Christian Gaya, Majira Oktoba 28,2014
Mojawapo
ya nyumba 491 zilizopo katika mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ambazo
zinakopeshwa kwa wanachama wa PSPF na kwa umma kwa ujumla. Nyumba hizo zipo
katika eneo la Kigezi Kata ya Majohe wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Fursa ya kumiliki nyumba bora
iliyojitosheleza inatambuliwa na tamko la haki za binadamu duniani (1948
kifungu cha 26), kuwa nyumba ama makazi bora yanayojitosheleza ni haki ya
msingi, na ni muhimu ili kutunza utu wa binadamu yeyote. Nyumba bora
inayojitosheleza ni haki ya msingi kwa watu wote
Nyumba ya kujitosheleza iliyojengwa
kwa gharama nafuu, inaweza kujengwa na kumilikiwa na mwana jamii yeyote
anayejiingizia kipato iwapo tu
mwanajamii huyo ataona umuhimu na kuamua kujenga au kuboresha nyumba
yake.
PSPF inatambua jukumu kubwa la
serikali kuwawezesha wananchi kupata makazi, kuyalinda na kuyaboresha. Hivyo PSPF
inashirikiana na wananchi kwa kuwajengea uwezo wa kununua nyumba bora au
kuboresha makazi yao hata kuifanya hali hiyo iwe endelevu ili kila mmoja awe na
nyumba bora inayojitosheleza na ya gharama nafuu.
Ni wazi kuwa jamii za kiafrika
hususani wale waishio kusini mwa jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania, kwa muda
mrefu sasa imekuwa ikiishi katika makazi duni na yasiyojitosheleza. Ili kuwa na
nyumba au makazi bora yaliyojitosheleza, makazi husika lazima yawe katika ardhi
iliyopimwa ili kutambulika na kulindwa kisheria, yawe na huduma muhimu za
kijamii, miundombinu bora na jamii iweze kumudu gharama za ujenzi.
Makazi ya watu hayana budi kuwa na
huduma za kijamii ambazo ni endelevu, kuwa na usalama wa raia, faragha na
mazingira yasiyohatarishi kwa majanga mbalimbali kama mafuriko na magonjwa ya
milipuko.
Ongezeko la watu katika miji mingi
iliyopo katika nchi zinazoendelea ni matokeo ya watu na familia zao kuhamia
mijini ili kukidhi nguvu kazi inayohitajika kwa wingi katika sekta ya viwanda
Hivyo, watu wa aina tofauti waishio
mijini hutoa huduma mbalimbali muhimu
ikiwemo nguvukazi ambayo hufanya miji kukua, lakini kwa upande mwingine
inashangaza kuona watu hao ambao wengi wao ni wenye vipato duni na wachangiaji
wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii, huhangaika kutafuta sehemu za kuishi
zitakazo watosheleza ambazo ni bora na
nafuu.
Haki za watu hawa hupuuzwa na mara
nyingi wamekuwa wakitengwa na huduma muhimu za kijamii kama; ardhi salama,
makazi bora, ajira, umeme, maji safi n.k. Kutokana na mfumo huu wa kibaguzi
katika usambazaji wa huduma za kijamii, ni dhahiri kuwa tunahitaji kuwa na
mipango endelevu katika nchi yetu.
Mipango endelevu ambayo itapanga na
kusimamia usambazaji wa huduma za kijamii ikiwemo kuwa na nyumba bora na nafuu
kwa wote, hii itachochea kukua kwa uchumi wa watu binafsi na hatimaye taifa
kwa ujumla hivyo kupunguza kama si
kutokomeza umasikini unaoendelea kukua kwa kasi maeneo ya mijini.
Uwekezaji katika ujenzi wa nyumba na
makazi bora kwa wananchi wenye vipato vya chini ni muhimu kama miji ina malengo
ya kujenga uchumi endelevu kwa watu wote.
Maendeleo endelevu mijini hayawezi
kutenganishwa na uboreshaji wa makazi holela hasa pale watu wengi kama vile
wafanyakazi na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii wanapoishi katika
mazingira yanayotishia afya za familia zao. Ukweli ni kwamba makazi holela ni
matokeo ya kutokuwepo kwa nyumba ama ardhi zinazopatikana kwa gharama nafuu. Kutokana
na mabadiliko ya kiuchumi katika miji inayopanuka kwa kasi, usimamizi na
mipango miji ni muhimu sana.
Malengo ya milenia ya umoja wa
mataifa ya kuboresha maisha ya watu milioni 100 ifikapo mwaka 2020 kati ya watu
milioni 900 waishio katika makazi duni duniani, yatafikiwa ikiwa serikali na
taasisi mbalimbali zitashiriki katika kuwawezesha waishio katika makazi duni.
