Tuesday, September 24, 2013

wanachama, wadau mifuko ya hifadhi ya jamii


http://pamelamollel.files.wordpress.com/2012/10/ppf_day3-2-1.jpg

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio, akitoa hotuba wakati wa kufunga mkutano wa 22 wa wanachama na wadau wa Mfuko huo kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa AICC mjini Arusha.
 
Njia mojawapo ya wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni kufuatilia na kujua utendaji wa mifuko hii inayosimamiwa na bodi za wadhamini kwa njia ya mikutano mikuu inayofanyika kila mwaka. Ambapo wadau kama vile wanachama ambao ndio wachangiaji na waaajiri ambao mara nyingi ndio waliodhaminiwa au wakala wa kuhakikisha ya kuwa wanashirikiana na mifuko hii kama vile kusimamia ukataji na kupeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi na kuhakikisha ya kuwa wanatunza kumbukumbu za wafanyakazi wao, pamoja na wawakilishi kutoka katika vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini na baadhi ya taasisi za serikali na zisizo za kiserikali. Kwa kawaida hii inakuwa nafasi ya kipekee na muhimu sana kwa wadau kama wanachama wa  mifuko hii ya hifadhi ya jamii kuhudhuria kwa ajili ya kuzungumzia mambo muhimu yanayogusa  afya na ustawi wa mifuko zinazohusiana na taarifa za hesabu, taarifa za ukaguzi wa mahesabu, zinazohusiana na taarifa za bodi ya wadhamini wa mifuko na kujua nafasi na uwezo wa mfuko kifedha.
Lakini pamoja na hayo wadau wanakuwa na haki ya kujua maamuzi muhimu yaliyoamuliwa kwa mfano na mkutano wa mwaka jana ambayo yalipewa kipa umbele pamoja na yatokanayo ambapo tumeona mara nyingi wadau kama mwanachama inakuwa nafasi nadra sana kwao kama wachangiaji au mwana hisa kuitumia vizuri.

Kwa mfano mfuko wa pensheni wa PPF unategemea kuwa na mkutano wa 23 wa wanachama wa mfuko na wadau mbalimbali wa sekta ya hifadhi ya jamii utakao anza tarehe 2-4 Oktoba 2013. Wanachama na wadau wakiwa kama vile Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi, Maofisa Watendaji Wakuu (CEO), Maofisa wanaoshughulika na Raslimali Watu na Utawala, Sheria, Uhasibu, Fedha, Teknolojia na Mawasiliano na Bima, kutoka Serikali Kuu na Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma, Makampuni binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Wawakilishi wa Vyama vya Wafanyakazi kutoka sehemu za kazi, vyama vya waajiri na watu wengine wowote watakaopenda kushiriki kwa lengo la kujua na kupata elimu ya masuala ya hifadhi ya jamii. Mkutano huu utafanyika Arusha katika ukumbi wa Simba, AICC – Arusha ukiwa na mada kuu ya 'PPF na Wadau; Miaka 35 ya Kukua Pamoja'.

Hivyo basi hima kwa wanachama na wadau kuhakikisha ya kuwa mnaitumia nafasi ya nadra inayotokea mara moja kwa kila mwaka kwa kuchambua ustawi na afya ya mfuko wenu huu wa PPF ili kuondoa dukuduku zenu na kuboresha utendaji wa mfuko. Kuwawezesha wanachama na wadau kutekeleza haki, wajibu na nguvu walizopewa katika mkutano mkuu wa mwaka kama huu wanatakiwa kuandaliwa mapema kwa muda muafaka na kupewa habari bora na za hali ya juu   na isipofanyika hivyo basi uwezo wa nguvu wa kisheria waliopewa unakuwa hauna nguvu yeyote kwa wanachama, waajiri na hata kwa wadau wengine. Ni wajibu wa bodi ya wadhamini ya PPF kuhakikisha ya kuwa taarifa za kuwapasha wadau zinawafikia wadau wa mfuko huu juu ya kufanyika mkutano mkuu wa mwaka kwa muda muda muafaka na siyo vinginevyo. Maswali ya kujiuliza ni kama vile taarifa au habari hizo zinazotolewa na PPF zina ubora gani na je zimewafikia wadau wanaohusika kwa muda muafaka?

