Thursday, June 16, 2016

Tigo yatoa dola 12,000 (26.4m/-) kwa C-Sema kuboresha kituo cha Huduma ya simu kwa Mtoto

Meneja wa Huduma za Jamii wa Tigo Woinde Shisael akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya dola za Kimarekani 12,000(26.4m/-) Ofisa Mtendaji Mkuu wa C-Sema Kiiya kwa  ajili ya kuboresha kituo cha kutoa cha kupokelea simu cha Huduma ya Simu kwa Mtoto kilicho mjini Zanzibar, zoezi hili limefanyika leo katika viwanja vya JMK, Dar es Salaam kwa ajili ya kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika.
 

 Kampuni ya Tigo Tanzania imeshiriki katika kumbukumbu ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2016 kwa kuchangia  zaidi ya shilingi 26.4m/-($12,000) kwa asasi isiyo ya kiserikali ya  C-Sema  ambayo inaendesha kituo cha kupokelea simu cha Huduma ya Simu kwa Mtoto (Child Helpline Call Centre)  mjini Zanzibar ambacho kinatoa ushauri na kuwaunganisha watoto kupata huduma sahihi za kijamii  kikishirikiana na serikali.
Tigo na asasi ya C-Sema  watafanya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika  mwaka huu katika Kituo cha Michezo cha JMK Park jijini Dar es Salaam Alhamisi Juni 16. Siku ya Mtoto wa Afrika ni tukio linalofanyika duniani kote  kila Juni 16 ya kila mwaka. 
Akizungumza wakati wa kukabidhi  msaada huo, Meneja wa Huduma za Jamii wa Tigo, Woinde Shisael  alisema  msaada huo ni sehemu ya  mkakati wa kampuni  wa kuwekeza katika  ajenda ya kumlinda mtoto iwe kwa njia ya mtandao  na hata nje ya mtandao.
Akitoa shukrani  kutokana na msaada, huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa C-Sema, Kiiya JK aliishukuru kampuni hiyo ya simu kwa  kutoa mchango sahihi katika  kuwekeza rasilimali zake  ili kuhakikisha kwamba watoto na wazazi wanakuwa na uhakika wa kupata jukwaa ambalo wanaweza kutoa taarifa  kuhusu aina yoyote ya ukatili dhidi yao.
“Ninaishukuru  Tigo kwa msaada huu wakati leo tunasherehekea watoto wa Afrika kwa kuzisikiliza sauti zao wakati wakitueleza  kile wanachokifikiria kuhusu masuala mbalimbali yanayowasibu na nini kitu gani kifanyike  kutokomeza  matendo mabaya ambayo yanaweza   kukwamisha maendeleo yao.”
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la mwaka huu la Siku ya Mtoto wa Afrika.
Kituo cha taifa cha kupokelea simu za huduma ya simu kwa mtoto (Child Helpline call centre) kilianzishwa rasmi Juni 15, 2013  kikiwa na kituo cha Dar es Salaam na Zanzibar.

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YAELEZA HALI YA ULINZI NA USALAMA KWA MTOTO WA TANZANIA

TUM1Mkurugenzi wa Haki za Binadamu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bw. Francis Nzuki akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Mapendekezo ya Tume hiyo kwa Serikali na Jamii katika kuhakikisha Ulinzi na Usalama kwa Mtoto  unaimarika. Katikati ni Kamishna wa Tume hiyo Bi. Salma Ali Hassan.
TUM2 
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bi. Salma Ali Hassan akiongea na waandishi wa Habari(hawapo pichani) kuhusu hali ya mtoto wa Tanzania na mazingira hatarishi wanayokutana nayo ikiwemo ubakaji, ulawiti na unyanyasaji wa kijinsia. Kushoto ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bw. Francis Nzuki

MATUKIO YA PICHA KUTOKA BUNGENI DODOMA LEO

NGE1 
Wabunge wa Upinzani wakitoka Bungeni baada ya dua kusomwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson Juni 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NGE2 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali bungeni mjini Dodoma Juni 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NGE3 
Wageni waliofika Bungeni mjini Dodoma kujionea shughuli  mbalimbali za bunge wakifuatilia kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu  Juni 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NGE4 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiteta na Mbunge wa Nkansi Kaskazini, Ally Kessy bungeni mjini Dodoma Juni16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NGE5 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa zamani wa Singida mjini , Mohammed Dewji kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Juni 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NGE6 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana  na Mbunge wa zamani wa Singida mjini , Mohammed Dewji kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Juni 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NGE7 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Mwibara, Kange Lugola kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma Juni 16, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)