Neno miliki humaanisha hali ambayo
ardhi ama jengo kuwa katika himaya ya mtu au jamii fulani. Wakati miliki ya
ardhi humaanisha haki ya mtu au kundi la watu katika umiliki wa ardhi.
Kwa upande mwingine, miliki salama
ya ardhi ni makubaliano kati ya mtu na mtu ama kundi la watu juu ya ardhi au
makazi, makubaliano ambayo huongozwa na kuratibiwa na vyombo vya kisheria ama
uongozi fulani.
Mfuko wa pensheni wa PSPF unatambua
kampeni ya kimataifa juu ya miliki ardhi salama, ambayo malengo makuu ni
kuboresha hali za maisha ya watu waishio na kufanya kazi katika makazi holela
kwenye miji mikuu duniani. Ili kuunga mkono kampeni hiyo PSPF imekuwa
ikipigania upatikanaji wa makazi yenye
miliki salama.
Vilevile, PSPF inatambua na kuunga
mkono malengo ya milenia ya kuboresha
maisha ya watu wapatao milioni 100 wanaoishi
katika makazi holela ifikapo 2020. Kampeni hii ni chombo kilichoundwa
kwa lengo la kuchochea upatikanaji wa miliki salama kwa jamii masikini hususani
wale waishio katika makazi holela, ikiwa na lengo la koboresha maisha na
mazingira ya kazi kwa wananchi masikini waishio mijini kote duniani.
Shirika linaloshughulikia makazi
duniani (UN-HABITAT) linatambua miliki salama kuwa si dawa bali ni chanzo
muhimu cha kupunguza umasikini. Katika hali halisi watu waishio katika makazi
holela ni wazi kuwa miliki salama huchochea uwekezaji wa rasilimali walizonazo
kwa lengo la kuboresha makazi na huduma mbalimbali za kijamii.
Wakati mwingine hati au leseni ya
makazi inaweza kusimama kama chombo muhimu katika kudai rasilimali za umma au
kufanya majadiliano na mamlaka ya nchi juu ya usambazaji wa huduma za kijamii.
Pia, miliki salama huweza
kuhalalisha umiliki wa ardhi au jengo kama dhamana ya kupata mikopo na hatimaye
kuwekeza zaidi katika maendeleo. Miliki salama hutoa haki ya kumiliki. Mamlaka
ya nchi huwapa haki ya kuishi mijini bila bugudha wamiliki wa ardhi hasa kwa
wale waishio katika makazi holela.
Hati miliki haimfanyi mtu kuwa huru
kiuchumi tu, bali pia humfanya athaminike mbele za watu. Vilevile, huwafanya
wakazi wa mijini kujitambua na kutekeleza majukumu yao kama raia waishio
mijini.
Miliki salama, husimama kama chombo
kinachounganisha jamii na kuamusha uelewa wao juu ya mambo mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kujenga vikundi vya maendeleo katika nyanja tofauti za kidini,
kiuchumi, kijinsia, na kimazingira
Kwa upande mwingine, miliki salama
si sababu pekee inayoweza kutatua tatizo la watu kutokuwa na nyumba ama makazi
bora, umasikini, kuishi katika mazingira hatarishi ama nyumba
sisizojitosheleza.
Lakini pia, miliki salama ni moja ya
sehemu muhimu katika kujenga mkakati imara na endelevu juu ya kujenga na
kuboresha makazi ambayo yatatuletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi pia.
Hivyo, ni sababu tosha kuvutia wawekezaji wa ndani, hakuna mtu anayeweza
kuwekeza kama hakuna usalama unao muhakikishia kuwekeza. Uzoefu unaonesha kuwa
hata masikini wanaweza kuwekeza endapo wanakuwa na usalama wa kutosha, hivyo
miliki salama ni muhimu kwa maendeleo ya watu wenye vipato vidogo waishio
katika makazi duni.
Takwimu
zilizofanywa utafiti na Shirika la Nyumba la Taifa zinaonesha ya kuwa mpaka
mwisho wa mwaka 2007 Tanzania ilikuwa na upungufu wa nyumba zilizokisiwa kuwa
ni milioni 3 zenye thamani ya shilingi bilioni 180 ya fedha za Kimarekani
Kutokana na utafiti huo huo wa shirika
la nyumba la taifa takwimu vile vile zinaonesha ya kuwa mahitaji ya nyumba hasa
katika maeneo ya mjini ni nyumba 200,000 kwa mwaka zinazokisiwa kuwa ni zenye
thamani ya gharama ya shilingi bilioni 12 za kimarekani. Wakati takwimu zikionesha hivyo, ni asilimia 2 tu ya watu
wanaojenga kupitia mikopo ya nyumba huku asilimia 98 wakiwa wanajenga bila
mikopo. Wakati
kwa upimaji uliofanywa hivi karibuni unaonesha ya kuwa kwa sasa jiji la Dar es
salaam lina gharama kubwa kwa upande wa kupanga nyumba za makazi na ofisi
ukilinganisha na majiji jirani kama vile ya Nairobi na Afrika kusini
Makazi
ni moja ya mahitaji muhimu ya binadamu na kuna uhusiano wa karibu kati ya
makazi, afya bora na kupata fursa za kiuchumi kama mikopo. Katika utamaduni
wetu wa Kiafrika, kumiliki nyumba kunafanya ujisikie kuwa ni sehemu kamili ya
jamii. Hata hivyo, kutokana na hali ngumu ya maisha, wengi wao wamejikuta
wakimaliza ujenzi katika hali ya kujinyima na wengine kuishia njiani kutokana
na kukosa fedha.
