Friday, September 13, 2013

JK katika mtihani wa Katiba Mpya

Rais Jakaya Kikwete akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Kijiji cha Katunguru/Nyamtelela wilayani Sengerema, mkoani Mwanza juzi. Kulia ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe. Picha na Ikulu  
Na Fidelis Butahe na Mwinyi Sadallah

Posted  Ijumaa,Septemba13  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
  • Wasomi, wanasiasa wamsihi asikubali kusaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Katiba, Profesa Lipumba asema akisaini itakuwa majanga

Dar na Zanzibar. Wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa asaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 ili kuwa sheria kamili, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamemshauri asifanye hivyo, wakisema itapatikana Katiba Mpya isiyo na tija.

Wananchi hao kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walisema kwa nyakati tofauti kuwa, Rais Kikwete anatakiwa kutumia busara ya kushauriana na kupata maoni ya watu wa kada mbalimbali ili kujua nini kifanyike, kabla ya kuamua kusaini muswada huo.

Mjadala wa muswada huo uliopitishwa Ijumaa iliyopita na wabunge wengi wakiwa wa CCM, ulizua tafrani bungeni iliyosababisha Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) kutolewa nje na askari. Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.

Wapinzani walisema Serikali iliubadili kwa nguvu muswada huo kwa kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia walilalamikia kitendo cha wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge kutokwenda Zanzibar kuchukua maoni ya upande huo wa muungano.
Wasomi

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Gaudence Mpangala alisema mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ulikuwa ukienda vizuri... “Lakini umebadilika vibaya, tena katika kipindi muhimu. Kupitishwa kwa muswada na kusubiri saini ya Rais kunaweza kuleta Katiba Mpya, ikawa siyo ile ambayo Watanzania wanaitarajia.” Alishauri busara itumike kabla ya kusainiwa kuwa sheria kamili.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tunguu Zanzibar, Ali Uki alisema hakuna haja ya muswada kukimbiliwa kusainiwa kwani katiba ni mali ya wananchi na kuupitisha ili uwe sheria bila kuyashirikisha makundi mengine, kutaendeleza malalamiko na kurudisha nyuma malengo ya kupatikana kwake. Uki alisema upo wasiwasi kwamba Katiba Mpya itatokana na utashi wa kisiasa badala ya matakwa ya wananchi, jambo ambalo alisema linaweza kuathiri malengo ya kuandikwa kwake.

“Utashi wa vyama umeanza kujitokeza, huku chama kimoja kikiwa na uwakilishi mkubwa kwenye Bunge hilo, chama kimoja kina uwakilishi wa asilimia 72 katika Bunge la Katiba,” alisema Uki.

Alikosoa Kifungu cha 8 na Kifungu kidogo cha 4 na 5 cha muswada huo kwamba vina kasoro kwa kuruhusu wabunge wa Bunge la Katiba kufanya uamuzi kwa wingi wa kura badala ya kutumika utaratibu wa theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.

Profesa mwingine wa UDSM, Chris Peter Maina alisema ikiwa kuna nia njema ya kupata Katiba bora, lazima suala la uwiano wa idadi ya wabunge katika Bunge la Katiba litazamwe upya.

“Rasimu ya pili ikishatolewa na kukabidhiwa kwa Bunge la Katiba, kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndiyo itakuwa imekwisha. Sasa inakuwaje Bunge linajadili Rasimu ya Katiba huku waliyoiandaa hawapo, hiki kitu kinashangaza,” alisema Profesa Maina.
Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk Frank Tilly alisema hakuna umuhimu wa kukimbiza muswada kutiwa saini wakati kuna mambo mengi ya msingi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi... “Watanzania hawajakubaliana kwa pamoja, ili jambo liwe zuri ni lazima pande mbili au zaidi zenye masilahi na kitu husika zikubaliane, sasa hilo halijafanyika tunakimbilia wapi?” alihoji.

No comments :

Post a Comment