Mkurugenzi mkuu wa mfuko wa mafao ya kustaafu Daudi Msangi
Christian Gaya Majira February 17.2015
Mojawapo ya malengo ya
mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii ni kulinda na kuhakikisha ya kuwa
pensheni za wanachama ziko katika hali ya usalama na zinapatikana kwa wakati
uliopangwa na kuhitajika na mwanachama, na kutoa habari kamili zilizokamilika
kwa wanachama wa mifuko ya pensheni na wategemezi wao.
Uwajibikaji ni sehemu
muhimu sana ya utawala bora, bila ya kuwa na mfumo mzuri wa uwajibikaji utawala
bora hauwezi kusimamiwa au kongezeka kwa ufanisi wake. Kwa kweli tunaweza
kusema kwamba utawala bora unabeba majukumu, uwazi na uwajibikaji mkubwa wa
kuendesha kampuni.
Mahitaji ya uwazi na
uwajibikaji kwa upande wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii ni kitu
kinachojionesha chenyewe. Kama mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii hauna
imani na kukosa kusaidiwa na waanzilishi au wachangiaji wa mfuko, kufanikiwa kwake utakuwa ni kidogo sana hata
kama unaendelea kuishi. Ijulikane ya kuwa, uelewo wa umma na kuwa na moyo wa
kupenda huenda ikawa ni kitu bora na muhimu sana kwa mfuko wa hifadhi ya jamii.
Kama kuna uwazi na
uwajibikaji mfumo wenyewe utategeneza mahitaji yote ya utawala bora. Utafiti
umefanywa kuchambua juu ya uhusiano kati ya mambo mbalimbali ya utawala wa
mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii kuhusiana na matokeo ya ufanisi mfuko wa
pensheni wa hifadhi ya jamii
Ingawa kumeonesha kuna
baadhi ya tofauti mbalimbali katika matokeo ya utafiti unaosema ya kuwa utawala
bora unasababisha matokeo makubwa kwa upande wa utendaji wa mfuko wa pensheni
ya hifadhi ya jamii. Na kwa upande wa matokeo mabaya ya utendaji wa mifuko ya
pensheni ya hifadhi ya jamii unasababishwa na viashirio au viindiketa vya kuwa
na utawala mbovu ndani ya mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii
Uwazi kwa umma na kutoa
taarifa yaani ripoti kwa washika dau wote unatakiwa kuwa ndiyo moyo wa mfuko wa
pensheni wa hifadhi ya jamii. Mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii unaundwa
kwa kutumia fedha zinazotokana na michango ya wanachama zikichangiwa moja kwa
moja na mwanachama na mara nyingine zingine kutoka kwa mwajiri wake zikiwa na
malengo ya kuja kumwandalia mafao ya kustaafu kwa siku zijazo. Umma au mwananchi
ambaye huenda ni mwanachama au mtegemezi anapenda kujua ni mambo gani
yanayotokea juu ya utendaji wa fedha au michango yake anayochangia kila mwezi
na kunaweza kiungwana kutokea kutegemea kupata nini kwa siku zijazo. mfuko wa
pensheni wa hifadhi ya jamii unaweza kuwa na aina nyingi ya wadau na uwazi
pamoja na uwajibikaji wa ngazi ya juu
vyote hivi vinaweza kutumika.
Wajibu wa mifuko ya
pensheni ya hifadhi ya jamii ni kuhakikisha ya kuwa inawashirikisha wadau wake
wote wakuu hasa waajiri, serikali na bila kusahau wanachama na familia zao
ambapo makundi hayo matatu yanaunda kitu kinachoitwa utatu. Wananchi lazima watambue
kuwa wawekezaji wa mifuko hii ni waajiri na wafanyakazi pale wanapojiandikisha
na kuwa wanachama wachangiaji kwa kukatwa asilimia fulani kutoka katika
mishahara yao na mwajiri na yeye kuchangia kiasi hicho hicho au zaidi kwa ajili
ya mfanyakazi wake kwa makubaliano ya kupata huduma mbalimbali za muda mfupi na
za muda mrefu kutoka katika kwa hiyo mifuko.
Na ndiyo maana mkurugenzi mkuu wa mfuko
wa kustaafu wa GEPF anatoa taarifa ya utendaji ya unaoishia June 2013
Kwa mwaka 2013 ulikuwa mwaka muhimu
sana katika historia ya Mfuko kwani waliweza kuandika upya sheria ya Mfuko
ambayo ilibadilisha muundo wa Mfuko kutoka Mfuko wa Akiba na kuwa Mfuko wa
Pensheni.
Mabadiliko ya muundo kutoka akiba
kuwa pensheni umewawezesha wanachama kupata mafao ya muda mrefu na muda mfupi.
Matokeo ya mabadiliko haya ni kuongezeka kwa mafao ikiwemo pensheni ya uzee,
pensheni ya warithi, pensheni ya kuumia kazini, fao la kifo, fao la elimu na
msaada wa mazishi. Mfuko pia umeanza kutoa mikopo ya nyumba kwa wanachama wake
kupitia mafao yao kama dhamana. Mfuko
unaendelea kuwa na ukuaji mzuri wa wanachama na thamani ya mali zake.
