Thursday, January 16, 2014

NSSF na fao la kuumia, magonjwa kazini





Daktari Ramadhani Dau Mkurungenzi mkuu wa NSSF 

Na Christian Gaya majira 14 januari 2014
Mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii wa NSSF ulianza kama idara ya serikali mwaka 1964 kabla ya kuanzishwa kama shirika la taifa la akiba ya wafanyakazi (NPF) kwa sheria Na 36 ya mwaka 1975. Shirika hili liliendelea hadi pale serikali ilipopitisha sheria Na 28 ya mwaka 1997 iliyoanzisha shirika la taifa la hifadhi ya jamii (NSSF) kama mpango kamili wa hifadhi ya jamii unaozingatia kanuni za kimataifa za hifadhi ya jamii 


Mabadiliko hayo yameiwezesha NSSF kutoa mafao mengi na bora zaidi yakiwemo pensheni ya ulemavu na fao la kuumia kazini na magonjwa yatokanayo na kazi kwa wanachama wake na kuongoza kwa afrika mashariki na kati. Sheria hii ya kuumia kazini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (Na. 28 ya 1997), ilianza kutekelezwa mwaka 2002. 


Tanzania imeanza kuwahusisha wafanyakazi wa sekta zisizo rasmi katika sheria za kazi ili kuwapatia kinga kama vile za hifadhi ya jamii au haki za msingi kama vile likizo ya uzazi, likizo ya ugonjwa na ruzuku ya serikali pindi wanapokuwa hawana kazi. Hata hivyo, inaweza kuwa vigumu sana kutekeleza sheria hii katika nchi yetu kama vile OSHA ambacho ndicho chombo cha kusimamia wa sheria za kazi hawana vitendea kazi au rasilimali za kutosha za kufanyia kazi zao na mifumo ya taarifa/habari ni duni.Aidha, wafanyakazi wengi wa hawajui haki zao, hivyo hawawezi kudai ulinzi au haki zao kutoka kwa waajiri wao.
 

Tanzania imeridhia Mkataba wa Ukaguzi Kazini, 1947 (Na. 81), na Itifaki Na. 81 ya 1995 katika Mkataba wa Ukaguzi wa Kazi, na sheria nyingine husika. Mfumo wa kisheria uliopo unaundwa na Sheria ya Afya na Usalama Kazini ya mwaka 2003 na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ya mwaka 2008. Kwa mara nyingine, kuwepo kwa mfumo huu na hatua hizi zilizochukuliwa na Serikali kunaonyesha maendeleo yaliyo katika jambo hili. 


Kwa upande wa sheria na kanuni za afya na usalama katika maeneo ya kazi (OHS), Tanzania kama nchi endelevu. Tanzania hivi karibuni ilipitisha sera ya Afya na Usalama Katika Maeneo ya Kazi (OHS) ambayo inafuata Mkataba 155 wa ILO yaani Shirika la Kazi Duniani katika kufafanua sehemu yoyote ambayo watu wanapata maisha au kipato kama mahali pa kazi. 


Tanzania imeanzisha mfumo wa huduma za msingi za afya ya umma ambao unajumuisha huduma za afya na usalama makazini kwa wafanyakazi wote, iwe rasmi au isiyo rasmi, na inatakiwa kuwa na mfumo wa ukaguzi wa kazi ambao unajumuisha sehemu zote za sekta rasmi na zisizo rasmi. 


Katika viwanda, idadi ya ajali kazini iliongezeka ghafla kutoka 90 mwaka 1999 hadi 309 mwaka 2008, kuanzia yale yenye idadi ndogo hadi yale yenye idadi kubwa ya ajali miongoni mwa sekta tatu zilizochunguzwa. Kinyume chake, sekta ya biashara, na hususan sekta ya huduma, imeonesha mwelekeo wa kupungua kwa ajali katika miaka yote, ingawa kuna mabadiliko kila mwaka.


Idadi kubwa ya ajali zilizoripotiwa hazikusababisha vifo, na hakukuwa na mfululizo wa ajali kazini zilizosababisha vifo katika miaka hiyo, hii ilikuwa wastani wa karibu ajali 22 kwa mwaka, vilevile kukiwa na mabadiliko kila mwaka. Wakati wote katika miaka hiyo, viwanda vimekuwa na idadi kubwa zaidi ya ajali zilizoripotiwa kusababisha vifo, kwa wastani wa ajali 12 kila mwaka. Kwa kuwa sekta ya kilimo ambayo huajiri idadi kubwa ya wafanyakazi inajulikana kuwa na viwango vikubwa vya ajali, kama ingeingizwa ingeonesha idadi ya ajali kuwa kubwa. 


