Na Faustine Felician
Kwa ufupi
- Haiwezekani mbunge akakaa mjini na kushindwa kwenda kuwatembelea watu wake jimboni.
Busega. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta amesema baadhi ya wabunge wa CCM ni mizigo kwani
hata wakienda bungeni, hawachangii na wanabebwa na chama.
Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, alisema hayo juzi jioni kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Busega Mkoa wa Simiyu ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuimarisha uhai wa chama.
“Ukweli ni kwamba, baadhi ya wabunge wa jinsi hii hawatufai. Wanakwenda bungeni hawachangii, wanakwenda bungeni hawana hata hoja za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo,” alisema Sitta.
Sitta alisema licha ya aina hiyo ya wabunge, pia wapo wale ambao hawafiki majimboni kwao kukagua shughuli za maendeleo.
“Wapo baadhi ya wabunge, hawajawahi hata siku moja kwenda kwenye majimbo yao kuwatembelea wananchi waliowachagua... inawezekana hata wapiga kura wakawa wamewasahau. Hawa hawafai hata kuchaguliwa wakiomba tena kura,” alisema na kuongeza:
“Haiwezekani mbunge akakaa mjini na kushindwa kwenda kuwatembelea watu wake jimboni. Mbunge anakwenda jimboni kwa kuchungulia halafu wananchi wanamshabikia na kumpa kura?
“Rais Jakaya Kikwete amejitahidi sana kuleta mabadiliko, ameleta mafanikio ya uchumi na mambo mengi. Inatakiwa wabunge waende wakawaeleze wananchi maendeleo haya, inawezekana hawayajui lakini watu hawaendi majimboni, wananchi watayafahamu vipi haya maendeleo?”
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya, Sitta alisema: “Kwanza kuna viashiria vya baadhi ya watu kuanza kuipinga Katiba mahakamani. Watu hao wasiungwe mkono kwani ndio wanaoanza chokochoko.
“Katiba tunayoitaka ni kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania na Watanzania na si ya wengine. Hivyo hatuna budi kila mmoja kutumia nafasi hiyo kuwasilisha mchango wake wa kuboresha kwenye Mabaraza ya Katiba.”
Aliwataka wajumbe wa Mabaraza ya Katiba watumie nafasi kuwasilisha hoja zinazojenga na wasiwe mamluki wa kuharibu mchakato mzima.
Awali, Sitta alishiriki katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki la Kiloleli, Wilaya ya Busega na kuchangia Sh3 milioni.
Akizungumza katika harambee hiyo, iliyotarajiwa kukusanya Sh217,538,000, Sitta aliwataka wazazi kuwalea watoto wao katika misingi ya dini ambayo baadaye hutoa viongozi bora na wenye maadili... “Huwezi kuchukua tu mtu awe kiongozi, lazima wafunzwe misingi ya maisha na uongozi.”
No comments :
Post a Comment