Watanzania watakiwa kutumia fursa za soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki

index 
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO,
WAFANYABIASHARA wa Tanzania wametakiwa kutumia fursa za biashara zinazopatikana katika soko la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  kwa kuuza bidhaa zao ndani ya Jumuiya hiyo.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
“Wafanyabiashara wanatakiwa kuchangamkia fursa ya biashara katika soko la pamoja kwa kuwa ni haki yao na ni utekelezaji wa malengo ya Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu cha tano ambapo ilianzishwa itifaki ya umoja wa forodha ” ,alisema Bi. Mindi
Wafanyabiashara hao pamoja na wasafirishaji wanaotaka kufanya biashara katika soko la Jumuiya hiyo watatakiwa kuonesha cheti cha uasilia wa bidhaa wakati wakiingia nchi wananchama wa Jumuiya hasa kwa wafanyabiashara wadogo wenye bidhaa zisizozidi dola za kimarekani 2000, ambapo hawalazimiki kuwa na wakala wa forodha.
Wanatakiwa kufuata utaratibu kwa kufika katika kituo chochote cha forodha kilichopo mpakani wakiwa na bidhaa zao ili wapewe cheti cha uasilia wa bidhaa.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, katika  Wizara hiyo, Bw. Geofrey Mwambe, amesema ni vyema wafanyabiashara wakatoa taarifa endapo watakumbana na vikwazo visivyo vya kiforodha kupitia mfumo wa ujumbe mfupi kwa kuandika neno ‘NTB’ kwenda namba 15539.
Bw. Mwambe amesema pia ,madereva  wanaosafirisha mizigo  kwenda nchi wanachama watakapokutana na vikwazo  visivyo vya kiforodha barabarani watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi kupitia namba 0713631780.
Kwa mujibu wa Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu namba 5 ambapo Jukuiya ilianzisha Itifaki ya Umoja wa Forodha (East African Community Customs Union) wafanyabiashara wa nchi wanachama wa Jumuiya  hiyo wana fursa  za kufanya biashara kwa kuuza bidhaa zao ndani ya nchiwanachama  wa Jumuiya hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi  bila kutozwa ushuru wa forodha ilimradi bidhaa zao zimezingatia vigezo na kufuata utaratibu ulioainishwa katika itifaki hiyo.
Japokuwa Sudani ya Kusini imeridhia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki bado fursa za kufanya biashara nchini humo hazijakamilika.