Kukosekana kwa ubora wa nyumba
zinazojengwa na mafundi wa mitaani na wasio aminika kutoka sekta isiyo rasmi ya
ujenzi kazi nako kunachangia sana kwa kutomiliki nyumba imara hasa kwa kutumia
malighafi za ujenzi zisizo na ubora, kutozingatia ushauri wa kitaalamu,
kukosekana kwa usimamizi mzuri wa Serikali za mitaa kwenye ujenzi na kukosekana
kwa mwamko wa kuzingatia taaluma kwa wananchi wanaojenga.
Pia kukosekana kwa miundombinu
kama vile umeme, maji, simu, mfumo wa majitaka n.k. pamoja na viwanja kuuzwa
kwa bei za juu, serikali haiweki miundombinu yoyote kuyafanya maeneo hayo yawe
na gharama zilizojificha. Kujenga
maeneo holela na hatarishi, kushindwa kuandaa mpango kabambe kuzuia ukuaji wa
makazi holela pembezoni mwa miji. Wananchi wanajitwalia jukumu la kupanga
makazi wenyewe. Baadhi ya
watumishi wa serikali kama watumishi wengine kutoka sekta isiyo rasmi
wanalazimika kuishi kwenye chumba kimoja na familia zao kwa sababu ya kuzuiwa
na kodi za juu za nyumba za kupanga.
Mfuko wa PSPF unatoa
mikopo ya nyumba kwa ajili ya makazi kwa wanachama wake pamoja na mikopo ya
pensheni kwa wale waliostaafu kwa masharti nafuu. Mkopo kwa mwanachama wa PSPF aliyechangia
chini ya miaka mitano (5) ambapo atatakiwa kulipia kiasi cha shilingi milioni
tano za kitanzania (shilingi 5,000,000/=) kama malipo ya mwanzo ya nyumba na
kiasi kilichobaki anaweza kurejesha hadi muda wa miaka 25. Lengo la mkopo ni
kumwezesha wanachama kupata nyumba ambazo zimejegwa na mfuko ili kumhakikishia
mwanachama kuwa na uhakika wa makazi yake wakati anapoendelea kufanya kazi na
baada ya kustaafu. Mwanachama anaweza kununua nyumba kupitia akaunti ya mfuko
na kisha kusaini makubaliano kabla ya kuhamishiwa umiliki
Pamoja
na hayo yote mfuko huu wa PSPF ni mfuko pekee unatoa mkopo wa fedha taslimu kwa
mwanachama aliyebakiza miaka 5 kustaafu kwa lazima kwa ajili ya kujenga,
kukarabati na kununua nyumba ya makazi popote anapotaka yeye hapa Tanzania, ili
kuandaa makazi mazuri mara tu anapostaafu. Na mikopo hii ya pensheni ya kila
mwezi huwa inatolewa bila kutozwa riba ambapo mstaafu au mtegemezi ataweza
kukopa hadi pensheni ya miezi kumi na miwili (miezi 12) bila hata kutozwa riba
hata kidogo.
Ili
kuweza kulipa mafao na pensheni makubwa na kwa uhakika kama walivyoahidiwa
wanachama, wastaafu pamoja na wategemezi na kutunza thamani ya fedha mfuko wa
PSPF unawekeza katika vitega uchumi mbalimbali. Wakati wa kuwekeza huwa mfuko unazingatia misingi muhimu kama vile usalama,
faida, ujazo wa fedha, uwajibikaji katika jamii na uchumi, kuwekeza katika
vitega uchumi zaidi ya moja ili kuepuka upotefu wa fedha. Mafanikio makubwa ya
PSPF kuwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za hizi za makazi kwa ajili ya
kuwauuzia wananchi na kuwakopesha wanachama wake.
