Tuesday, October 21, 2014

Ujue mpango wa uchangiaji wa hiari wa PSPF





                                             Mkurugenzi mkuu wa PSPF Adam Mayingu


Pensheni zinatolewa na mifuko iliyopo hapa nchini hazitoshelezi mahitaji ya watanzania wakiwemo wastaafu na familia zao.  Takwimu zilizotolewa mwaka 2012 zinaonesha ya kuwa ni watu milioni 1.7 tu ndio waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii wakati idadi ya watanzania wote ni milioni 44.9 hii ikiwa ni asilimia 6.5 tu ya nguvu kazi yote ya watu milioni 23.7.  Hivyo ni kwamba asilimia 93.5 ya watanzania wote wanaotegemewa kuwa ni milioni 44.9 hawana kinga ya hifadhi ya jamii ya aina yeyote.


Hifadhi ya Jamii ni haki ya kila Mtanzania. Haki hii imeanishwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 11(1) na Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003. Haki hii pia imeiainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu wa mwaka 1948 pamoja na mikataba ya shirika la kazi duniani (ILO) ibara ya 102 ya mwaka 1952.
Idadi kubwa ya watanzania hawana elimu ya hifadhi ya jamii inayoweza kuwaelemisha juu ya mafao yanayotolewa, wajibu wao, na haki zao za pensheni kwa ujumla. Kuna haja kubwa hata kuelemishwa juu umma juu ya kujiunga na mifuko ya pensheni ya ziadi ya kujiunga kwa hiari hata kama ni wanachama wa wachangiaji wa mifuko hii ya lazima kisheria. Kufuatia kupitishwa na sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Sheria Na. 8 ya mwaka, 2008 mtu yeyote anaweza kujiunga na mfuko wowote wa pensheni ya hifadhi ya jamii. Uanachama kwenye mifuko ya ziada iliyoruhusiwa na SSRA kuanzishwa na mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii ni ya hiari kwa mtu yeyote aliyeajiriwa au kujiajiri mwenyewe, mwanachama aliye katika mifuko mingine, na kwamba mwanachama wa mpango wa hiari anayo fursa ya kuhamia kwenye mpango wa uchangiaji kwa mujibu wa sheria.

Mfuko wa pensheni wa PSPF ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kwa sheria Namba 2 ya mafao la hitimisho la kazi kwa watumishi wa umma ya mwaka 1999

Mabadiliko katika sekta ya hifadhi ya jamii nchini yamepelekea kuwepo na mabadiliko ya sheria ya mfuko wa pensheni wa (PSPF). Sheria ya Mfuko wa pensheni wa PSPF sasa unaruhusu kusajili wanachama katika sekta zote za umma na binafsi. Na kwa sasa mfuko una mipango miwili ya uchangiaji wa lazima yaani PSPF Mandatory Scheme na mpango wa uchangiaji wa hiari yaani PSPFSupplementary Scheme yaani kwa kifupi PSS

Adam Mayingu ambaye ndiye Mkurugenzi mkuu anasema mwanachama wa mpango huu anastahili kulipwa michango pamoja na faida itakayopatikana kutokana uwekezaji ambayo huwekwa katika akiba mara mbili kwa mwaka yaani kwa mwezi wa Januari na Julai.
Anaongezea kwa kusema ya kuwa mpango huu wa hiari ni mahususi kwa ajili ya kuwapatia huduma ya hifadhi ya jamii wale wote ambao awali kutokana na matakwa ya kisheria hawakuweza kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. “Watanzania wachukue fursa hii kujiwekea akiba ya ziada hata kwa wale ambao tayari wamo katika mifuko mabalimbali ya hifadhi ya jamii hii itawasaidia kujiongezea na kutunisha na hivyo kunufaika na mafao ya muda mrefu na ya muda mfupi wakati wanapoendelea kufanya kazi na baada ya kustaafu,” anasema mkurugenzi mkuu.

Katika mpango huu wa uchangiaji wa hiari wa wa pensheni wa PSPF, mwanachama anapaswa kuchangia si chini ya Tshs 10,000 kwa mwezi. Michango inaweza kuwasilishwa kwa siku, wiki, mwezi au awamu. Mwanachama anawekewa gawio la akiba yake kwa kila mwaka mara moja. Uanachama ni kwa watanzania wote na wasio watanzania wanaofanya kazi nchini na hata waliopo nje ya nchi. Wanachama waliokwisha kujiunga na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii ikiwemo mfuko wa pensheni wa PSPF wanaweza kujiunga na mpango huu. “Hivyo wananchi wote mnakaribishwa kujiunga ili kufaidika  na mpango huu hiari wa
mfuko wa pensheni wa PSPF” mkurugenzi mkuu anasema.

