Thursday, November 19, 2015

Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa: Sikutegemea jina langu kuteuliwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli

Kassim-Majaliwa-559x520
WAZIRI Mkuu mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa.
……………………………………………………………………………………………………..
Na Ismail Ngayonga MAELEZO Dodoma
WAZIRI Mkuu mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa amesema hakutegemea nafasi ya jina lake kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa wa nafasi hiyo kubwa katika Serikali.
Alisema Uteuzi huo ulioidhinishwa na Bunge, umedhihirisha imani ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyonayo kwake iliyomwongoza katika kuliwasilisha jina lake Bungeni.
Akizungumza mara baada ya zoezi la uthibitisho wa uteuzi wa jina lake Bungeni Mjini Dodoma (leo), Mhe. Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa alisema kilichopo mbele yake kwa sasa ni kuwatumia Watanzania pasipo kujali itikadi ya vyama vyao.
Aliongeza kuwa mara baada ya kuanza kazi yake atahakikisha anazunguka katika mikoa mbalimbali nchini ili kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania na maendeleo yaliyofikiwa katika sehemu mbalimbali.
Aidha Mhe. Majaliwa aliwahakikishia Wabunge ushirikiano wa karibu zaidi katika kupokea ushirikiano ili kuweza kuwaletea maendeleo ya haraka Watanzania.
Awali akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa na Wabunge wa Bunge kwa ajili ya kuidhinisha jina hilo, Msimamizi wa jina hilo ambaye ni Katibu wa Bunge, Thomas Kashilill ah alisema katika uchaguzi huo, Mhe. Majaliwa alipata kura za Ndiyo 258 sawa na asilimia 73.5% ya kura zote.
Aidha Kashilillah alisema kura 91 sawa na asilimia 25% ya kura zote zilisema hapana wakati kura 2 sawa na asilimia 0.06% ya kura zote ziliharibika.
Wakizungumzia uteuzi huo, Wabunge mbalimbali Bunge la Jamhuri ya wamesifu uteuzi waMhe. Kassimu Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa kusema ni kiongozi mwadilifu, mchapakazi na asiye na makundi.
Wakizungumza kwa wakati tofauti mjini hapa katika mkutano wa Bunge mjini Dodoma, wabunge hao walisema, walisema uteuzi wa Mhe. Majaliwa ni chaguo sahihi katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuzingatia kauli ya hapa kazi tu.
Mbunge wa Ismani (CCM), Mhe. Wiliam Lukuvi alisema uteuzi huo umekuja katika wakati mwafaka kwa kuzingatia kuwa Mhe. Majaliwa amepata uzoefu wa kutosha katika katika Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI hivyo anao uelewa wa kutosha kuhusu matatizo mbalimbali ya nchi yetu ikiwemo sekta ya Elimu.
“Mhe. Majaliwa ni Mwalimu na mara zote Walimu ni watu wa kujifunza, amekuwa Naibu Waziri TAMISEMI kwa muda mrefu, amejibu maswali mbalimbali Bungeni yanayoihusu TAMISEMI na pia amezunguka katika maeneo mbalimbaliya nchi na kujinea matatizo ya Watanzania, hivyo ni chaguo sahihi”
Naye Mbunge wa Newala Mjini (CCM), Mhe. George Mkuchika alisema Mhe. Rais amaengalia vizuri kuhusu uteuzi wa Mhe. Majaliwa kwani, Mhe. Majaliwa ni kiongozi mwadilifu, mchapakazi na pia ni mmoja wa Viongozi aliyekuwa na ushirikiano na uhusiano wa karibu na Wabungewote wa Bunge lililopita, na hivyo ana imani kuwa uteuzi wakeutalisaidia Bunge katika kujenga umoja na mshikamano.
Aidha Mbunge wa Kaliua (CUF), Mhe. MagnalEna Sakaya alisema anamfahamu Mhe. Majaliwa kwa kipindi kirefu kama Kiongozi mchapakazi na aliye tayari kujishusha na kuwatumikia wananchi wote pindi kujali itikadi za vyama vya siasa.
“Namfahamu vizuri sana Mhe.Majaliwa kuliko mtu yeyote kwani amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo kwa kipindi cha miaka 5, ambapo alifanya kazi zake kwa ushirikiano mkubwa zaidi na wananchi, hivyo kuteliwa kwake kuwa Waziri Mkuu kutalisaidia Bunge na Serikali.”
Mhe. Sakaya alisema , anaunga mkono uteuzi wa Mhe. Majaliwa kwani ni kiongozi asiye na chembe ya ufisadi na iwapo Serikali ingewasilisha jina la Kiongozi mwenye kashfa, wabunge wa kambi ya upinzani wangeungana pamoja kupinga uteuzi wa kiongozi huyo.
Mbunge wa Msalala (CCM),Mhe. Ezekiel Maige alisema Mhe. Rais Joseph Magufuli amemteua mtu sahihi katika nafasi ya Waziri Mkuu, kwani kwa uzoefu alionao ikiwemo nafasi ya Naibu Waziri wa TAMISEMI na Mkuuwa Wilaya utaweza kumsaidia kusimamia shughuli mbalimbali za Serikali ndani ya Bunge.
Mhe.Maige alisema Mhe. Majaliwa ni miongoni mwa Viongozi walio mstari wa mbele katika ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za Taifa ikiwemo mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira “kuna wakati Fulani wakati ule akiwa Mkuuwa Wilaya alikoswakoswa msituni kutekwa na majangili wakati alipoongoza operesheni ya kuzuia majangili, hivyo ni kiongozi sahihi” alisema Mhe. Maige.
Mbunge wa Momba Mhe. Job Silinde alisema uteuzi wa Mhe. Majaliwa ni chaguo sahihi, kwani ni mtu aliye tayari kujishusha na kuwa karibu na watu wote pasipo na kujali itikadi ya vyama vya siasa, na hivyo Wabunge wote hawana budi kutoa ushirikiano kwake ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake.
“Mhe. Majaliwa amekaa TAMISEMI, na Ofisi ile ni Mhimili wa nchi, hivyo amepata uzoefu wa kutosha kuhusu nini maana ya Serikali na namna inavyoendesha kazi zake na umri alionao ni umri wa kati na ataweza kuendana na kasi ya Serikali itakayoundwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli.” Alisema Mhe. Silinde.
Mhe. Silinde alisema wakati akiwa TAMISEMI, Mhe. Majaliwa alikuwa Naibu Waziri na kuwa chini ya Viongozi wake, Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Pinda na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Hawa Ghasia, hivyo kupitia Viongozi hao amejifunza masuala mbalimbali ya Serikali ikiwemo usimamizi wa shughuli za Serikali Bungeni.

