Tuesday, April 28, 2015

Mfuko wa ZSSF na uzinduzi wa fao la uzazi



 dk6



Christian Gaya, Majira Aprili 28, 2015

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Bi Fatma Ali Makame akiwa na mtoto wake mafao ya uzazi baada ya kuufungua mkutano wa kwanza wa Wadau wa ZSSF wa siku mbili katika ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Unguja (katikati) Mwenyekiti wa Bodi ya ZSSF Dkt,Suleiman Rashid.

Kutokana na kanuni na haki za uzazi na utaratibu wa shirika la kazi duniani (ILO) lengo la kubwa la kuwa na fao la uzazi ni kuhakikisha kuwa kazi za wanamke haziingiliwi na hali hatarishi ya afya ya wanamke pamoja na mtoto wake na kwamba shughuli za kuzaa hazikwamishi shughuli zao za kiuchumi za kila siku pamoja na usalama wa kazi zao ziwe za kujiajiri au kuajiriwa. 

Fao hili ni la muhimu sana kwa upande wamama kwani husaidia kupunguza vifo vya watoto na wamama wenyewe. Utafiti unaonesha ya kuwa idadi kubwa ya wamama wanaokufa kwa sababu ya kukosa huduma wakati wa kujifungua inaongezeka kila siku hasa kwa nchi zinazoendelea kama vile Tanzania. Na kwamba kati ya wajawazito kumi wanajifungua akina mama wanne hupoteza maisha pamoja na watoto wao. Na matukio haya yote hutokea nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania


Takwimu za hivi karibuni hapa nchini zinaonesha kwamba kwa mwaka, Tanzania inapoteza kina mama 7,900 kutokana na sababu zitokanazo na ujauzito. Idadi hiyo ni sawa na vifo 22 kwa siku.
Magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo vya wazazi nchini na mataifa mengine ni kifafa cha mimba, uzazi pingamizi, kupoteza damu nyingi wakati na baada ya kujifungua na maambukizi baada ya kujifungua.

Na elementi kuu za kinga za uzazi ni kama kupata likizo ya uzazi, kupata mafao taslimu ya kuhakikisha kuwa mama anaweza kujikimu yeye pamoja na mtoto wake wakati akiwa wa likizo ya uzazi, kuhakikisha kuwa anapatiwa matibabu, kuhakikisha ya kuwa mama mjamzito anapatiwa kinga ya afya ya ujauzito pamoja na mama anayeyonyesha bila kumsahau mtoto wake kupatiwa kinga kutokana na hali hatarishi zinazoweza kusababishwa na sehemu za kazi zenyewe. Mama mjamzito au anayeyonyesha ana haki kupewa kinga ya kutofukuzwa na kubaguliwa na kupewa kinga ya kwenda kunyonyesha mara tu baada ya kurudi kazini baada ya kurudi likizo yake ya uzazi 

Wanawake wengi wanakosa fursa ya kupatiwa malipo ya uzazi kabla ya kujifungua na hata baada ya kujifungua. Na wanawake wengi zaidi wanatishiwa kufukuzwa kazi na hata kubaguliwa. Lakini pamoja na hayo mazingira ya kazi, biolojia na kifizikia na kemia mbalimbali za madawa zinazosaidia kuzalishia kazi zinaweza kuleta hali hatarishi zaidi kwa upande wa uzazi na watoto wanaozaliwa hasa kwa kukosa mikakati ya uhamasishaji wa elimu ya umma, miongozo na thathimini juu ya kinga ya mama anategemewa kujifungua au aliyetoka kujifungua.

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeendelea kuchukua juhudi kubwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya madaktari na wataalamu wanaotoa huduma za afya kutoka madaktari 3,634 mwaka 2010 hadi kufikia 4,618 mwaka 2015 ambapo kwa mujibu wa madaktari wote wa sasa daktari mmoja anatoa huduma kwa watu 9,708. 

Ingawa SMZ imekuwa ikitoa taaluma kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa akinamama kujifungua hospitalini sambamba na kuondoa aina zote za malipo kwa akinamama wanaojifungua kwenye hospitali za Serikali.

“Kuanzishwa kwa fao la uzazi katika Mfuko wa ZSSF) ni matokeo ya juhudi za Serikali za kupambana na kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto nchini. Mfuko wa ZSSF unakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo katika mwaka 2012 alitangaza rasmi kufuta malipo kwa wajawazito wakati wanapojifungua katika hospitali zote Unguja na Pemba” Dkt Ali Mohamed Shein anasema.

Dk. Shein anaeleza ya kuwa utolewaji wa mfao hayo ya uzazi ni faraja kubwa kwa wanafamilia ambao ni wanachama wa ZSSF kwani kila mmoja anaelewa taabu wanayopata akina mama katika kipindi cha kabla na wakati wa kujifungua.

“Uamuzi huu wa kutoa fao na uzazi unakwenda sambamba na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuimarisha ustawi wa kinamama wajawazito pamoja na kupunguza vifo vya watoto ambavyo baadhi ya wakati husababishwa na umasikini unaopelekea watoto wakiwa tumboni kukosa mahitaji ya msingi kwa afya zao au huduma muhimu wakati wanapozaliwa na mara baada ya kuzaliwa”anasema Dkt. Shein.

Makame Mwadini Silima ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF  anasema mafao ya uzazi yatalipwa kwa wanachama wanawake waliotimiza vigezo vya  kuchangia kwa muda wa miezi 36, miezi sita iwe mfululizo kutoka tarehe anayoomba mafao, uthibitisho wa madaktari wenye kutambulika, vielelezo vya ushahidi wa kuthibitisha madai ya mafao, awe mjamzito ambaye ujauzito wake umefikia miezi 28, na awe amejifungua mtoto alie hai.

Anasema kuwa kigezo cha malipo hayo ya fao la uzazi ni asilimia 30 ya wastani wa mshahara wa mwezi wa wanachama wote wa Mfuko. Anasisitiza kuwa Mfuko utatangaza kiwango cha wastani wa mshahara utakao tumika kukokotoa mafao ya uzazi kila baada ya kufanyiwa tathmini ya afya ya mfuko.
Mfuko wa hifadhi ya jamii wa Zanzibar ulianzishwa mwaka 1998 kwa sheria Namba 2. Lengo la kuundwa kwa mfuko ni kulipa mafao ya muda mrefu na ya muda mfupi kwa wafanyakazi wa makundi mbalimbali ambao ni wanachama wake baada ya kukoma kwa ajira kutokana na sababu mbalimbali zinazoainishwa na sheria hiyo.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala ya hakipensheni. Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa barua pepe: gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment