Friday, July 1, 2016

Wafanyakazi wa majumbani na mazingira hatarishi ya kiafya





Mmojawapo  wa wafanyakazi wa majumbani ambao wengi wao hawana habari juu ya haki zao kuhusiana na masuala ya afya na usalama ikiwemo ya kinga ya hifadhi ya jamii
 
Christian Gaya Majira Ijumaa, 1Julai 2016

Wamiliki wa nyumba ambapo wafanyakazi wa majumbani wanafanyia kazi zao wanaweza kufikiri nyumba zao ni maeneo salama, lakini nyumba hizo hizo zinaweza kuwasilisha matatizo kadhaa ya kiafya na ki-usalama kwa watu wanaofanya kazi ndani mwake.


Utafiti uliofanywa nchini Salvador na Brazil, kwa mfano, uligundua kwamba wanawake wanaofanya kazi za majumbani wanakabiliana na viwango vya juu vya kuumia na kuambukizwa magonjwa kuliko wanawake wanaofanya kazi zingine. Wafanyakazi wa majumbani wanatambua kwamba kazi zao zinaweza kuwa hatari kwa afya zao.


Wafanyakazi wengi wa ndani hawajui haki zao, hivyo hawawezi kudai ulinzi au haki zao kutoka kwa waajiri wao kama vile kuandikishwa na mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii.

Mapato ya chini na ukosefu wa ulinzi au uzingatiwaji wa haki unamaanisha kwamba wafanyakazi wa majumbani wapo katika mazingira magumu na hivyo hatarishi kwa afya zao.

Endapo itatokea wakaugua au kuumia na hivyo kushindwa kuja kazini, wanaweza kupoteza mishahara au ujira wao au kufukuzwa kazi.

Tanzania zikiwemo Brazil na nchi kadhaa, zimeanza kuwahusisha wafanyakazi wa majumbani katika sheria za kazi ili kuwapatia kinga au haki za msingi kama vile likizo ya uzazi, likizo ya ugonjwa na ruzuku ya serikali pindi wanapokuwa hawana kazi.

Hata hivyo, inaweza kuwa vigumu sana kutekeleza sheria hii katika nchi yetu ambayo wasimamiaji wa sheria za kazi hawana vitendea kazi au rasilimali za kutosha za kufanyia kazi zao na mifumo ya taarifa/habari ni duni.

Wanaweza kuwa hawana hifadhi ya jamii ya aina yeyote au akiba ili kulipa bili za matibabu au kuwafanya waendelee na maisha mpaka watakapopata kazi mpya.

Hali hii inaweza kuonekana isiyo ya haki kabisa hususani kwa wafanyakazi ambao awali ya yote, chanzo cha ugonjwa au kuumia ni hiyo kazi yenyewe.

Taratibu au sheria za Afya na Usalama katika Maeneo ya Kazi yaani Occupational safety and health (OSH), ambazo zimelenga katika kuzuia hatari za kuumia au kupata ugonjwa katika sehemu za kazi, mara nyingi zimeonekana kuwalinda wafanyakazi rasmi waliopo katika mazingira rasmi ya kazi kama vile migodini, viwandani, ofisini na madukani ingawa bado kiwango kinachotakiwa hakijafikiwa.

Kanuni hizi haziwalindi wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika nyumba binafsi, kitu ambacho kinamaanisha kwamba japokuwa kazi za nyumbani ni chanzo muhimu cha ajira, na ingawa kuna hatari nyingi za kiafya na kiusalama katika kazi hizo, na japokuwa wafanyakazi wa majumbani wapo katika mazingira magumu ya umasikini endapo wataugua au kuumia, taratibu au sheria za OSH katika nchi yetu hii haziwazingatii.

Nchini Tanzania watafiti pia mara nyingi wanatumia njia au mbinu inayoitwa “orodha ya kukagulia afya” yaani health checklist. Tatizo ni kwamba mara nyingi watu huwa wanasita kuongelea juu ya miili yao na matatizo ya kiafya wakiwa wanahojiwa na kundi la watu ambao hawawajui vizuri.