KOCHA MKWASA AWASHUKURU WATANZANIA

Kocha Mkuu wa timuya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Charles Boniface Mkwasa amewashukuru watanzania kwa kuwapa sapoti katika michezo miwili ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Akiongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume, Mkwasa amesema pamoja na kupoteza nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya makundi kuwania kufuzu kombe la dunia nchini Urusi mwaka 2018, anawashukuru watanzania wote kwa ujumla kwa sapoti waliyowapatia.
“Tumepotezea mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria, wenzetu walituzidi kiufundi, uwezo wa wachezaji binafsi ulikua chachu ya kuweza kuibuka na ushindi nyumbani kwzo, lakini bado watanzania waishio Algeria na washabiki waliokuja uwanjani walitusapoti katika mchezo huo” alisema Mkwasa.
“Tupo katika kipindi cha kujenga timu, tuna vijana wengi wanaochipukia, hivyo wanahitaji muda wa kucheza zaidi na kupata uzoefu, tuendelee kuwapa sapoti vijana hawa kwa ajili ya kujenga kikosi bora cha baadae” ameongeza Mkwasa.
Mkwasa amewaomba watanzania kuendelea kuwasapoti vijana, pamoja na matokeo mabaya dhidi ya Algeria, bado kuna nafasi ya kufanya vizuri katika michezo inayofuata ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2017.
Naye nahodha msaidizi wa Taifa Stars, John Bocco ameishukuru TFF kwa kuwapatia huduma bora za maandalizi na wakati wa michezo yao yote, amewashukru watanzania na vyombo vya habari kwa kuwapa sapoti na kuwaomba kuendelea kuwaunga mkono pindi wanapokua na majukumu ya kuiwakilisha nchi katika michuano mbalimbali.
“Matokeo ya juzi (dhidi ya Algeria) sisi wachezaji yametusikitisha, tulikua na malengo na mtazamo tofauti wa kupata ushindi, lakini katika mpira kuna matokeo matatu, tumepoteza mchezo huo kikubwa ni kujipanga kwa ajili ya michezo ijayo na watanzania muendelea kutusapoti timu ya Taifa kama ambavyo mmekua mkifanya kwa sasa” alisema Bocco.
Stars imerejea leo alfajiri ikitokea nchini Algeria ilipokua na mchezo wa marudiano dhidi ya Algeria, Jumanne katika uwanja wa Mustapher Tchaker mjin Bilda ambapo ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 7 -0.

No comments :

Post a Comment