Na Mwandishi Wetu
Kwa ufupi
Atahadharisha nchi za Afrika kutotegemea fedha za kuendesha majadiliano kutoka Ulaya.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Mubalozi wa Afrika
nchini Ubelgiji, Dk Diodorus Kamala, amesema majadiliano ya biashara
kati ya nchi za Afrika na Jumuiya ya Ulaya (EPA), yameshindwa kuzingatia
misingi mikuu na mkataba wa Cotonou wa mwaka 2000.
Akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa majadiliano ya EPA Libreville, Gabon jana, Dk Kamala alisema mkataba wa Cotonou uliweka misingi ya majadiliano ya EPA, ambayo ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda wa nchi za ACP.
Pia, alisema yalitaka kuzingatia mahitaji ya maendeleo ya nchi za ACP, kuongeza kazi ya maendeleo ya nchi hizo na kuimarisha ushirikiano wa uchumi na biashara kwa manufaa ya wote. “Inasikitisha majadiliano ya EPA yanayoendelea hivi sasa kushindwa kabisa kuzingatia misingi muhimu iliyowekwa na nchi za ACP na Jumuiya ya Ulaya (EU),” alisema.
Kuhusu kuimarisha ukanda, Dk Kamala ambaye pia ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, alisema nchi za Mauritius, Ushelisheli na Zimbabwe zimeweka saini mikataba ya EPA na kuridhia, hivyo kudhoofisha ushirikiano wa kikanda maeneo yao.
Alisema Ghana na Ivory Coast zimesaini mikataba ya EPA kama nchi na kudhoofisha utangamano wa Ecowas.
“Nchi za Afrika Mashariki zisipokuwa makini zitajikuta zikisaini mkataba wa EPA kama nchi, hivyo kudhoofisha utangamano wa Afrika Mashariki,” alisema Dk Kamala.
Alisema nchi za Ulaya hazionekani kuwa tayari kuendelea kushirikiana na nchi za ACP kwa maendeleo kama ilivyo mkataba wa Cotonou na kwamba, bajeti ya miaka saba ya EU kuanzia mwaka 2014 hadi 2020 haijatenga fedha yoyote kusaidia nchi hizo kukabiliana na makali ya utekelezaji mikataba ya EPA.
“Mikataba ya EPA inaziweka nchi za ACP katika njia ya magari yaendayo kwa mwendo wa konokono. Afrika lazima twende kwenye njia ya magari yaendayo kasi ili tuweze kufika,” alisema.
Alisema nchi za Ulaya hazitaki kuacha kutoa ruzuku kwa wakulima na wafugaji wao, hivyo kukosesha soko mazao ya kilimo kutoka nchi za ACP.
“Nchi za Ulaya zinataka kuzifunga mikono nchi za ACP kwa uhuru wa kuchagua marafiki na nchi za kufanya nazo biashara (Most Favoured Nation Clause). Tusikubali jambo hili,” alisema Dk Kamala na kuongeza:
“Nchi za Ulaya zinataka kuziondolea uhuru wa
kutoza kodi kwenye bidhaa zinazouzwa nje ya ACP. Kodi hii hutumiwa na
nchi kulinda viwanda vichanga na kuzuia kuuza malighafi.”
No comments :
Post a Comment