WAZIRI MKUU: KILA MKOA UUNDE KAMATI YA AMANI

 DOM1 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika futari aliyoiandaa kwenye makazi yake mjini Dodoma Juni 15, 2016. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Dodoma, Alhaj Adam Kimbisa na Wapili kushoto ni Kaimu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Ahmed Said.Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na mazingira, January Makamba.(Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
DOM2 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Makamu Mwenyekiti Mstaafu, John Malecela  katika futari aliyoiandaa kwenye makazi yake mjini Dodoma Juni 16, 2016. (Picha  na Ofisi ya Waziri Mkuu)
DOM3 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na  Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga katika futari aliyoiandaa kwenye makazi yake mjini Dodoma Juni 15, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
DOM4 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba katika futari aliyoianda kwenye makazi yake mjini Dodoma Juni 15, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
DOM5 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akisalimiana na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson katika fuatari aliyondaa kwenye makazi kake mjini Dodoma Juni 15, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kila mkoa unatakiwa kuunda Kamati ya Amani kama njia ya kudumisha amani na utulivu kwenye mikoa yote nchini.
Waziri Mkuu ametoa wito huo jana usiku (Jumatano, Juni 15, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa dini wa mkoa wa Dodoma na baadhi ya wazee maarufu wa mkoa huo aliowaalika kwenye futari katika makazi yake mjini Dodoma.
Amesema anatambua kuwa mkoa wa Dodoma uko shwari kwa sababu ya mshikamano uliopo baina viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo. “Nimegundua kuwa siri kubwa ya mkoa wa Dodoma kuwa na utulivu ni kuwepo kwa kamati ya amani yenye viongozi mahiri, kwani sote tunatambua kuwa kazi ya viongozi wa dini ni kuwaimarisha watu kiroho,” alisema.
Waziri Mkuu alisema ziko nchi zinatamani kuwa kama Tanzania kwa sababu wao hawana uhakika wa kulala na kuamka salama asubuhi. “Pamoja na yote sisi tuna uhakika wa asilimia 99 kulala usiku na kuamka salama asubuhi, kwa sababu ya amani iliyopo,” alisema.
Hadi sasa mikoa ambayo imekwishaunda kamati za amani ni Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Dodoma, Arusha, Lindi, Mtwara, Tanga na Mbeya.
Akigusia suala la mauaji ya hivi karibuni, Waziri Mkuu alisema anawaomba Watanzania kila mmoja kwa imani yake akemee kwa nguvu matendo hayo kwa sababu yeye haamini kama yamefanywa na Watanzania ambao wamelelewa kwenye misingi ya dini.
“Siamini kama kuna mtoto aliyelelewa kwenye misingi ya Uislamu anaweza kuingia msikitini na kuwaua wenzake wakati wakimwomba Mungu. Na wala siamini kama kuna mtoto aliyelelewa na kukuzwa Kikristo anaweza kuingia kwenye nyumba ya ibada akakuta watu wanasali na kuamua kuwaua. Ninawaomba tukemee kwa nguvu zote tabia hii,” alisisitiza.
Aliwataka watanzania wote wawe na walinzi wa wenzao kwa sababu kila mmoja ana jukumu la kumlinda mwenzake. “Tusiachie majeshi kazi hii kwa sababu kila mmoja na jukumu la kwanza kujilinda yeye mwenyewe na kisha kumlinda jirani yake,” alisema.
Kwa upande wake,  Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Ahmed Said alisema wanawaombea dua Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika kazi za kuleta maendeleo kwa Watanzania. “Pia tutaendelea kuiombea nchi yetu ili Mwenyezi Mungu azidishe amani yake na watu wake waishi kwa amani, upendo na utulivu,”  aliongeza.
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Dk. John S. Malecela ambaye alikuwa miongoni mwa wazee maarufu walioalikwa kwenye futari hiyo aliwataka waalikwa wenzake waendelee kuwaombea viongozi wa kitaifa na kusisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuombea amani ya Tanzania ambayo imedumu kwa miaka mingi iendelee kuwepo.
Katika hatua nyingine, Askofu wa Kanisa la Mennonite Tanzania Dayosisi ya Kati, Askofu Amos Muhagachi, ambaye alipewa fursa ya kutoa salamu fupi kwenye hafla hiyo, alisema kwenye mkoa huo hakuna magomvi ya kidini kwa sababu viongozi wa dini zote wanashirikiana kwa karibu sana.
“Hapa Dodoma Maaskofu tunashirikiana vizuri na Masheikh. Hivi sasa, masheikh vijana na wachungaji vijana wameanza kuiga haya tunayofanya, na zaidi ya yote tunashirikiana pia kuwaombea Rais wetu, Makamu wa Rais pamoja na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu,” alisema

TANZANIA MWENYEJI MAADHIMISHO YA 6 WIKI YA MAJI BARANI AFRIKA

JIM1Mkurugenzi Msaidizi Maji Shirikishi kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji Bw. Sylivester Matemu akiongea na waandishi (hayupo pichani) kuhusu Maadhimisho ya 6 ya Wiki ya Maji Barani Afrika na Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Nchi za Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 18-22 Julai 2016. Kulia ni Afisa Mawasiliano wa Wizara hiyo Bw. Dennis Kiilu.
JIM2Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano huo
…………………………………………………………………………………………………….
Frank Mvungi- Maelezo
Tanzania Mwenyeji maadhimisho ya 6 ya wiki ya Maji Barani Afrika na Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa  Nchi za Afrika yatakayofanyika  Julai,2016 Jijini Dar es salaam.
Kauli hiyo imetolewa na  Mkurugenzi Msaidizi Maji Shirikishi kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji Bw. Sylivester Matemu wakati wa mkutano na waandishi wa  Habari leo jijini Dar es salaam.
Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Maonyesho ya Wiki ya maji yatakayofanyika kabla ya mkutano wa Baraza la Mawaziri atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Kassim Majaliwa.
Akifafanua Matemu amesema kuwa mkutano huo utahusisha washiriki zaidi ya 1000 kutoka mataifa 54 kutoka Bara  la Afrika na wengine kutoka nje ya Afrika.
Maadhimisho  hayo yataambatana na maonyesho ya shughuli za wadau wa sekta ya maji na umwagiliaji, kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es salaam.
Kauli mbiu ya kongomanao hilo ni “ Kufikia lengo la maendeleo Endelevu Juu ya usalama wa Maji na usafi wa mazingira” alibainisha Matemu.
Mkutano huo utawasaidia wataalamu wa maji  kutoka Mataifa mbalimbali ya Afrika kujadiliana kuhusu mikakati mbalimbali itakayosaidia kupambana na changamoto zinazoikabili sekta ya maji katika bara la Afrika.
Akizungumzia faida za Mkutano huo Matemu amesema kuwa  utasaidia kufungua fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya maji na Sekta nyingine ikiwemo kukuza na Kutangaza vivutio vilivyopo hapa nchini hali itakayosaidia kukuza Utalii.