Utafiti juu ya Afya na Usalama Katika Maeneo ya Kazi (OSH) na wafanyakazi wa majumbani unatakiwa kufanyika na mara nyingi unakuwa na malengo makuu mawili.

Lengo la kwanza unakuwa kuelewa matatizo ya kiafya na kiusalama ambayo wafanyakazi wa majumbani wenyewe wanayapa kipaumbele. Wafanyakazi wa majumbani wanajua vizuri zaidi juu ya matatizo wanayokabiliana nayo wao ni wataalamu wa hali ya juu kuhusu mazingira yao ya kazi, na katika mradi wowote unaojaribu kuelewa mazingira hayo, ni muhimu kwa kuanza kwa kuzungumza na wafanyakazi wenyewe.

Lengo la pili inatakiwa kujua zaidi kuhusu sheria/taratibu za OSHA nchini Tanzania na kuona ni aina gani ya mwingiliano wafanyakazi wa majumbani wanao na mamlaka za nchi katika maeneo ya afya na usalama.

Nchini Brazil watafiti walifanya kazi kupitia Sindoméstico, umoja wa wafanyakazi wa majumbani. Nchini Tanzania, watafiti walifanya kazi na Chama Cha Wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani (CHODAWU), umoja ambao pia unaratibu wafanyakazi wa majumbani.

Orodha ya kukagulia afya ni njia nyingine ya kuhamasisha washiriki katika mjadala wa pamoja kuongelea kuhusu matatizo ya kiafya wanayokumbana nayo kutokana na kazi zao bila kuongelea sana kuhusu matatizo yao binafsi.

Maeneo rasmi ya kazi mara nyingi huweka orodha ya kukagulia afya, ambazo ni fomu zinazoorodhesha matatizo ya kawaida ya majeraha na magonjwa ambayo hutokea katika eneo la kazi. Ikitokea kwamba wafanyakazi wanaugua au kuumia, hutoa ripoti juu ya tukio hilo katika sehemu zao za kazi na hurekodiwa au kuandikwa katika orodha ya kukagulia afya.

Hii ina maana kwamba viwango vya ugonjwa na kuumia katika sehemu ya kazi hufuatiliwa kwa makini na endapo itatokea kwamba watu wengi wanaugua au kuumia katika sehemu fulani ya kazi, vyama vya wafanyakazi au serikali inaweza kuingilia kati.

Wakati wa uchunguzi katika makundi nchini Tanzania, watafiti walielezea dhana ya orodha rasmi ya kukagulia afya mahali pa kazi kwa washiriki, ambao baadaye walitakiwa kutengeneza orodha za kukagulia afya ambazo zitawasilisha matatizo ya kawaida ya kiafya maalum kwa wafanyakazi wa ndani.  

Njia hii pia inahimiza majadiliano ya kutosha katika kundi au makundi kwa ajili ya kutafuta mwelekeo au muongozo.

Taarifa za matokeo ya utafiti juu ya afya na usalama, mazingira mengine ya kazi na mahusiano na mamlaka mbalimbali kuhusiana na afya na usalama zinasema nchini Brazil, wafanyakazi wa ndani walisema matusi na udhalilishaji wanaokumbana nao katika sehemu zao za kazi unawakilisha matatizo yao ya msingi ya kiafya na kiusalama.