Mmoja wa wanachama wa PSPF
waliofaidika na mradi huu ambaye hakutaka kutaja jina lake anasema shukrani
zake za dhati kwa mfuko wa pensheni wa PSPF “Niliweza kuboresha nyumba yangu
baada ya muda mfupi kwa kutumia mkopo wa nyumba niliokopa toka PSPF ”
Mwalimu huyu mwanachama wa PSPF ni
mmiliki wa nyumba yenye vyumba kadhaa na amekuwa mfano katika jamii yake,
anaamini kuwa asingeweza kuwa na nyumba bora kama si huduma ya mikopo na nafuu
toka PSPF, iliyomwezesha kuboresha nyumba yake
Hivyo
basi mfuko wa pensheni wa PSPF unauza nyumba zake zilizojengwa kwa ajili ya
makazi katika mikoa ya Dar es Salaam-Ilala (Buyuni), Morogoro (Lukobe), Tabora
(Usule), Mtwara (Mang’amba), Shinyanga (Ibadakuli) na Iringa (Mawelewele).
Bei
za nyumba ni huuzwa kati ya sh. 52,000,000.00 hadi sh. 71,000,000.00 bila kodi.
Bei hizi ni kulingana na ukubwa wa nyumba na mkoa nyumba
ilipo. Ukubwa wa nyumba ni kuanzia vyumba viwili hadi vinne.
Ununuzi
kama mpangaji yaani hire purchase mnunuzi hulipia kwa mpango wa mwezi mmoja
mmoja au miezi mitatu kwa mkupuo kulingana na thamani ya nyumba. Katika mpango
huu, mnunuzi anaweza kulipia kutokana na vyanzo vingine vya mapato yake mbali
na mshahara wake.
Mwanachama
wa PSPF aliyechangia chini ya miaka mitano (5) hutakiwa kulipia kiasi
cha sh. 5,000,000.00 kama malipo
ya mwanzo ya nyumba na asiye mwanachama wa PSPF hutakiwa kulipia kiasi
cha sh. 10,000,000.00 kama
malipo ya mwanzo ya nyumba kukidhi vigezo vya kununua nyumba kama mpangaji.
Mpango
huu wa ununuzi kama mpangaji yaani hire purchase unamwezesha mnunuzi kulipa
kati ya sh. 450, 000.00 (laki nne na
hamsini tu) na sh. 813,000.00 (laki
nane na kumi na tatu tu) kwa mwezi kama malipo ya nyumba zinazouzwa na Mfuko
kulingana na ukubwa na eneo nyumba ilipo.
Malipo
ya mara moja yaani outright purchase, mnunuzi hulipia gharama ya kununua nyumba
kupitia akaunti ya Mfuko na kisha kusaini makubaliano kabla ya kuhamishiwa
umiliki.
Mkopo wa nyumba kupitia benki yaani
kwa mpango wa mortagage basis, Mnunuzi anaweza kuchukua mkopo katika mojawapo
ya benki ambazo Mfuko wa PSPF ina mikataba nazo na kutumia mkopo huo kununulia
nyumba. Mabenki hayo ni; CRDB, Azania, Exim na NMB. Tayari wanachama wengi
wamefaidika toka kuanza kwa mradi. Hapa
umuhimu ni kwamba iwapo mwanachama ananunua nyumba kupitia mkopo wa
benki anapaswa kuwa amesajiliwa kwenye Mfuko na kuchangia kwa muda wa miaka
mitano au zaidi. Muda wa kurejesha mkopo ni mpaka miaka ishirini na mitano (25)
kulingana na matakwa ya benki husika.
Kwa
mtu yeyote anayehitaji kuona au kukagua nyumba na kwa maelezo zaidi unatakiwa
kufika makao makuu ya PSPF yaliyopo jengo la Golden Jubilee Towers, Barabara ya
Ohio au ofisi za PSPF zilizopo katika kila mkoa.
Hata hivyo PSPF imekuwa ikikumbana
na mbalimbali katika utekelezaji changamoto wa mradi kama vile; uhaba wa
viwanja vilivyopimwa, huduma mbalimbali za ardhi, kutokuwepo kwa miliki salama
za ardhi, na uelewa mdogo juu ya huduma ya mikopo ya nyumba.
Wanashauri walengwa kutumia nafasi
hii ya mikopo ya nyumba ya gharama nafuu kama inavyo kusudiwa. Watu kutumia
fursa iliyopo kwa kukopa na kuboresha nyumba zao kwani mikopo ni nafuu na
itawasaidia kuongeza thamani ya nyumba zao kuwapa thamani na kuwafanya
wakubalike katika familia na jamii zao kwa ujumla. Watanzania itumieni nafasi hii popote mlipo
kutumia fursa zilizopo PSPF kuwawezesha kumiliki nyumba za gharama nafuu na
kuboresha nyumba zenu.
No comments :
Post a Comment