Mayingu ambaye ndiye mkurugenzi mkuu wa PSPF anasema Mpango huu wa hiari umeanzishwa na mfuko wa pensheni wa PSPF kwa ajili ya kupanua wigo wa uwanachama kwa kuandikisha wananchi waliojiajiri au kuajiriwa katika sekta rasmi na isiyo rasmi mpango huu utawezesha wale wote ambao hapo awali hawakuweza kupata huduma ya hifadhi ya jamii kutokana na kutokua na ajira rasmi vilevile utawawezesha wananchi ambao tayari ni wanachama katika mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo kuweza kuwa na akiba za ziada.


Anasema hifadhi ya jamii ni haki ya kila mtu na si kwa wale tu walio katika ajira rasmi ila hata kwa wale waliojiajiri wenyewe na hata kwa wale ambao ni wanachama wa katika mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kuweza kuwa na akiba ya ziada.
“Kwa sababu mpaka sasa kulingana na takwimu zilizotolewa mwaka 2012 idadi ya watanzania wote ni milioni 44.9 ambao kati yao watu milioni 1.7 tu ndio waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, hii ikiwa ni asilimia 6.5 tu ya nguvu kazi yote ya watu milioni 23.7”. Ananukuu mkurugenzi mkuu.
Kwa vile hifadhi ya jamii ni haki ya kila mtu  mkurugenzi mkuu wa PSPF ndugu Mayingu anasema ndiyo maana mfuko wa pensheni PSPF tuna mpango wa uanachama wa hiari kama mkakati wa makusudi juu ya kupanua wigo wa hifadhi ya jamii ili kuhakikisha ya kuwa hata wale waliojiajiri kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa hiari na hata wale wanachama wa mifuko iliyopo kuweza kuwa na akiba ya ziada ya kutosha kwa baadaye.
Hili ni jambo ambalo liko wazi kabisa ya kwamba kila binadamu ana uhusiano mkubwa na hifadhi ya jamii iwe kinadharia au kivitendo kutoka kuzaliwa kwake mpaka kufa, binadamu mwenyewe lazima ajishughulishe na kazi hatarishi na kuugua magojwa mbalimbali   na kwa hiyo binadamu lazima akumbane na majanga mbalimbali kama vile majanga ya kiuchumi na ya kijamii yanayosababishwa na kukoma au kupungua kipato kutokana na maradhi, kujifungua mtoto, ajali za kuumia kazini, ukosefu wa ajira, ulemavu, uzee, kifo na kuongezeka kwa gharama za matibabu haya majanga yote ni matukio ya kila siku kwa binadamu ambayo hayatabiriki na yote yanaaangukia kwenye mpango wa hifadhi ya jamii. Hivyo ni kitu cha asili ya kwamba kila mtu lazima ajue hifadhi ya jamii ni nini kwa sababu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu

Na ndiyo maana mfuko wa pensheni wa PSPF unakaribisha wananchi wote wenye umri wa kufanya kazi, kuanzia miaka 18 na zaidi  walioajiriwa  katika sekta iliyo rasmi hata kama wanachama kwenye mifuko iliyopo hapa nchini au sekta isiyo rasmi yaani kwa wale waliojiajiri kama vile Wakulima, wafanyabiashara ndogondogo,wasusi,vinyozi,mamalishe,mafundi cherehani n.k.  kuwa wote wana haki ya kujiunga na mpango wa uchangiaji wa hiari wa mfuko wa pensheni wa PSPF

Mkurugenzi mkuu anasema uanachama wa mpango huu wa hiari wa PSPF ni kwa raia na asiye raia wa Tanzania anayefanya kazi nchini na nje ya nchi hivyo hauna ubaguzi nchi wala wa rangi ya mtu. Mayingu anakumbusha ya kuwa pamoja na hayo ni kwamba mfanyakazi anapaswa kuwa mwanachama wa mfuko mmoja tu katika mpango wa lazima, lakini ana haki ya kujiunga na mpango wa hiari zaidi ya mmoja kama huu wa mfuko wa pensheni wa PSPF.
Anasema aina za mafao yanayo tolewa na mpango huu wa hiari chini ya mfuko wa pensheni wa PSPF ni kama vile fao la uzeeni, fao ya kuumia kazini, fao la kifo, fao la elimu, fao la ujasiriamali, fao ya urithi, fao ugonjwa/ulemavu, na  fao la kujitoa. Mayingu vile vile anasema mafao haya hutolewa na kunufaika sawasawa bila kujali ya kuwa mwanachama anachangia kwa hiari au kwa lazima kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii.

