ili kupata faida.
“Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi ,upo message sent,mchezo huu upo sana wanazichukua na kupeleka kwenye Commerce Banks,wanaweka kwenye Fixed Deposit Accounts kwa makubaliano baina ya mkuu wa taasisi na taasisi za fedha husika.”
“TEA imeanzishwa kwa makusudi maalum bil.zaidi ya 30 lakini wamechukua fedha hizo na kupeleka kwenye taasisi za kifedha ,wakati kwenye elimu watu wanapata shida,sasa wananchi wakati mkiona serikali inachukua hatua ya kutumbua mtuachie tuu tuendelee kutumbua”alisema Dk.Magufuli.
Dk Magufuli alisema kumekuwa na mchezo wa wakuu wa taasisi mbalimbali kuchukua fedha na kuziwekwa kwenye akaunti maalumu ambapo serikali inakwenda kukopa kwa gharama kubwa.
“Kwa sasa huu ndo mchezo ambao unachezwa na kuisababishia serikali kukosa fedha jambo ambalo serikali haiku tayari kuona matumizi mabaya ya fedha zake,”
“Naomba mtuombee tuendelee kutumbua kwani nchi ilifika mahali pabaya lakini sasa tumbua hii mapato yameongezeka na kufikia trilioni 1.2 na kufikia 1.8 ambapo uchumi umeimarika,” alisema Dk Magufuli.
Uchumi umeimarika kwa asilimia 7 unatakiwa ukue kwa asilimi 7.2 hadi robo ya mwaka huu umekuwa 7.9 na kuwa moja ya nchi ambazo uchumi wake unakua ambako kati ya nchi tano imekuwa ya pili baada ya Ivory Coast.

Alisema kuwa suala la ubora wa elimu nchini halina mjadala na hakuna njia ya mkato kupata elimu bora.
Hata hivyo alifafanua kwamba lengo ni kulinda ubora wa elimu inayotolewa ili kuwa na wasomi ambao watakuwa watumishi bora.
Dk Magufuli alisema kuwa kutokana na kutaka kuhakikisha elimu inatolewa kwa ubora ambapo hata wale wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) walipohakikiwa walikutwa wenye sifa za kuwa pale ni wanafunzi 322 kati ya 7,500.
“Tungependa kila mtu asome kwa sifa aliyonayo na si vinginevyo tungependa sifa ya elimu yetu iwe kuwa juu na ni bora kuwa na wanafunzi wachache kuliko kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wasio na sifa,” alisema Dk Magufuli.
Alisema kuwa serikali ilipoamua kufanya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari kulijitokeza changamoto nyingi ambapo wanafunzi wa shule za msingi
idadi iliongezeka kwa asilimia 84 kwa shule za msingi na sekondari kidato cha kwanza iliongezeka kwa asilimia 26.
“Madawati tumepambana na sasa imefikia asilimia 98 huku mikoa michache inamalizia zoezi hilo pia kuliongezeka wanafunzi hewa 65,000 kwa shule za msingi na sekondari ambao walikuwa wakilipwa malipo hewa kwa kuongezwa majina ya uongo,” alisema Dk Magufuli.
“Changamoto zilizidi kuongezeka kwani bajeti ya mikopo iliongezeka kutoka bil. 340 na kufikia bilioni 473 kutokana na ongezeko la wanachuo 98,000 hadi kufikia 124,389 ambapo wanafunzi waliokuwa wanapewa mikopo hewa kwenye vyuo hadi sasa imefikia kiasi cha shilingi bilioni 3.5,” alisema Dk Magufuli

No comments :

Post a Comment