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa 22 wa wanachama na wadau wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, wakifuatilia mkutano huo kwenye siku ya ufungaji uliodumu kwa siku tatu kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa AICC mjini Arusha
Na kwa upande mwingine mtu anaweza kujiuliza ya kwamba chukulia ya kuwa mwanachama amepelekewa habari na kupata taarifa mapema juu ya kuhudhuria mkutano mkuu wa 23 wa wanachama na wadau wa PPF. Je baada ya hapo inafuatiliwa ili kuhakikisha ya kuwa hawa wanachama na wadau watakaochaguliwa kuwawakilisha wenzao kwenye mkutano huo watawajibika kama inavyotakiwa. Hivyo kwa upande mwingine unaweza kusema ya kuwa wadau kupatiwa taarifa na bora kwa muda muda muafaka hiyo haitoshi kabisa  kinachotakiwa hapa ni kwa hali na mali mdau kuwa tayari kujua au kuelewa kilichoandaliwa kwenye makabrasha ambalo ni jambo linaloonekana kuwa ni tatizo kubwa kwa wanachama na wadau wengi wa mifuko ya hifadhi ya jamii 
Mtu mwingine anaweza kuwa na mashaka na kilichopo ndani ya makabrasha kama siyo pambo tu la kuvutia mfuko wa pensheni kwa idadi kubwa ya wadau na wanachama. Kwa upande mwingine wanachama mara nyingi wameonekana kuwa ni kundi ambalo halina nguvu kabisa kwa kusimamia utendaji na uendeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo kufuatilia tabia na utaratibu wa utendaji wa wadhamini au bodi hizi za hifadhi ya jamii  na hata inaonekana wanatofautiana katika mitazamo kwa upande mwingine
Hapa ikumbuka kwamba uhai na ustawi wa mifuko ya hifadhi ya jamii siyo kweli ya kwamba inategemewa na mikutano mikuu ya mwaka ya mifuko kama huu utakaofanyika wiki ijayo huko arusha na PPF ingawa ni mojawapo ya mlango muhimu wa ufahamu kama mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii. Wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii wametawanyika karibu mikoa yote ya Tanzania kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji, wilaya, kimkoa na hadi kitaifa hivyo kwa maana hii inalazimisha kuwepo na uwakilishi katika kuhudhuria kwenye mikutano mikuu hii ya mwaka.
Kutokana na msambaratiko huu wa wanachama au wadau na hatimaye kuwakilishwa na watu wachache kutoka kila kampuni za umma na  za watu binafsi, na taasisi mbalimbali kwa hiyo hata mahudhuria ya wadau na wanachama kwenye mkutano mkuu wa mwaka umekuwa wa matatizo kwa kuhudhuriwa na wanachama na wadau wachache wawakilishi. Kwa sababu hii imesababisa mpaka kuwepo na uwakilishi katika mkutano mkuu ya kila mwaka badala ya wanachama kuhudhuria. Jambo la kujiuliza ni kwamba je hawa wawakilishi kutoka kwa waajiri mbalimbali wanakutana na wafanyakazi wenzao  au kama ni mwajiri je naye anahakikishaje kutoa taarifa kwa ukamilifu na ubora ule ule uliotolewa wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama au wadau wa mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii kama PPF.

Kwa kifupi ni kwamba je wanachama hupewa taarifa na wawakilishi mara tu baada ya kutoka kwenye mahudhurio ya mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa mfuko? Na kama hawapewi kunakuwepo na maana gani ya kuwa na mwakilishi? Hivyo kuna haja ya kuwa  na malengo na mikakati ya makusudi ya kuhakikisha ya kuwa waajiri, wafanyakazi, na taasisi mbalimbali kuchagua mwakilishi ambaye atakuwa ni mtu ambaye atashiriki kwa malengo ya kuelewa na kujua mambo muhimu ya mkutano mkuu hasa yanayogusa uhai, afya na ustawi wa mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii kwa malengo ya kuboresha kinga ya wanachama wake wachangiaji wakati wanapofanya kazi na baada ya kustaaafu na siyo vinginevyo
Wawakilishi wa wanachama na wadau mbalimbali wa PPF tumieni fursa hii ya kuwa na utahitaji wa kujifunza zaidi utendaji wa mifuko ya pensheni kutoka kwa wataalamu wa PPF na mamlaka inayohusika kama vile mdhibiti na msimamizi wa mifuko ya pensheni ya  hifadhi ya jamii (SSRA) wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wanachama wa PPF


Manejimenti ya PPF ikumbuke kuwa kuendesha na kusimamia mfuko wa hifadhi ya jamii kama vile kuwa na mkutano mkuu wa mwaka wa wadau haukuanza jana mfuko huu una uzoefu wa muda mrefu tangia miaka 23 iliyopita kuendesha mikutano kama hii hivyo ni mfuko wa kwanza wa pensheni ya hifadhi ya jamii kuanzisha wa mfumo huu kuwashirikisha wanachama na wadau wa hifadhi ya jamii. 