Idadi ya wakaguzi wa kazi ni ishara ya uwezo wa Serikali kusimamia kanuni, sheria na taratibu za usalama kazini. Mamlaka ya Usalama na Afya Kazini (OSHA), chini ya Wizara ya Kazi Ajira na Maendeleo ya Vijana, inaendesha ukaguzi wake wa viwanda. Inasemakana kuwa wakaguzi wa kazi, ukiondoa wale walioajiriwa na OSHA, wamebaki kuwa wachache kwa idadi ya wastani 70 nchini Tanzania katika kipindi kuanzia mwaka 2005 hadi 2009. Vilevile, kama wakipangwa kulingana na ajira, idadi ya wakaguzi wa kazi ni ndogo sana na inazidi kupungua: Tanzania (bara) ilikuwa na 0.33 ya wakaguzi wa kazi kwa kila wafanyakazi 10,000 wa kulipwa, au wakaguzi wa kazi 0.04 kwa kila watu 10,000 walioajiriwa.


Hii inaonyesha kuwa wakaguzi wa kazi bado hawatoshi nchini Tanzania. Hii inatoa nafasi ya ajali nyingi kutokea au mazingira mengine ya kazi yasiyo salama kutokea bila kuripotiwa ili hatua sahihi ziweze kuchukuliwa ili kuimarisha mazingira ya kazi yenye staha.


Licha ya kuwepo Sheria ya Usalama na Afya Kazini ya mwaka 2003 yaani OSHA na kuundwa kwa Wakala wa Usalama na Afya Kazini, suala la kazi salama halijashughulikiwa vya kutosha, kama inavyoshuhudiwa na kuwepo kwa wakaguzi wachache sana wa kazi na ukosefu wa raslimali


Hapo awali, maafisa kazi walitakiwa kwa upande mmoja, kuendesha ukaguzi na uchunguzi wa kazi na, ikibidi, kuwashtaki waajiri katika mahakama na, kwa upande mwingine, kuwa wenyeviti wa tume za usuluhishi na maamuzi ambazo zilikuwa zikiwabana waajiri. Kazi za wakaguzi wa kazi kwa sasa zimetenganishwa na zile za wasuluhishi na waamuzi. Kuna haja ya kuajiri zaidi wakaguzi wa kazi, kuamsha ufahamu miongoni mwa wafanyakazi na waajiri kuheshimu sheria.


Mapato ya chini na na ukosefu wa ulinzi au uzingatiwaji wa haki unamaanisha kwamba wafanyakazi wengi hapa nchini wapo katika mazingira magumu. Endapo itatokea wakaugua au kuumia na hivyo kushindwa kuja kazini, wengi wanapoteza mishahara au ujira wao au kufukuzwa kazi. 


Na mara nyingi wanakuwa hawana kinga ya hifadhi ya jamii au akiba ili kulipa bili za matibabu na kuwafanyia ukarabati wa viungo bandia au kuwafanya waendelee na maisha mpaka watakapopata kazi mpya. Hali hii inaweza kuonekana isiyo ya haki kabisa hususani kwa wafanyakazi ambao awali ya yote, chanzo cha ugonjwa au kuumia ni hiyo kazi yenyewe.


Wamiliki wa mahali au sehemu za kazi ambapo wafanyakazi wanafanyia kazi zao wanaweza kufikiri mahali pa kazi zao ni maeneo salama, lakini sehemu hizo hizo zinaweza kuwasilisha matatizo kadhaa ya kiafya na ki-usalama kwa watu wanaofanya kazi ndani mwake. 


Wafanyakazi wa sekta zisizorasmi wanatambua kwamba kazi zao zinaweza kuwa hatari kwa afya zao. Utafiti wa hivi karibuni huko California ulionyesha karibu wafanyakazi wawili kati ya watatu wa sekta zisizo rasmi walioshiriki wanachukulia kazi zao kuwa “zenye hatari/hatarishi” (Smith 2001).


Taratibu au sheria za Afya na Usalama katika Maeneo ya Kazi yaani OHS, ambazo zimelenga katika kuzuia hatari za kuumia au kupata ugonjwa katika sehemu za kazi, mara nyingi zinawalinda wafanyakazi rasmi waliopo katika mazingira rasmi ya kazi kama vile migodini, viwandani, ofisini na madukani.


Kanuni hizi haziwalindi wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika sekta zisizokuwa rasmi, kitu ambacho kinamaanisha kwamba japokuwa kazi za sekta zisizo rasmi ni chanzo muhimu cha ajira, na ingawa kuna hatari nyingi za kiafya na kiusalama katika kazi hizo, na japokuwa wafanyakazi hao wapo katika mazingira magumu ya umasikini endapo wataugua au kuumia, taratibu au sheria za OHS katika nchi hii ya Tanzania haziwazingatii.