“Tumeongeza ubora wa huduma kwa
wateja kulingana na malengo tuliojiwekea kwa mwaka. Kwa miaka mitano mfululizo
tumeweza kufikia malengo yetu. Mafanikio
haya ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na wajumbe wa Bodi, Menejimenti,
wafanyakazi na muhimu zaidi wadau wetu mbalimbali ambao wamekuwa wakituunga
mkono wakati wote” mkurugenzi mkuu Daudi Msangi anasema.
Kulikuwa na ongezeko kubwa la
uandikishaji wa wanachama na ukusanyaji wa michango. Anasema kwa mwaka 2012/13
wanachama waliongezeka kwa asilimia 12.10 kutoka wanachama 52,670 mpaka wanachama
59,042. Ongezeko hili lilikuwa ni matokeo ya Mfuko kuendelea kufahamika
kutokana na elimu inayotolewa na
ubora wa huduma zetu kwa wanachama.
Eneo lingine ni ukusanyaji wa
michango ambao kama ilivyokuwa kwa ongezeko la wanachama, ukusanyaji uliongezeka
kwa asilimia 22.11 kutoka shillingi millioni 30,149.13 mwezi June 2012 na
kufikia shillingi millioni 36,816.18 mwezi Juni 2013. Ongezeko hili lilitokana
na wanachama wapya waliojiunga na Mfuko na ongezeko la viwango vya mishahara ya
wafanyakazi.
Skimu ya Lazima
Katika mwaka huu idadi ya wanachama
waliojiunga na Mfuko ilishuka, hata hivyo makusanyo yaliongezeka kwa asilimia
4.85 kutoka asilimia 17.26 na kufikia asilimia 22.11. Ongezeko hili ni matokeo
ya kuongezeka kwa mishahara ya wanachama na wanachama wapya waliojiunga na
Mfuko na waajiri kulipa michango mapema.
Idadi ya wanachama wanaojiunga na
Mfuko imekuwa ikiongezeka kila mwaka kutoka mwaka 2008/09 mpaka mwaka 2011/12
kabla ya kushuka mwaka 2012/13. Mwaka huu ulikuwa mwanzo wa ushindani baina ya
Mifuko na GEPF ilipata pigo kwa sababu ilikuwa Mfuko pekee wa Akiba na hivyo
kuwa na mafao machache. Hali hii inatarajiwa itabadilika baada ya Mfuko
kubadili mfumo na kuwa Mfuko wa Pensheni ambapo mafao ya muda mrefu kama
pensheni yataanza kutolewa
Skimu ya Hiari
Mfuko uliendelea na utekelezaji wa
Mpango wa Hiari wa Kujiwekea Akiba ya Uzeeni ambao uliingia mwaka wa tatu
katika kipindi cha 2012/13. Ili kupanua huduma na kuwafikia watanzania wengi
zaidi, Mfuko uliajiri wafanyakazi 18 na kufungua ofisi 3. Aidha Mfuko
ulianzisha dawati mahsusi kuhudumia wanachama wa hiari na ulipaji wa mafao kwa
wanachama wa aina hii na na kuendelea kutoa elimu kupitia warsha, semina na
namna nyingine tofauti za kuitangaza Skimu hii.
Kupitia hatua hizi, wanachama
wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2009/10 mpaka 2012/13.
Wanachama waliojiunga na Mfuko kwa mwaka 2012/13 ni 5656 ambao kwa pamoja
wanafanya idadi ya wanachama kufikia Juni 2013 kuwa 18,050. Kama ilivyokuwa kwa
usajili wa wanachama, michango kutoka kwa wanachama pia imekuwa ikiongezeka
mwaka hadi mwaka kutoka shilingi 1,839.00 milioni na kufikia shilling 3,050.80
milioni
Malipo ya Mafao
Malipo ya Mafao ni moja kati ya
gharama zinazototakana na huduma kwa wanachama. Kupitia huduma hii kiasi cha
shilingi milioni 9,162.62 kililipwa
kwa wanachama 1,955 ambao miongoni mwao wapo waliostaafu na wengine kujiunga na
pensheni. Uhamishaji wa wanachama kujiunga na pensheni umekuwa ukifanyika kwa
kuwa wakati huu Mfuko ulikuwa haulipi fao la pensheni.
Kuanzia mwaka 2008/09 hadi 2012/13
wastani wa asilimia 24.88 ya michango ya wanachama ililipwa kama mafao na hivyo
kubakiwa na zaidi ya wastani wa asilimia 75 ya makusanyo kwa ajili ya uwekezaji
Mkurugenzi anasema Mfuko utaendelea
kuhakikisha kuwa kiasi kinachokusanywa kama michango wakati wote kinazidi
mafao, ili kuhakikisha fedha kwa ajili ya uwekezaji zinapatika. “Hili
litawezekana kwa kuendelea kuongeza wigo wa wanachama na kuhakikisha kuna mahusiano bora kati ya Mfuko na waajiri ili
michango iwasilishwe kwa wakati” Msangi anabainisha
Uwekezaji na Mapato yake
Mkurugenzi mkuu anasema Mfuko
uliendelea kuwekeza katika maeneo manne ambayo ni vitegauchumi vyenye faida
inayojulikana kabla ya kuwekeza, hisa za makampuni, majengo (ardhi) na
uwekezaji wa pamoja. Jumla ya shilingi milioni 179,552.60 ziliwekezwa katika kipindi
cha mwaka huo na kuuletea Mfuko mapato ya shilingi milioni 18,253.99 ambayo ni
sawa na asilimia 10.17 ya fedha zote zilizowekezwa.