“Hivyo mtu yeyote aliyejiajiri, mkulima, mvuvi, mfanyakazi wa ndani, wafanya biashara wadogo wanaweza kujiandikisha kwa hiari na kulipa kadri ya uwezo wake wa mapato kwenye mfuko wa pensheni wa PSPF. Uchangiaji katika mpango huu wa hiari wa PSPF Wanachama wana uhuru wa kuchagua jinsi ambavyo wanaweza kuwasilisha michango yao, iwapo ni kwa wiki Mwezi au kwa msimu kutegemea na upatikanaji wa kipato cha ziada kwa ajili ya akiba na michango huwasilishwa moja kwa moja kupitia akaunti ya benki au wakala wa malipo wa M-pesa, Tigo-pesa na Airtel money. Na kiwango cha uchangiaji ni kuanzia shilingi 10,000 za kitanzania  au zaidi”. Mkurugenzi mkuu anabainisha.
“NIMEJIUNGA kuwa mwanachama wa hiari katika Mfuko wa Pensheni wa PSPF, kwa kuwa kuna utaratibu baada miezi 12 unaweza kuchukua fedha zako,” anaanza kueleza, Charles Lucas mpiga picha wa gazeti la majira ’ alipozungumza na Kituo cha HakiPensheni .
Lucas ambaye ni mwanachama wa mfuko wa hiari wa PSPF na mpiga picha mwandamizi wa gazeti la majira, anasema ni muhimu kwa wajasiriamali na watu wengine walio katika sekta isiyo rasmi kujiunga na mfuko huu wa PSPF ili waweze  kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo kwa kwamba yeye ana  wasilisha michangi yake kwa wiki, mwezi au msimu kutegemeana na upatikanaji wa kipato cha ziada kwa ajili ya akiba.

Anasema mtu yeyote anaweza kuwa mwanachama kwa kujiunga na mpango huu wa hiari kwa kujaza formu PSS FN.1 na kuambatanisha picha moja ya rangi yaani passport size pamoja na taarifa muhimu za wanachama kama vile; majina; tarehe ya kuzaliwa;  anwani na nambari za simu; shughuli au kazi na mara baada ya kukamilisha usajili, mwanachama hupewa kitambulisho na nambari ya uanachama

“Katika mpango huu wa uchangiaji hiari wa mfuko wa pensheni wa PSPF mwanachama akisha anza kuchangia naye anakuwa na haki ya kupata mafao yote yatolewayo na mpango huu wa hiari wa PSPF”.Mayingu anabaisha wazi
Mkurugenzi mkuu anasema mafao katika mpango huu wa hiari mwanachama huwa anastahili kulipwa michango pamoja na riba inayokokotolewa kwa mujibu wa viwango vya riba vilivyoko katika soko kulingana na mfumuko wa bei na kwamba riba ambayo ni asimilia sita (6) huongezwa katika akiba ya mwanachama mara mbili kwa mwaka katika miezi ya Januari na Julai

Na anaendelea kubainisha ya kuwa mafao yaliyopo katika mpango wa hiari ni ya aina sita  (6) kama vile fao la elimu ambalo litatolewa kwa mwanachama ambaye amechangia kwenye mfuko kwa kipindi kisichopungua miezi 12.

“Nusu ya akiba ya mwanachama yaani asilimia 50 ya mchango itatumika kulipa fao hili na nusu itabaki katika akaunti ya mwanachama kwa ajili ya akiba ya uzeeni na mwanachama anapaswa kuandika barua ya maombi.

Kwa upande wa fao la ujasiriamali huwa linatolewa kwa mwanachama ambaye amechangia kwenye mfuko kwa kipindi kisichopungua miaka kumi na mbili (12) na nusu ya akiba ya mwanachama yaani asilimia 50 ya mchango inatumika kulipa fao hili na nusu yake inayobaki katika akaunti ya mwanachama hutumika kwa ajili ya akiba ya uzeeni na vile vile mwanachama atapaswa kuandika barua ya maombi.

Anasema mpango huu wa hiari Mwanachama anapata hata fao la uzeeni ambalo hulipwa kwa mwanachama aliyefikisha miaka 55 au zaidi. Mwanachama analipwa akiba yake ya asilimia mia moja (100%) pamoja na riba itakayokokotolewa. Mwanachama anapaswa kuandika barua ya maombi na kuambatanisha kitambulisho cha uanachama.

