Sunday, January 3, 2016

Umuhimu wa mikataba ya huduma kwa mwanachama


Mifuko itambue ya kwamba kuwa na mkataba wa huduma kwa wanachama utawezesha wanachama wao kujua mafao yatolewayo, haki na wajibu wao ndani ya mifuko hiyo na kwa upande mwingine mifuko hii itatoa fursa za wazi kwa wateja kuwasiliana na mifuko ili kutoa mapendekezo ya namna ya kutoa huduma bora zaidi.


Mfanyakazi anahitaji kujua kiundani zaidi juu ya ubora wa mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii, lazima ajue hata viwango vya ubora huduma zao, mazingira ya sehemu unapopatiwa huduma kuanzia getini kwa askari mpaka unapofungulia madai ambapo yanahitaji kuwa sehemu za kuvutia zaidi. 

Mwanachama angependa kujua je huchukua siku ngapi kupata hundi yake ya pensheni au ya mafao ya kujitoa, je ahadi zake zinatekelezwa kama alivyoahidiwa, na anayemhudumia anamchagamukia na kumhudumia mwanachama kama mfalme wa mfuko huo. Je hao wafanyakazi wa mifuko wanajua ya kuwa mwanachama ndiye mwajiri wao. 

Je wanaandaa pensheni yake ya kustaafu baada ya kila mwezi mmoja kama alivyoahidiwa. Kuna mambo mengi ya kuchunguza kwanza kabla ya kujiunga hasa kwa mwanachama mchangiaji anahitaji kujua kwanza utaratibu wa jinsi ya kujisajiri na kutaka kujua kiwango cha kuchangia ni asilimia ngapi ya kipato chake cha mwezi.

Mwanachama lazima afahamu michango yake ya hifadhi ya jamii inakatwa kwenye mshahara au kwenye mshahara pamoja na marupurupu mengine. Je, mafao yako ya pensheni yanakatwa kodi au hayakatwi. 

Mwanachama anatakiwa kujua ni kiwango gani mwajiri naye anatakiwa amchangie ili ichanganye pamoja na alichokatwa na kupelekwa kwenye mfuko wa pensheni. Na kuhakikisha ya kuwa michango hiyo ipelekwa kwenye huo mfuko kwa wakati gani wa muafaka kisheria. 

Mwanachama anatakiwa kufahamu ni wajibu wa nani kuhakikisha kuwa michango hiyo inapelekwa kwenye mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii. Na chama cha wafanyakazi sehemu ya kazi kina wajibu gani juu ya michango hii ya pensheni kazini. 

Je mfumo gani wa hifadhi ya jamii, ni wa pensheni, akiba au wa hiyari. Ni aina gani ya mafao yanayotolewa na mfuko huo. Je kuna mafao ambayo unaweza kunufaika wakati unapoendelea kufanya kazi na yale ambayo unaweza utanufaika baada ya kustaafu.
Familia yako inawezaje nayo kunufaika na mafao hayo ya muda mrefu na ya muda mfupi. Je ukusanyaji wa michango ya pensheni una urasimu mwingi na usio na uwazi na ukweli kwa mchangiaji. 

Je mipango ya malipo ya mafao kwa mwanachama inalipwa kwa wakati muafaka na kwa usahihi wa uhakika kabisa bila ya mapunjo au kuzidishiwa na kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Je mwanachama anaweza kupata habari zote na ushauri na zilizokamilika kutoka mfuko wa pensheni karibu na mahali karibu anapoishi. 

Mwanachama anaweza kupata habari na ushauri wowote hata bila ya kuanza yeye kudai huduma hiyo kutoka mfuko wa pensheni. Je muda unaotumika kukokotoa mafao yake ya pensheni ni mfupi au ni wa muda mrefu. 

Vile vile ni muhimu kama mwanachama mchangiaji pamoja na mwajiri wake kila mmoja  anatakiwa kujua wajibu wake kwenye mfuko huo. 

Mfuko lazima uweke wazi haki za wanachama hasa zile za kumruhusu mwanachama kukata rufaa kwenye bodi ya sheria ya mfuko atakapoona kwamba pale hajatendelewa haki inavyotakiwa na mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii kama vile kulipwa pungufu ya mafao yake. 

Kama wanachama mchangiaji wa mfuko lazima ajue atashirikishwaje kwenye maamuzi na uendeshaji wa mfuko huo na kwa faida ya nani. Ni juu ya mfanyakazi mwenyewe kuchagua kwa kutumia vigezo vya kitaalamu 

Hivyo kuna haja kubwa kila mfuko wa pensheni ya hifadhi ya jamii kuwa na mkataba wa huduma kwa wateja wao ili kukuza uelewa kuhusu upatikanaji wa huduma ubora zinazotolewa na mifuko hii ya hifadhi ya jamii.

No comments :

Post a Comment