Uwekezaji katika vitegauchumi
Vitega uchumi vya aina hii
vinajumuisha amana za mabenki, hati fungani, amana za serikali na mikopo. Hadi
kufikia. Mpaka Juni 2013 Mfuko ulikuwa umewekeza jumla ya shilingi milioni
154,365.64 ikilinganishwa na shilingi milioni 119,279.03 zilizowekezwa mwaka
2011/12.
Msangi anasema uwekezaji huu ni sawa
na asilimia 85.97 ya fedha zote zilizowekezwa ambazo zilikuwa shilingi 179,552.60
milioni na kiasi kilichosalia sawa na asilimia 14.08 kiliwekezwa katika
vitegauchumi vingine. Wakati shilingi 80,788.96 milioni za kitanzania ziliwekezwa
katika amana za serikali, shilingi 57,316.00 milioni benki za biashara na
kadhalika.
Eneo lililoongoza kwa uwekezaji
mkubwa ni amana za serikali na amana za mabenki za muda mfupi ambapo kwa pamoja
uwekezaji ulifikia asilimia 76.92 ya fedha zote zilizowekezwa. Mapato
yanayotokanayo na uwekezaji huo yalikuwa shilingi milioni 17,510.37 sawa na ongezeko
la asilimia 60.09 kutoka mapato ya mwaka 2012 ya shilingi milioni 10,938.13.
Katika mapato yote ya uwekezaji, asilimia 46.08 ilitokana na amana za serikali
na asilimia 43.42 ilitoka na amana za mabenki za muda mfupi.
Uwekezaji katika Majengo
Uwekezaji katika majengo ulifikia kiasi cha shilingi milioni 13,864.62 hadi kufikia mwezi Juni 2013 sawa na ongezeko la asilimia 30.75 kutoka shilingi
milioni 10,603.88 zilizowekezwa hadi kufikia 2011/12.
Uwekezaji katika Majengo ulifikia
asilimia 6.99 ya thamani ya Mfuko. Vile vile katika mwaka 2012/13 Mfuko
ulifanikiwa kununua ekari 50 za ardhi katika eneo la Kijaka-Kimbiji Kigamboni
jijini Dar-es-salaam na ekari 40.54 za ardhi eneo la Njedengwa Dodoma.
Mkurugenzi anasema ardhi hiyo
itatumika kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya kuwauzia wanachama na
wananchi kwa ujumla. Wanachama watauziwa
nyumba hizi kwa pesa taslimu au mikopo kupitia mafao yao kama dhamana.
Uwekezaji katika Hisa
Anasema uwekezaji katika hisa
unajumuisha hisa katika makampuni yaliyoidhinishwa katika soko la mitaji la
Dar-es-salaam (DSE), ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni 2013, uwekezaji katika
hisa ulikuwa umefikia shilingi milioni 10,308.45 kutoka shilingi milioni
6,846.46 zilizowekezwa mwaka 2012. Uwekezaji huu ulionesha ongezeko la asilimia
50.57 ambalo lilitokana na kupanda
kwa thamani za hisa
Thamani ya Mfuko
Msangi anasema thamani ya Mfuko
imeongezeka kutoka shilingi milioni 154,410.99 mwezi Juni 2012 na kufikia
shilingi milioni 198,435.07, sawa na
ukuaji wa asilimia 28.50. “Kukua huku kwa Mfuko kulichangiwa na kuongezeka kwa
makusanyo ya michango na mapato kutoka katika vitegauchumi. Ukuaji wa mapato
yalitokana na vitegauchumi na matokeo ya uwekezaji makini unaozingatia
vitegauchumi vinavyolipa zaidi na salama”.
Gawio kwa Wanachama
Kifungu na. 8 cha Sheria ya GEPF ya
mwaka 1942 (R.E.2002), kinaitaka Bodi ya Mfuko kutangaza gawio kwa wanachama
kwa mwaka husika. Gawiwo hutolewa mara baada ya hesabu za Mfuko kukaguliwa na
kutambua faida iliyopatikana. Kwa mwaka 2012/13 Bodi ya Mfuko ilitangaza gawio
la asilimia 6.65. Moja ya malengo ya Mfuko ni kulinda thamani ya fedha za
wanachama ambao ndiyo sababu muhimu ya kutoa gawio. Kiasi kilichotolewa ni
kiasi kikubwa ikilinganishwa na kiasi kinacholipwa na taasisi nyingine za
fedha.
No comments :
Post a Comment