MWENYEKITI WA CHAMA CHA WAKULIMA (AFP) AZUNGUMZA NA WANDISHI WA HABARI JUU YA HUJUMA ALIYOFANYIWA

wz1 
Mhariri Mkuu Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Ramadhan Ali akimkaribisha Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP) ambae pia ni Waziri wa SMZ asie na Wizara Maalum Saidi Sudi azungumze na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo.
wz2Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP) Saidi Sudi akizungumza na waandishi wa Habari hawapo (pichani) kuhusiana na kadhia ya kukatwa mikarafuu, minazi na mihogo katika shamba lake lenye urefu wa eka moja na nusu huko Pemba.
wz3 
Baadhi ya wandishi wa Habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP) Saidi Sudi hayo pichani katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA JESHI LA POLISI MWANZA

ut6 
MNAMO TAREHE 15.06.2016 MAJIRA YA SAA 14:20HRS KATIKA KIJIJI NA KATA YA BUHAMA TARAFA YA BUCHOSA WILAYA YA SENGEREMA MKOA WA MWANZA, NDIMILA LUPOGOSHA MIAKA 30 MVUVI NA MKAZI WA KIJIJI CHA BUHAMA ALIUAWA KWA KUPIGWA NA KITU CHENYE NCHA KALI KICHWANI NA SHINGONI NA MKEWE AITWAYE MARTHA MAGUGU MIAKA 40 PINDI WALIPOKUWA WAKINYWA POMBE KATIKA GROCERY YA MAMA ALI ILIYOPO KATIKA KIJIJI HICHO.
INADAIWA KUWA TAREHE 14.06.2016 MAJIARA YA SAA 23:00HRS USIKU WAKATI WAKINYWA POMBE KATIKA GROCERY TAJWA HAPO JUU, MKE WA MAREHEMU BI MARTHA ALIMUONA MUMEWE AKIONGEA NA MWANAMKE MWINGINE KITENDO AMBACHO HAKIKUMFURAHISHA NA KUAMUA KUMPIGA NA KITU CHENYE NCHA KALI KICHWANI NA SHINGONI HALI ILIYOPELEKEA KUTOKWA NA DAMU NYINGI KICHWANI NA KUFARIKI DUNIA SIKU YA JANA YA TAREHE 15.06.2016 MAJIRA YA SAA 14:20HRS MCHANA WAKATI AKIPELEKWA HOSPITALI, NA  BAADA YA KIFO NDUGU WA MAREHEMU NDIPO WALIPOTOA TAARIFA POLISI.
CHANZO CHA MAUAJI  INADAIWA KUWA WIVU WA KIMAPENZI NA MTUHUMIWA WA MAUAJI HAYO AMEKAMATWA YUPO CHINI YA ULINZI WA JESHI LA POLISI, HUKU MAHOJIANO DHIDI YA TUHUMA ZA MAUAJI ANAYODAIWA KUTENDA YAKIENDELEA. PINDI UCHUNGUZI PAMOJA NA UPELELEZI KUHUSIANA NA TUKIO HILO UKIKAMILIKA MTUHUMIWA ATAFIKISHWA MAHAKAMANI , MWILI WA MAREHEMU TAYARI UMEFANYIWA UCHUNGUZI NA DAKTARI NA KUKABIDHIWA KWA NDUGU WA MAREHEMU KWA AJILI YA MAZISHI.
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MWANZA KAMISHINA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI AHMED MSANGI ANATOA WITO KWA WANANCHI AKIWATAKA KUWA MAKINI WAKATI WOTE NA MAAMUZI WANAYOYACHUKUA PINDI WANAPOKUWA KATIKA UGOMVI ILI KUWEZA KUZUIA MAJERAHA NA VIFO VINAVYOWEZA KUEPUKIKA, KWANI KUJERUHI AU KUUA NI KOSA LA JINAI HIVYO JESHI LA POLISI LITAMSHUHULIKIA MHUSIKA NA KUHAKIKISHA ANAFIKISHWA KATIKA VYOMBO VYA SHERIA KUJIBU TUHUMA ZITAKAZO MKABALI.

