Sunday, January 3, 2016

Kuwa makini uchaguapo mfuko wa pensheni



Mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii nchini inatakiwa kujiwekea malengo na mikakati mbalimbali ili kuleta ufanisi na tija katika shughuli za ulipaji wa mafao. 

Huu ni muda wa muafaka kwa mifuko kuanzisha utaratibu wa kuwa na mapatano ya utoaji wa huduma baina taasisi hizo na wateja wao kwa kuanzisha mikataba ya huduma kwa wateja kwa kutekelezwa kwa vitendo.


Ambapo mikataba hiyo inakuwa ni hatua muhimu sana katika utoaji wa huduma bora katika misingi ya uwazi na uwajibikaji. 

Kwa kufanya hivyo kwa mifuko wateja wao ambao ni wanachama, wastaafu na familia zao, na wageni wanaofanya kazi kwa mikataba watapata uhuru na uelewa wa kufahamu matarajio yao katika huduma zinazotolewa na mifuko 

Wateja watafahamu hata viwango vya muda ambavyo vitawawezesha kupanga mambo yao vyema kabisa bila kusumbuka, badala ya kusubiri huduma bila ya kufahamu upatikaji wake wa huduma hizo na kwa viwango fulani vilivyoanishwa wazi kwa wateja wa ndani na wa nje.

Mifuko kwa kufanya hivyo itawezesha kuwa na mapatano yatakayowawezesha wateja wao kufahamu huduma zinatolewa na mifuko, vikiwemo na hata viwango vya huduma na hatua ambazo mteja anaweza kuzichukua iwapo viwango vya huduma vitakuwa kinyume na matarajio ya mkataba.

Jambo la kuangalia kuhusu mifuko ni kujua bidhaa au huduma zake. Je huduma au bidhaa hiyo inahitajika na watu wote, chukua mfano wa fao la matibabu. 

Hivyo jaribu kujiunga na mfuko ambao huduma zake zinahitajika na wengi au wafanyakazi wengi na familia zao, pamoja na wazee, vijana, watoto, walemavu, wajane, pamoja na watoto yatima kwa kukidhi mahitaji yao wanapopatwa na majangwa ya aina mbalimbali. 

Lazima ujiulize kama huduma zinazotolewa na mfuko zina mbadala au hazina mbadala. Na hiyo huduma ina uhakika mkubwa wa soko. Ina nguvu kubwa ya ukiritimba ikiwa na maana ya kuwa na uwezo wa huduma kuwa na soko kubwa lenye uwezo wa kudai bei kubwa bila kupunguza uhitaji na matumizi. Hivyo jiunge na mfuko wenye huduma zenye sifa nzuri. 

Unahitaji kufanya uchunguzi wa kutosha au kina kuhusu utendaji wa mifuko hii hasa kwa kufanya utafiti wa kutambua thamani, soko, kutatua udhaifu, kutoa majibu ya maswali tata, kupata taarifa zaidi na za uhakika. 

Kujiunga na mfuko wowote wa hifadhi ya jamii ni kutafuta sehemu yenye usalama ya kuweza kuwekeza michango yako ya kila mwezi kwa ajili ya aina mbalimbali ya majanga yanayoweza kusababishwa na ugonjwa, kuumia ukiwa kazini, kifo, kupata ulemavu, na kadhalika. 

Hivyo unahitaji kufanya utafiti wa makini sana kwa kuchunguza taarifa mbalimbali juu ya mfuko huo unaotaka kujiunga nao ili taarifa hizo ziweze kukusaidia kutoa maamuzi wa busara wa kukuwezesha kuzingatia kanuni misingi na vigezo maalumu ambazo vitakusaidia kujibu maswali mengi. 

Baadhi ya maswali muhimu yanaweza kuwa kama vile utawezekeza wapi? Na mfuko upi, na watakata kiasi cha asilimia ngapi kutoka katika mshahara wangu, na mwajiri wangu yeye atatoa kiasi cha asilimia ngapi kama umeajiriwa. 

Hivyo ni juu ya mtu au mfanyakazi mwenyewe kama mwekezaji kufanya utatafiti wa kina ili kujua ubora wa mfuko huo unaotegemea kujiunga nao kabla ya kujisajiri. Unatakiwa usiwe mwepesi wa kufanya maamuzi bila kwanza kuwekeza kwenye utafiti hasa kama vile kuwaona wataalamu wanaoweza kukusaidia kukupa ushauri mahiri. 

Ni muhimu kuangalia mifuko hii ya pensheni kwa kuangalia uongozi, yaani menejimenti, hali ya kifedha, thamani ya mfuko wa pensheni kwa sasa, taarifa mbalimbali, matarajio ya mfuko wa pensheni  kwa kipindi kijacho kama pamoja na thamani ya mfuko wa pensheni kwa miaka ijayo.  

Uchambuzi unahitajika uwe unaolenga zaidi katika kuchambua thamani ya mfuko wa pensheni kutokana na taarifa halisi zilizopo na siyo taarifa za matarajio ya baadaye.

No comments :

Post a Comment