Monday, October 31, 2016

WATANZANIA WATAKIWA KUSHIRIKIANA KATIKA KUTUNZA MAZINGIRA

20
Na: Frank Shija, MAELEZO.
WATANZANIA watakiwa kufanya jitihada za makusudi katika suala zima la utunzaji wa mazingira ikiwa ni hatua za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Hali ya hewa na Tabia nchi.

Rai hiyo imetolewa leo na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua Tamasha la Kimataifa linalohusu Mabadiliko ya Tabia ya Nchi linalowakutanisha Wanasayansi, Watafiti na wadau wa mazingira chini ya Usimamizi wa Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Mazingira na Mabadiliko ya Tabia ya nchi.
Amesema kuwa suala la Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia nchi siyo hadithi ni jambo ambalo lipo wazi kuwa ni janga ambalo ipo haja ya kuchukua hatua za makusudi katika kutatua changamoto zake.
“Wadau wote tuone haja ya kuyatunza mazingira yetu mwananchi na wadau wa mazingira kwa ujumla, ni muhimu kwa umoja wetu tukaongeza jitihada za kupanda miti katika maeneo yetu ili kukabiliana na hali tete ya uharibifu wa mazingira nchini”.Alisema Mama Samia.
Aidha alisema kuwa wakati sasa umefika wa kuacha uharibifu wa mazingira kuanzia leo na kuanza kuyatunza ili kukabiliana na athari za Mabadiliko hayo ya Hali ya Hewa na Tabia nchi.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya amesema kuwa umefika wakati wakuitazama upya mitaala yetu ili kutoa fursa kwa elimu ya mazingira inaingizwa katika masomo kuanzia ngazi ya msingi.
Aliongeza kuwa elimu ikitumika vizuri inaweza kusaidia kwa kuongeza uelewa miongoni mwa jamii hali itakayopelekea wananchi kutambua namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko hayo na ikiwa ni pamoja na namna ya kuyahifadhi.
Mhandisi Manyanya alisema kuwa ni faraja kuona Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinamuenzi Mwl. Nyerere kwa Kuwa na Kigoda cha Mwalimu kinachohusiana na Mazingira kwani ni ukweli kwamba Mwalimu alikuwa Mwanamazingira na Muhifadhi wa Mazingira ndiyo maana utaona aliweza kuweka maeneo mengi ya Hifadhi za Taifa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala alisema kuwa imekuwa ni kawaida duniani kote kuwa na Vigoda ambavyo utumiwa kama njia ya kuwaenzi baadhi ya watu kwa michango yao.
Wao kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanamuenzi Baba wa Taifa kwa kuwa na Kigoda cha Mwalimu ambacho kilianzishwa mwaka 2008 kikiwa kimoja na kuongeza kuwa mpaka kufikia sasa vimeanzishwa Vingine viwili ambacho kimoja kinahusu Elimu ya Maendeleo na kingine ndicho hiki cha Masuala ya Mazingira ambacho kinafanya kazi nzuri sana.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabia ya nchi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amabye pia ndiye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi, Profesa Pius Yanda amesema mkutano huo wa siku TANO utakuwa na jukumu kubwa la kujadili kwa kina namna bora ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia ya nchi.

No comments :

Post a Comment