Mkurugenzi Kinondoni amewataka walipa kodi na ushuru kupewa stakabadhi za kielektroniki

BARAZA 5 
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni amewataka walipa kodi na ushuru katika Manispaa hiyo kudai stakabadhi za kielektroniki baada ya kufanya malipo ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato.
Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya njia wanazozitumia katika ukusanyaji wa ushuru wa Manispaa hiyo.
“Napenda kuwasisitiza wananchi kuwa unapofanya malipo yoyote ya Manispaa lazima uhakikishe unapewa stakabadhi ya kielekroniki na iwapo hutopewa, unaruhusiwa kutoa taarifa kwa kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi kwenda 0767643460 na utapatiwa maelekezo ya nini cha kufanya”,alisema Kagurumjuli.
Kagurumjuli ameongeza kuwa Ofisa yeyote atakayekaidi kutoa stakabadhi hizo atachukuliwa hatua kali za kisheria kwani kukwepa kulipa mapato ni kurudisha nyuma uchumi wa nchi.
Aidha, Mkurugenzi huyo ameyataja maeneo ambayo mwananchi anaweza kulipia kodi au ushuru na kupata stakabadhi za kielekroniki ni Ofisi za Manispaa, Ofisi za Kata, Benki ya CRDB pamoja na watumishi wa Manispaa waliopo katika shughuli maalumu za ufuatiliaji wa kodi na ushuru.
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilianza kutumia mfumo wa kulipa kodi na ushuru kwa njia ya kielekroniki mnamo mwaka 2013 , na mwaka 2015 ilipata tuzo ya ukusanyaji bora wa mapato kwa njia hiyo kwa Tanzania na Afrika nzima.

WENGI WAJIUNGA NA NSSF JIJINI MWANZA

Ofisa Uandikishaji wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kwandu Ikombe (kushoto), akiwaandikisha wanachama wapya wa NSSF katika eneo la Tanganyika Bus mjini Mwanza. (Na Mpigapicha Wetu)
Afisa Mwandamizi wa Masoko na Uhusiano wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Aisha Sango akigawa vipeperushi vyenye taarifa kuhusu NSSF wakati wa zoezi maalum la utoaji  elimu kwa umma kuhusu mafao na huduma mbalimbali za NSSF .
Ofisa Masoko Mwandamiza wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Amina Mmbaga akitoa elimu kuhusu NSSF kwa wanawake wajasiriamali wa kuuza viatu katika eneo la Tanganyika jijini Mwanza.
Afisa Mwandamizi wa Masoko na Uhusiano wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Anna
Nguzo akitoa elimu kuhusu NSSF wakati wa zoezi maalum la utoaji  elimu kwa umma kuhusu mafao na huduma mbalimbali za NSSF.

KAMATI YA MAWASILIANO MKOA WA MWANZA YATOA ELIMU KWA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Mkoa wa Mwanza, Jonathan Abdallah Kasibu, akizungumza katika Semina
kwa Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Jijini Mwanza iliyofanyika jana katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwanza.

……………………………………………………………………………………………..
Katika semina hiyo, watumiaji wa hudumza za mawasiliano ikiwemo simu pamoja na vyombo vya habari ambao waliwakilisha makundi mbalimbali kama vile wanahabari, wajasiriamali na walemavu, walipewa elimu juu ya uwepo wa Kamati hiyo pamoja na uwepo wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa huduma za Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA-CCC).
Pia walielimishwa juu ya mwongozo wa kuwasilisha malalamiko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano, haki na wajibu wa mtumiaji wa huduma za mawasiliano pamoja na sheria ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015.
Semina hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano, kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA-CCC) ambapo iliambatana na viongozi wa Kamati ya Mawasiliano mkoani Mwanza kujitambulisha kwa baraza hilo.
Watumiaji wa huduma za mawasiliano walielezwa kwamba ni wajibu wao kuwasilisha malalamiko yao ikiwa
wanapokea huduma zilizo chini ya kiwango ama ikiwa wana malalamiko ya aina yoyote kuhusu huduma za mawasiliano.
Walihimizwa kuwasilisha malalamiko yao kwa kuanza na mtoa huduma, yasiposhughulikiwa wanawayawasilisha
katika Kamati ya Huduma za Mawasiliano mkoa, yasipotatuliwa yatawasilishwa katika Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano kutoka TCRA na hata ngazi nyingine zaidi hadi pale utatuzi utakapofanyika.
Semina hiyo ilionekana kuwafungua ufahamu watumiaji wa huduma za mawasiliano jijini Mwanza kwani
baadhi yao walieleza kuwa awali walikuwa hawatambui haki na wajibu wao katika kutumia huduma za mawasiliano.
Baadhi ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Jijini Mwanza, wakiwa katika semina ya
kuwaelimisha juu ya Matumizi ya Huduma za Mawasiliano

No comments :

Post a Comment