“Wakati fao la kifo hulipwa kwa wategemezi wa mwanachama aliyefariki. Malipo yanayolipwa ni ya asilimia mia moja (100%) ya akiba ya mwanachama na riba inayokokotolewa. Wategemezi wanapaswa kuwasilisha cheti cha kifo, kitambulisho cha uanachama za marehemu pamoja na nyaraka za mahakama zinazodhibitisha msimamizi wa mirathi na wategemezi wa marehemu. Aidha mpango wa mirathi unahitajika kutoka mahakamani”. Mkurugenzi mkuu anataja

Anaendelea kwa kusema ya kuwa fao la ugonjwa au ulemavu huwa linatolewa kwa mwanachama ambaye kutokana na sababu za ugonjwa au ulemavu hataweza tena kumudu kufanya kazi za uzalishaji kwa ajili ya kujipatia kipato cha kila siku. Mwanachama analipwa asilimia mia moja (100%) ya akiba yake pamoja na riba inayokokotolewa. Mwanachama anawasilisha barua ya maombi, kitambulisho cha uanachama na uthibitisho wa taarifa ya daktari

Kwa upande wa fao la kujitoa anasema fao hili linalipwa kwa mwanachama anayetaka kujitoa. Mwanachama analipwa asilimia mia moja (100%) ya akiba yake pamoja na riba itakayokokotolewa. Mwanachama anatakiwa kuuarifu mfuko kuhusu kujitoa kwa njia ya barua na kurejesha kitambulisho cha mfuko.
Anasema mwanachama wa mpango huu wa hiari wa PSPF anapolazimika kuchukua michango yake yote na faida kutokana na sababu zozote zile, anaweza tena kuchangia upya bila masharti yoyote,” alisema.

Mkurugenzi mkuu  anasema ya kwamba uanachama ni wa hiari kwa mtu yeyote aliyeajiriwa au kujiajiri mwenyewe, mwanachama aliye katika mifuko mingine, na kwamba mwanachama wa mpango wa hiari anayo fursa ya kuhamia kwenye mpango wa uchangiaji kwa mujibu wa sheria ya mfuko wa pensheni wa PSPF

Akizungumzia mwamko wa watu kujiunga na mpango huu wa hiari yaani wa PSS, Mkurugenzi mkuu anasema kumekuwa na mafanikio makubwa kwani tangu kuzinduliwa kwake mapema machi 7 mwaka 2013 tayari wanachama zaidi ya 5,000 wamejiunga na mpango huo. “Makundi zaidi ya 25 yamejiunga na mfuko huu kutokana na ubora wa mafao yake na mikopo inayotolewa kwa wanachama waliojiunga na mfuko huo kwa miaka mitano tofauti na wakati wa nyuma ambapo mikopo ya nyumba ilitolewa kwa wanachama waliobakiza miaka mitano ya kustaafu” anasema .

Anasema ya kuwa mfuko wa pensheni wa PSPF una uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya hifadhi ya jamii tangu ulipoanzishwa mfumo wa hifadhi ya jamii usio wa kuchangia wa pensheni mwaka 1954 hadi mfuko wa pensheni wa PSPF ulipobadilishwa mwaka 1999 kuwa mfuko wa pensheni unaojitegeme. Mkurugenzi mkuu  anaongeza ya kuwa, watanzania wasiwe na wasiwasi kwa kuwa thamani ya mfuko inaongezeka anatolea mfano ya kuwa mwaka 2000 thamani ya mfuko ilikuwa fedha ya kitanzania shilingi bilioni 36, na  mpaka mwaka huu 2014 imefika fedha za kitanzania shilingi trilioni 1.25

“Dira ya mfuko wetu wa PSPF ni kuwa mtoa huduma bora wa huduma za hifadhi ya jamii nchini kwa dhima ya kutoa huduma zenye ushindani katika sekta ya hifadhi ya jamii kwa wateja wao kwa kutumia watumishi wenye ari ya kazi  na teknolojia inayofaa. Maadili Yetu ni kuhakikisha ya kuwa Mfuko unatoa huduma zake kwa wateja, wadau na umma kwa kuzingatia misingi ya Uwajibikaji, Wajibu, Muitikio, Nidhamu, Juhudi. Uwazi na Unyenyekevu kwa wote”. anataja

No comments :

Post a Comment