Wednesday, September 28, 2016

Chimbuko mifuko ya hifadhi ya jamii na manufaa yake Tanzania.




Tokeo la picha la PSPF JENGO PACHA

Jengo pacha la mfuko wa pensheni wa PSPF ambalo ni mojawapo ya vitega uchumi ya hifadhi ya jamii vinavyotokana na michango ya wanachama

Christian Gaya Majira 27 Septemba 2016

Hifadhi ya jamii ni mfumo wa jamii ambao umekuwapo tangu mwanzo wa mwanadamu. Tangu enzi za kale, jamii zote zimekuwa na taratibu mbali mbali za kuhakikisha ya kwamba kila mtu anakuwa na uhakika wa kuishi maisha yake katika mazingira yo yote yanayoweza kumkwaza kuishi kama majanga, maradhi, ulemavu, umri na kadhalika
Mfumo wa hifadhi ya jamii ambao ni wa lazima kisheria ambapo wafanyakazi pamoja na mwajiri wanachangia pamoja na kupeleka michango kwenye chombo cha mfuko wa pensheni au mfuko wa akiba ya wafanyakazi

Ingawa mpaka sasa idadi kubwa ya nguvukazi ndiyo inayojitoa kwa kuondoa mafao yao kabla haiyaifa na kwenda kinyume na malengo ya hifadhi ya jamii ambalo ni kumwezesha mwananchi kuishi maisha yenye staha kwa kuwawezesha kupata huduma za msingi pale wanapokuwa hawana kipato kutokana na sababu mbalimbali zinatokana na uzee, kifo,ugonjwa, uzazi n.k.

Kwa mujibu wa shirika la kazi duniani (ILO) hifadhi ya jamii ni mfumo ambao jamii husika imejiwekea kwa lengo ya kujikinga dhidi ya matukio yasiyotarajiwa.

Hifadhi ya jamii ni haki ya kila mtu na ndiyo maana haki hii imeanzishwa katika katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ibara ya 11(1) na sera ya taifa ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2003.

Haki hii pia imeiainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu wa mwaka 1948 pamoja na mikataba ya shirika la kazi duniani (ILO) ibara ya 102 ya mwaka 1952.

Wazee, watoto, yatima, wajane, na wagonjwa ambao kutokana na hali zao hawawezi kujikimu ni baadhi ya makundi ambayo yamekuwa yakipata kinga maalumu tangu enzi hizo hadi sasa, kama sehemu ya mfumo wa jamii ya mwanadamu duniani kote.

Jamii ilikuwa inahakikisha kuwa vikundi hivyo vya watu wasiojiweza wanapata hifadhi ya jamii kwa maana ya msaada wa chakula, malazi na matibabu.

Ili kuweza kutoa hifadhi hiyo jamii ilijiwekea taratibu na kanuni ambazo ilibidi zifuatwe kabla ya mtu hajapewa hifadhi kwa nia ya kuhakikisha kuwa ni wale tu wanaohitaji msaada ndiyo wanaopata.

Na utaratibu mpaka leo unafanyika ndani ya jamii za Kitanzania na penginepo pale hapa afrika na hata ulaya.

Hifadhi ya jamii ni haki ya msingi ambayo kila mtu anastahili kupata kutoka katika jamii. Jamii zilijiwekea utaratibu na sheria ambazo hutumika kuhakikisha jamii inapoondokana na utegemezi.

Sheria ya kwanza kabisa kutungwa na kuandikwa kuhusu hifadhi ya jamii ilikuwa in ile sheria ya kusaidia maskini huko uingereza iliyotungwa karne ya 16. Sheria hiyo ilifuatiwa na nyingine iliyotungwa mwaka 1883 kwa ajili ya matibabu.

Baadaye nchi nyingi hasa za ulaya zilianza kutunga sheria mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha mifumo ya hifadhi ya jamii. Na hiyo ilitokana na mapinduzi ya viwanda (industrial revolution) yaliyo tokea ulaya wakati huo, ambapo watu wengi walikimbilia mijini kutoka mashambani kwa kazi ya kuajiriwa viwandani.