Walisema wanahisi kama wanachukuliwa kama watumwa, ambao wametengenezwa kufanya kazi za kiudhalilishaji, na mara nyingi wameonyeshwa kutoheshimiwa kama binadamu na waajiri wao. Kama dondoo ifuatayo inavyoonyesha, matusi na udhalilishaji umewaacha wakiwa na hisia za kutojithamini kabisa na hisia kwamba kazi wanayofanya haina maana wala thamani:

“[Matatizo makubwa ni] kuitwa majina yasiyofaa, kufedheheshwa na kusimama kwa  vipindi au muda mrefu. Niliwahi kufanya kazi katika nyumba fulani ambapo niliruhusiwa kuketi wakati wa kula tu. Endapo ningekaa chini kupumzika kungetokea ugomvi au malalamiko, ilikupasa uwe umesimama muda wote, hakuna ambaye aliweza kukaa katika nyumba yake

“... wanamnyonya msaidizi wao wa nyumbani kwa kumfanya amhudumie mbwa wao pia, kwa kumuogesha. Sidhani kama kuhudumia wanyama ni sehemu ya kazi za nyumbani...“ “Inatubidi tufanye vitu ambavyo hatuna hata fununu ya jinsi ya kuvifanya, ambavyo hatujawahi kujifunza jinsi ya kuvifanya, jinsi ya kuziba ukuta au jinsi ya kusafisha tanki la maji, lakini tunalazimishwa kufanya vitu hivi na hii ni aina ya vurugu.“

Katika moja ya makundi nchini Tanzania, wafanyakazi waliuchukulia unyanyasaji wa kijinsia kama tatizo muhimu zaidi la kiafya na kiusalama linalowakabili. Mwanamke mmoja alihusisha kisa cha jinsi alivyotoroka kutoka katika hali kama hiyo:

“Nilikuwa nimeajiriwa na mwajiri fulani katika mkoa wa Iringa kwa takribani miaka 3...
nilikuwa na tatizo kubwa la unyanyasaji wa kijinsia ambapo baba na mwana walijaribu kunishinikiza niwe na mahusiano ya kimapenzi nao, lakini mimi nikakataa!

Nilichokifanya, niliamua kumwambia jirani. Jirani akaniambia ni bora kutoroka; akanisaidia kupata kazi Dar-es-salaam kwa ndugu yake. Ilikuwa ni kitu cha hatari sana kwangu mimi nilipoamua kutoroka bila hata ya kuwaambia wazazi wangu ambao wanaishi Iringa vijijini...sifanyi kazi tena na mwajiri yule. Kitu kibaya ni kwamba bado wazazi wangu wanafikiri nafanya kazi Iringa, kwa sababu siwezi kuwasiliana nao.“

Usanisi wa Matokeo ya Utafiti kutoka Brazil na Tanzania Ukosefu wa vifaa vya kujikinga pia ni tatizo wakati wafanyakazi wa ndani wanapowahudumia wanafamilia ambao wanaumwa-hususani kama wanaoumwa wana magonjwa yanayoambukiza kama vile VVU/ UKIMWI na/au TB.

Matatizo mengine muhimu ambayo yalitajwa ni pamoja na kubeba vitu vizito na kulazimishwa kupanda hadi mahali pa juu. Wafanyakazi wa majumbani wa Tanzania walikusanya pamoja orodha ya kukagulia afya kwa wafanyakazi wa ndani ambavyo inaonesha baadhi ya matatizo ya kiafya yanayotokana na hatari zilizotajwa hapo juu:

Hapa Tanzania inaonesha wazi kwamba wafanyakazi wengi wa majumbani hawana habari juu ya haki zao kuhusiana na masuala ya afya na usalama.Tatizo hili lipo kwa sababu wafanyakazi wengi wa majumbani wanatokea katika mazingira ya kimasikini, mara nyingi wana elimu kidogo, na wanatengwa kutoka katika makundi ya mengine ya wafanyakazi.

Hii inamaanisha kwamba, kwa pamoja, serikali na mashirika ya wafanyakazi wa majumbani wanahitaji kufanya jitihada za makusudi kuwaelimisha wafanyakazi wa majumbani kuhusu haki zao na kuhakikisha haki hizi zinazingatiwa.
inaendelea wiki ijayo.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala ya hakipensheni au hifadhi ya jamii. Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa barua pepe: gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz au hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment