Thursday, November 19, 2015

Hifadhi ya jamii Tanzania na sekta ya isiyo rasmi





Wanachama wachimba madini wadogo wadogo kutoka katika sekta isiyo rasmi wakifurahia na kinga dhidi ya majanga kwa kunufaika na mafao yote yatolewayo na mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii NSSF. Utafiti wa hivi karibuni unaonesha ya kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini imeweza kuwafikia wakulima na wachimbaji wa madini ambapo hadi sasa wachimbaji madini zaidi ya 7,000 wamejiunga na baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii. Picha na mtandao

Christian Gaya Mwananchi Alhamis, Octoba 2015
Idadi kubwa ya watanzania bado wanaamini ya kuwa hifadhi ya jamii ni stahili ya wafanyakazi waajiriwa tu, tena wafanyakazi wale wa kipato kikubwa. Ambapo kabla ya kuwa na sera ya hifadhi ya jamii na msimamizi na mdhibiti wa hifadhi ya jamii na kabla ya mabadiliko ya sheria za hifadhi ya jamii na maendeleo ya mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa mifuko kamili ya hifadhi ya jamii, sheria nyingi zilikuwa haziwajumuishi wafanyakazi kutoka katika sekta isiyo rasmi sheria hizo zilizokuwa zimepitwa na wakati zilishughulika na wafanyakazi walioajiriwa na kupata mshahara kwa mwezi tu.
Hifadhi ya jamii ni haki ya kila Mtanzania. Haki hii imeanishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 11(1) na Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003. Haki hii pia imeiainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu wa mwaka 1948 pamoja na mikataba ya shirika la kazi duniani (ILO) ibara ya 102 ya mwaka 1952.

Hivyo ni jukumu la mifuko kuondoa fikra ndani ya vichwa vya idadi kubwa ya watanzania kwa kuwaelemisha ya kuwa hivi sasa hifadhi ya jamii haina ubaguzi wa aina yeyote, kwa sasa hifadhi ya jamii ni fursa huru kwa wote, kwa walioajiriwa na kwa wale waliojiajiri. Mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa kujipanga kwa makusudi ya kuhakikisha ya kuwa inawaelemisha wananchi wote walio kwenye sekta isiyo rasmi na hata watu binafsi kuwawekea utaratibu wa wao kujiunga, kuchangia na kunufaika na mafao pamoja na vivutio vinavyotolewa na mifuko hii. Mifuko inatakiwa kuonesha kwa vitendo na mifano hai ya wakulima, wanafunzi, wavuvi na wajasiriamali namna wanavyochangia na wanavyofaidika huko mijini na vijijini.
 


Inajulikana ya kuwa watanzania wanatambua ya kuwa wengi katika sekta ya kilimo na sekta isiyo rasmi ambao kwa vipato vyao wanavyopata wangeweza kujiunga na mifuko nchini. Uzoefu huu unashawishi kuwa mifuko hii sasa itazame katika sekta ya kilimo. Kilimo ndio sekta mama ya uchumi wetu na mpaka sasa inaajiri zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wetu, lakini ukuaji wake ni asilimia 4.4 ambayo ni chini ya kiwango kinachotakiwa cha asilimia 6 kwa mwaka kutokana na kukosa uwekezaji wa kutosha. Ndio sababu, pamoja na kasi nzuri ya ukuaji wa uchumi ya wastani wa asilimia 7, umasikini umepungua kwa asilimia mbili tu.

Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha ya kuwa mifuko hii kwa mipango yao mbalimbali ya hifadhi ya jamii imeweza kuwafikia wakulima na wachimbaji wa madini ambapo hadi sasa wakulima 29,000  wachimbaji madini 7,000 wamejiunga na baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii nchini na wanafaidika na mafao yanayotolewa yakiwemo ya muda mrefu na ya muda mfupi ikiwemo na mikopo ya gharama nafuu. Kwa takwimu hizi za utafiti inaonyesha ya kwamba wananchi wengi wamekosa elimu ya hifadhi ya jamii na taarifa sahihi juu ya utendaji wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii hapa nchini. 

Hifadhi ya jamii katika nchi hii si jambo jipya au la kigeni, hata katika jamii zetu kabla ya kuja kwa mifumo hii rasmi ya hifadhi ya jamii, kulikuwepo na utaratibu wa jamii kujiwekea mifumo ya hifadhi ya jamii isiyo rasmi na mpaka sasa inafanya kazi vizuri na kutoa huduma nzuri ya kinga ya hifadhi ya jamii. Katika jamii zetu kulikuwepo na utaratibu wa kuwahudumia wazee, wasiojiweza na watoto mpaka leo ndani ya makabila na familia zetu za kitanzania bado zinaendelea kutoa huduma hizi za hifadhi ya jamii ingawa kwa kiasi fulani zimeathiriwa na ujio wageni na nguvukazi kubwa kuhamia mijini kutafuta kazi za kuajiriwa. Mtu hakupoteza heshima na thamani yake katika jamii kwa kuwa amepoteza uwezo wake wa kuchangia katika jamii, ama kwa kustaafu, kwa ajali au kwa kutojaaliwa uwezo wa kuchangia

.
Mabadiliko ya kidunia yameifanya mifumo hii ya hifadhi ya jamii isiyo rasmi sasa isiweze kuhimili jukumu hilo la kutoa kinga ya hifadhi ya jamii kwa wale wazee, akina mama wajawazito, walemavu, wajane, wagane, watoto yatima, na wengineo. Hivyo, mifuko ndio mbadala na salama ya ustawi wa jamii na utu wake au mtu katika dunia ya leo kuanzia tumboni mwa mama yake, utotoni, ujana, mpaka utu uzima. Utafiti unaonyesha ya kuwa mara nyingi shida na majanga huwafika watu wakati ambao hawajajiandaa vema. Na ikumbukwe wazi ya kuwa maandalizi ya kustaafu huaanzia pale unapoanza kufanya kazi uwe umeajiriwa au umejiajiri kwenye sekta iliyo rasmi au isiyo rasmi.

No comments :

Post a Comment