Jonas Kamaleki, Maelezo
——————————
WAAENDESHA pikipiki maarufu kama
bodaboda wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali abiria wanaokataa
kuvaa kofia ngumu (Helmet) ili kutoa fundisho kwa watu wengine
wasihatarishe maisha yao.
Akiongea katika mahojiano maalum,
mwendesha pikipiki, Nathanael Kiula wa Dar es Salaam amesema kuwa abiria
wanaokataa kuvaa helmeti wachukuliwe hatua kali ikiwepo kutozwa faini
isiopungua Tsh. 30,000/= ili liwe fundisho kwa wengine.
“Mimi nina helmeti mbili ya kwangu
na abiria lakini abiria wengi hawataki kuvaa helmeti hasa akina mama
kwa madai kuwa nywele zao zinaharibika pia wanadai kuwa zina
uchafu.”alisema Kiula.
Kiula alisema kuwa elimu itolewe
kwa abiria na waendesha pikipiki juu ya umuhimu wa kuvaa helmeti kwani
ni kwa manufaa yao wanapopata ajali wasiumie sana au kupoteza maisha na
si kwa ajili ya kuwakwepa matrafiki.
Mwendesha pikipiki
aliyejitambulisha kwa jina la Isaac William alisema abiria wanaokataa
kuvaa helmeti waadhibiwe vikali ili kukomesha tabia hii isiokubalika
katika suala zima la usafirishaji.
“Abiria wangu baadhi wanakubali
kuvaa helmeti lakini walio wengi hukataa kuzivaa kwa madai kuwa
wanaogopa magonjwa ya kuambukizwa kupitia vifaa hivyo,”alisema William.
Naye abiria wa bodaboda ambaye ni
mkazi wa Dar es Salaam, Bi Fatuma Abdallah amesema yeye hawezi kuvaa
helmeti kwani zinatumiwa na watu wengi hivyo anaogopa kupatwa na
magonjwa.
“Siwezi kuvaa mikofia yao kwani
inatumiwa na watu wengi huwezijua wana magonjwa ya ngozi kiasi gani,
kamwe sintoyavaa ng’o,”alisema Fatuma.
Kwa upande wake Kamanda Mkuu wa
Kikosi cha Usalama Barabarani nchi, Mohamed Mpinga alisema kuwa uvaaji
wa kofia ngumu kwa waendesha pikipiki ni lazima. Anayekaidi amri hiyo
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji
Mkuu wa Taasisi ya Helmet Vaccine Initiative Tanzania Foundation, Bw.
Alpherio Nchimbi alisema matumizi ya Helmeti hayaepukiki kwa usalama wa
mwendesha pikipiki na abiria.
“Kwa umuhimu huo, Taasisi yetu
inatoa msaada wa kiufundi kwa Jeshi la Magereza nchini kwa ajili ya
uanzishwaji wa kiwanda cha kutengeneza kofia ngumu kwa kufuata viwango
vya Shirika la Viwango nchini (TBS) na pia tunatoa elimu kwa bodaboda
kuhusu matumizi ya kofia ngumu na madhara yatokanayo na kutovaa kofia
hizo kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla,” alisema Nchimbi.
Kuhusu suala la kuvaa helmeti,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kuwa mwendesha
pikipiki na abiria ni lazima wavae helmeti na ifikapo Julai 1, 2016
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya abiria au mwendesha pikipiki
atakayekaidi amri hiyo.
“Nawaambia, hatutamvumilia mtu
yeyote, mwendesha pikipiki na abiria asiyevaa helmeti tunawahesabu kuwa
wana mpango wa kujiua,”alisema Makonda wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa
Taifa wa Usalama wa raia wa Jeshi la Polisi.
Suala la kuvaa kofia ngumu au
helmeti kwa waendesha pikipiki na biria wao limekuwa likipuuzwa kwa muda
mrefu ndio maana serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na
Jeshi la polisi wameandaa utaratibu wa kuwafuatilia na kuwachukulia
hatua za kisheria kwa ajili ya kunusuru maisha yao. Mpango huu unaanza
rasmi tarehe 1, 2016.