Ili kutatua tatizo hili la kuumia na kupatwa na ulemavu na magonjwa yatokanayo na mahali pa kazi shirika la taifa la hifadhi ya jamii yaani NSSF linatoa mafao ya kuumia kazini na magonjwa yatokanayo na kazi. Sheria hii ya kuumia kazini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (Na. 28 ya 1997), ilianza kutekelezwa mwaka 2002;


Mkurugenzi mkuu daktari Dau Ramadhani anasema mafao haya hulipwa kwa mwanachama aliyepata ajali akiwa kazini au magonjwa yatokanayo na kazi anayoifanya na anazitaja sifa zake zinazotakiwa ya kuwa awe tayari alishaandikishwa na NSSF kama mwanachama na awe ameumia kutokana na kazi anayoifanya au kupata magonjwa yatokanayo na kazi yake.
Pamoja na haya yote ni kwamba NSSF hutoa fedha taslimu kama mojawapo ya mafao kwa mwanachama aliyepata maumivu ya muda. Mafao yanayotolewa ni 60% ya wastani wa mapato yake ya siku, na mafao haya hulipwa kwa muda usiozidi wiki 26 tangu tarehe ya kuumia au kupata ugonjwa, na kwamba kwa mwanachama aliyepata maumivu ya kudumu yaani maumivu ya 100% ya uwezo wake wa kufanya kazi, mafao yanayotolewa ni 70% ya wastani wa mapato yake ya mwezi. Malipo hufanyika kutegemea viwango vya kuumia kama vilivyoelewa katika Kanuni za NSSF za mafao haya Daktari Dau anasisitiza


Daktari Dau ambaye ndiye mkurugenzi mkuu wa NSSF anasema vile vile Shirika hutoa viungo bandia kwa ajili ya kumsaidia mwanachama iwapo vitahitajika kama vitakavyoelezwa na Madaktari wanaohusika. Viungo hivi ni vile vinavyopatikana katika hospitali zilizopo ndani ya Tanzania


Anaongezea na kusema ya kuwa siyo tu shirika hutoa mafao ya   kuumia kazini na kupatwa na magonjwa yatokanayo na kazi NSSF vile vile hutoa hata pensheni ya ulemavu pale mwanachama anapogundulika ya kuwa amepatwa na ulemavu kwa sababu ya kazi aliyokuwa akifanya, anasema ya kuwa  pensheni hii hulipwa kwa mwanachama aliyepoteza angalau 2/3 ya uwezo wake wa kufanya kazi kutokana na ulemavu wa kimwili au kiakili kama utakavyothibitishwa na Bodi ya Madaktari


Mkurugenzi mkuu anaainisha sifa zinazotakiwa ya kwamba kunahitajika kuwa na uthibitisho wa Bodi ya Madaktari wa kupoteza 2/3 ya uwezo wa kufanya kazi. Michango 180 au angalau 36 kati yake michango 12 iwe imelipwa karibu na kupata ulemavu na awe chini ya umri wa kustaafu yaani miaka 60 ya kustaafu kwa lazima


Dau anaeleza kwa kina ya kwamba mafao yanayotolewa chini ya pensheni ya ulemavu ukokotoaji ni wake ni sawa na ule wa pensheni ya uzee isipokuwa huongezwa 1% kwa kila michango 12 inayozidi kiwango cha michango 180, na mafao yanayotolewa ni sawa pia na mafao ya pensheni ya uzee yaani pensheni ya kila mwezi, mkupuo wa awali na mkupuo maalum kwa aliyekosa sifa zinazotakiwa na pensheni hulipwa hadi mwanachama atakapofariki au atakapotimiza umri wa kustaafu na kuhamia pensheni ya uzee.


Anasema ingawa Waajiri wanaohusika kisheria kuandikishwa katika mfumo wa taifa wa hifadhi ya jamii wa NSSF ni waajiri wote walio katika sekta binafsi, taasisi zisizokuwa za kiserikali, ofisi za kibalozi zinazoajiri watanzania, taasisi za kimataifa zinazofanya shughuli ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, taasisi za wizara za serikali zinazoajiri wafanyakazi kwa masharti ya muda, mashirika ya umma yanayoajiri wafanyakazi kwa mashari ya muda. Watu binafsi waliojiajiri wenyewe, sehemu yoyote ya shughuli kama mwajiri mlipa michango na kupewa namba ya uandikishaji mara tu anapoanza shughuli zake 


“Lakini hata mtu yeyote aliyejiajiri, mkulima, mfanyakazi wa ndani, wafanya biashara wadogo wanaweza kujiandikisha kwa hiari na kulipa kadri ya uwezo wake kuanzia shilingi 20,000 kwa mwezi asilimia 20 ya mshahara wa kima cha chini (KCC) wa serikali na atapata mafao yote saba yatolewayo na mfuko wa hifadhi ya jamii ikiwa na pamoja na kunufaika na mafao ya kuumia kazini na magonjwa yatokanayo na kazi na pensheni ya ulemavu” Daktari Dau anasistiza

No comments :

Post a Comment