Hivyo misingi ya kusaidiana kifamilia kwa watu wa mashambani, kifamilia kwa watu wa mashambani ikaanza kupotea. Kwa sababu nguvu kazi yote iliyokuwa ukitoa huduma katika koo mbalimbali iliishia kwenda mijini kwenda kufanya kazi. 
 
Lakini ikumbukwe kuwa hifadhi ya jamii ilitolewa na mpaka sasa bado inatolewa ndani ya jamii mbalimbali za kiafrika.

Na ndiyo maana wazee wengi wana imani hata ya kuzaa watoto wengi zaidi kama hifadhi yao ya jamii ya sasa na ya baadaye ingawa lengo kubwa ni kuendeleza ukoo na kufanya kuwa ni wajibu kuwa na watoto.

Watu wanateuliwa kubaki na wazee na wale wengine wasiojiweza ili kuwapa hifadhi.

Hata wakunga wa jadi tunao mpaka sasa ambao hutoa huduma kwa akina mama wajawazito na wanapojifungua.

Watoto waliofiwa na wazazi wao wana ukoo waligawana na kuwapa hifadhi ya jamii mpaka wanapofikia umri wa miaka 18 wa kujitegemewa na yule anayesoma anapewa hifadhi mpaka anapomaliza elimu ya juu.

Huo ni utaratibu ambao unawekwa na wanajamii hasa ndani ya koo mbalimbali.

Tumeona mara nyingi karibu mikoa yote hapa nchini huduma ya kupatiwa msaada wa mazishi unapotolewa ndani ya vikundi mbalimbali.

Na watu sasa wamegundua kuwa njia nzuri ya hifadhi ya jamii ni kwa ile isiyokuwa rasmi ambapo kuna vikundi mbalimbali vya kufa na kuzikana, kuweka na kukopa, ambapo wanachama wake hutokana na mkoa au wilaya anakotoka.

Na hata viongozi wakuu wa mashirika ya umma, mashirika yasiyo ya kiserikari, na wa serikali wamekuwa wanachama wachagiaji wazuri sana kwenye mifuko hii isiyo rasmi.

Na hii imeleta changamoto kubwa kwa hifadhi za jamii zilizo rasmi kama vile mashirika ya hifadhi ya jamii yaliyopo hapa nchini na sehemu zingine za kiafrika. 

Kwa kawaida anayetakiwa kuwajibika kutoa hifadhi ya jamii kwa wazee, walemavu, wategemezi, na kwa watu wasio na kazi ni serikali na jamii ya kitanzania kwa ujumla.

Umaskini zaidi ambao husababishwa na kukosa chakula, malazi, nguo au fedha kwa ajili ya kununuliwa hayo mahitaji muhimu huwa yanasababishwa na magojwa na hali ya uzee ukilinganisha na sababu zingine.

Kwa sababu hata mshahara wa mtu wa kila mwezi hautoshi kwa ajili ya kutimiza mipango ya leo na kwa siku sijazo. Kwa ujumla ni kwamba haitoshi kwa ajili ya mipango ya leo.

Kwa sababu ya kuwa na upungufu wa fedha hivyo inakuwa ni vigumu sana kwa mtu hata kuchangia kwa hiari kwenye mashirika ya hifadhi jamii kwa ajili ya siku za usoni.  

Na ndiyo maana imekuwa in kawaida ya kuwa kila nchi inawajibika kuhakikisha kuwa siyo tu kwa wale ambao wanaokufa kwa njaa ila pia inawajibika kuhakikisha kuwa maliasili ya nchi inagawanywa sawa ili kupunguza hali kama hii.

Hifadhi ya jamii ina maana ni aina ya hatua madhubuti au shughuli zilizobuniwa za kuhakikisha kuwa wananchi wa jamii hiyo wanapata mahitaji yao ya lazima na ya msingi  na wanapewa kinga ya hifadhi ya kutokana na majanga ili kuwawezesha kuwa na kiwango cha maisha ya kuishi kulingana na mila na desturi za jamii

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania na mshauri wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz au hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment