Taasisi
ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) imeshirikiana na kampuni ya
Getenrgy kuandaa mkutano wa Afrika wa Mafuta na Gesi (GETENERGY VTEC
AFRICA 2016) ambao unafanyika nchini kwa siku tatu kuanzia Novemba,
21-23, 2016.
Katika
hotuba yake ya utangulizi, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida
alisema kuwa mkutano huo umekutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya
mafuta na gesi kutoka nchi mbalimbali Afrika ikiwepo serikali, viwanda,
mashirika ya maendeleo na vyuo ambavyo vinatoa elimu ya mafuta na gesi.
Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida akitoa neno la utangulizi katika Mkutano wa Afrika wa Mafuta na Gesi.
“Malengo
ya mkutano huu ni kuangalia changamoto gani ambazo zinalikabili Bara la
Afrika katika sekta ya mafuta na gesi, kubadilisha ujuzi kwa wataalamu
wa mataifa ambayo yameshiriki na kujadili hatua ya kuchukua ili
kuboresha sekta hii lakini pia utasaidia kukuza ushirikiano baina ya
nchi washiriki,
“Katika
mkutano washiriki wataisaidia Serikali na wadau kuweka mikakati ya
kutekeleza na yenye ufanisi kuhusu sekta ya mafuta na gesi na kama
Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamiii tutaendelea kushirikiana na
wadau kutafuta changamoto zinazokabili sekta na mbinu za kutumia ili
kuyatatua,” alisema Dkt. Kida.
Mgeni
rasmi katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania, Mama Samia Suluhu akizungumza umuhimu wa mkutano huo na jinsi
ambavyo unaweza kuwanufaisha Watanzania.
Kwa
upande wa mgeni rasmi katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu alisema, Serikali kwa sasa
inataka kuhakikisha kunakuwapo na wataalamu wengi ili kunapokuwepo na
sehemu ambazo kunapatikana mafuta au gesi waweze kushiriki wenyewe ili
kipato kinachopatikana kiwanufaishe wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Nchi
ina akiba nyingi ya gesi na tunategemea kupata mafuta baadae lakini
tunangaalia upande wa wataalamu, tunahitaji kuwa na wataalamu katika
sekta ya mafuta na gesi ili tutakapoanza shughuli ya uchimbaji tayari
tuwe na wataalamu wanaohitajika hapa nchini,
“Huu
ndiyo mchango wa ndani, hatuwezi kufanya sisi pekee lazima tuwe na
wageni lakini pia tuwe na Watanzania wanaotumikia sekta hii na
wanaofaidika na uchimbaji wa hayo mafuta,” alisema Mama Samia.
Waziri
wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo akieleza jinsi ambavyo
Serikali imejipanga kuinua sekta na mafuta na gesi ili Watanzania wengi
wanufaike na uwepo wa mafuta na gesi nchini.
Nae
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alisema Serikali
imejipanga kuboresha sekta ya mafuta na gesi kwa kutoa elimu kuhusu
sekta hiyo katika baadhi ya vyuo mbalimbali nchini ili wahitimu
wanapomaliza waweze kuingia moja kwa moja katika sekta hii.
“Tupo
katika orodha ya nchi 20 Afrika ambazo zinafanya vizuri, baada ya miaka
mitano tutakuwa tumepiga hatua na mtaona ni jinsi gani tumefanikiwa,
kwasasa tuna wanafunzi wamehitimu UDOM na tunashirikiana na China na
Uingereza kwahiyo niwahakikishie kuwa tumejipanga,” alisema Prof.
Muhongo.
Mkurugenzi
wa kampuni ya Getenergy, Virginia Baker akitoa taarifa kuhusu kampuni
hiyo, malengo na umuhimu wa kufanyika kwa mikutano hiyo.
Mikutano
ya GETENERGY VTEC kwa mwaka 2016 tayari imeshafanyika katika nchi ya
Mexico na Uingereza na imekuwa ikikutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya
mafuta na gesi ili kujadili jinsi sekta hiyo inaweza kuboreshwa na kuwa
bora zaidi kuliko ilivyo sasa.
Wadau
mbalimbali wa sekta ya mafuta na gesi kutoka mataifa mbalimbali
wakifuatilia mkutano wa mafuta na gesi ambao mgeni rasmi alikuwa ni
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu akipewa
maelekezo kutoka kwa msimamizi wa banda la Chuo cha AGR TRACS kuhusu
masomo yanayotolewa na chuo hicho. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF,
Dk. Tausi Kida.
No comments :
Post a Comment