Hiki ni kipengele mojawapo muhimu cha kuzingatia utaratibu na kanuni za utawala bora hivyo tunaamini ya kuwa PPF utaendelea kujenga imani zaidi wakati wa mkutano mkuu kwa wanachama na wadau kwa kuwahakikishia ya kuwa mfuko unaendeshwa na kuongozwa na utawala bora na kwa ufanisi wa hali ya juu zaidi kwa kuendesha mkutano kwa njia ya ukweli na uwazi

Kuna haja ya uongozi wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa wazi kama kigezo muhimu cha utawala bora kuthibitisha pale uamuzi unapofanywa kwa kuzingatia masilahi ya mfuko kwanza na siyo masilahi binafsi ya viongozi. Uwazi ni matokeo ya mchakato na utaratibu wa uamuzi wa wazi wenye kuzingatia vigezo maalumu vinavyotumika katika kufanya maamuzi ya kuchagua wajenzi, makandarasi, kusaini mikataba, na viongozi kutoa taarifa nyeti zinazowasaidia kuboresha shughuli za mfuko na kufanya kuwa endelevu kwa wanachama wachangiaji na wadau wengine kwa njia mbalimbali kama vile kupitia magazeti, tovuti, televisheni, redio na mitandao ya kijamii. 

Nafikiri mmeshuhudia hata baadhi ya taasisi na makampuni makubwa ya kimataifa kufilisika na kuanguka na mara nyingi makampuni haya yamekuwa yakitoa taarifa za uongo za matumizi ya fedha na za kiutendaji, na wizi uliokithiri, malipo na marupurupu yasiyo ya kawaida kwa viongozi, mifumo ya ndani dhaifu ya udhibiti wa fedha, kushidwa kudhibiti hatari na majanga, mawasiliano duni kati viongozi na wanachama na uendeshaji mbaya unaosababisha wanahisa kupoteza mitaji yao na kupata hasara. Mara nyingi wanachama wamekuwa wakijiuliza kuwa imekuwaje viongozi hawakujua kuwa kuna hatari ya kufilisika?
Tunaamini ya kuwa mfuko huu wa PPF unazingatia kanuni za uongozi bora na kwa kufanya ndiyo maana hivyo kumekuwa na uwezekano mkubwa kwa mfuko kuwa na utendaji mzuri unaofikia malengo na kukidhi matarajio ya wanachama wake na familia zao.

PPF hivyo tumieni  nafasi hii ya mkutano mkuu wa wadau kwa kuhamasisha  kuanza kupanua wigo zaidi wa hifadhi ya jamii kwa kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wanachama, wadau na kwa umma wa Tanzania kwa ujumla kwa njia ya kujenga ushirikiano kati ya wadau ili kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii nchin
i.
Hivyo mkutano huu mkuu unategemewa kufanywa kwa ushirikiano mkubwa kati ya wanachama, wadau na mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii SSRA na mifuko mengine ya hifadhi ya jamii, shirika la kazi duniani (ILO), Hazina, Wizara ya kazi na ajira, wakala wa huduma za ajira Tanzania (TAESA), shirika la tija la taifa (NIP) na idara ya ajira pamoja na  Baraza la ushululisho na uamuzi (CMA) 
 
Hivyo tunagemea PPF kama mfuko wa pensheni ya hifadhi ya jamii kutumia vyombo vya habari kwa ajili ya kuwahabarisha hata kwa wale wanachama, wadau na wananchi wengine ambao idadi yao kubwa hawatapata nafasi ya kuhudhuria mkutano mkuu wa mwaka kuhamasishwa kwa njia ya programu za redio, runinga na machapisho mbalimbali kama vile magazeti, vipeperushi n,k, wakiwa majumbani mwao safarini Tanzania nzima na nchi za nje. Watanzania wengine tumieni fursa hii ya wiki ya mkutano mkuu kwa wanachama na wadau nchini kujifunza na kujielemisha juu ya uhai, utendaji,  afya na ustawi  wa mfuko wa pensheni wa taifa (PPF) juu ya taarifa zinazohusiana na hesabu, taarifa za ukaguzi wa mahesabu, na taarifa za bodi ya wadhamini wa mifuko na kujua nafasi na uwezo wa mfuko kifedha kwa njia ya magazeti, redio, luninga, blog na njia zingine za mitandao kwani pensheni ni haki yako



No comments :

Post a Comment