Sunday, August 28, 2016

KAMANDA SIRRO ATANGAZA KIAMA KWA WANANCHI WATAKAO ANDAMANA SEPTEMBA MOSI JIJINI DAR ES SALAAM



 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi (CP), Simon Sirro akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam leo, wakati akitangaza kiama kwa mwananchi yeyote atakayefanya maandamano Septemba Mosi ya kupinga udikiteta Tanzania yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). 

 Kamanda Sirro akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
 Magari ya polisi yenye zaidi ya askari 80 yakiondoka Kituo cha Polisi cha Kati, yakielekea Vikindu kwa ajili ya Operesheni saka majambazi.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Askari wa kikosi maalumu cha kupambana na uhalifu wakiondoka Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati kuelekea Vikindu kwa operesheni maalumu ya kuwasaka watu wanaotuhumiwa kwa ujambazi.

Na Dotto Mwaibale

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi (CP), Simon Sirro ametangaza kiama kwa mwananchi yeyote atakayefanya maandamano Septemba Mosi ya kupinga udikiteta Tanzania yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

“Jeshi la polisi mkoa wa Dar es Salaam tumejipanga vizuri siku hiyo nawaomba wananchi wasidhubuti kujitokeza kuandamana siku hiyo kwani watakiona cha moto” alisema CP Sirro.

Sirro alisema tayari jeshi hilo lina taarifa za kiinteligensia kuwa kuna vijana wanapewa fedha kwa ajili ya kuandamana na kufanya fujo Septemba mosi.  

Aliwasihi wananchi hasa vijana kutoingia barabarani Septemba mosi na kuwaachia wachache wenye nia ya kuletafujo.

“Ni rai yangu wale wananchi wazalendo wan chi hii wasiopenda kupambana na jeshi lao la polisi ambalo linawalinda na kulinda mali zao siku hiyo wasiingie barabarani,” alisema.

Aliwakaribisha wanao taka kuingia barabarani na kupambana na jeshi hilo na kuwa watakamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria.

“Sisi tupo vizuri na tupo imara hasa kwa wale wanaopenda kuvunja sheria kwa makusudi wata wajibika kwa mujibu wa sheria, hivyo suala la utiiwa sheria bila shuruti ni la msingi sana,” alisema Sirro.

Alisema jeshi hilo limejiandaa kwa wananchi wachache ambapo alibainisha  wananchi wengine hawana haja na maandamano hayo huku akibainisha vijana wachache wenye shida kupewa fedha na viongozi kwa lengo la kuandamana.

“Jiulize hiyo  40,000 unayo pewa kuingia barabarani na matokeo yake ukavunji kama mguu hiyo  40,000 ina thamani gani kwani… kwa hiyo mimi kama kiongozi wenu wa jeshi la polisi na sisitiza na ninaelekeza tuwaache wale wenye  sababu zao binafsi waingie barabarani,” alisema.

Katika hatua nyingine Kamanda Sirro alisema askari zaidi ya 80 wa kikosi maalumu cha kupambana na uhalifu wameondoka kwenda vikindu na maeneo mengine wilayani Mkuranga mkoani Pwani kufanya operesheni ya kuwasaka watu wanaodhaniwa kujihusisha na ujambazi.

No comments :

Post a Comment