Thursday, April 25, 2013

Ripoti ya CAG imeivua nguo Serikali

 
Kwa ufupi
Kama tulivyosema hapo juu, Serikali haionekani kufurahia utaratibu uliowekwa kwa shinikizo la wafadhili la kuweka wazi  ripoti hizi za CAG. Ndiyo maana imeushinikiza Uongozi wa Bunge kufuta utaratibu uliokuwapo wa Bunge kujadili ripoti hizo moja kwa moja na kuiwajibisha Serikali.

Moja ya mafanikio ambayo yametokana na ripoti za kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ni wananchi kutambua kwamba mhujumu mkuu wa uchumi wa nchi yetu siyo mwingine bali ni Serikali. Pamoja na Serikali kubuni mbinu mbalimbali ili wananchi wasizijadili kwa undani na kuweza kutambua chanzo cha kukwama kwa uchumi wa nchi yao, vyombo vya habari vimehakikisha mambo muhimu yaliyo katika ripoti hizo yanawafikia wananchi.

Hivyo, miezi miwili au mitatu hivi ijayo vyombo vya habari makini vitaendeleza utamaduni huo wa uwajibikaji kwa wananchi kwa kuhakikisha wananchi wanafahamu mambo muhimu yaliyomo katika Ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha uliopita. Ripoti hiyo iliwekwa wazi na CAG, Ludovick Utouh alipokutana na waandishi wa habari mjini Dodoma juzi, ambapo ilianika ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma na udhaifu katika usimamizi wa mikataba na ukusanyaji kodi.

Kama ilivyokuwa huko nyuma, ambapo ripoti hizo ziliwawezesha wananchi kupata mwamko wa jinsi Serikali na taasisi zake zinavyodumaza uchumi kwa vitendo vya ubadhirifu na ufujaji wa fedha za umma, Ripoti ya CAG iliyozinduliwa katikati ya wiki itawapa tena fursa ya kushuhudia kujirudia kwa vitendo hivyo ndani ya Serikali na taasisi zake.

Kama tulivyosema hapo juu, Serikali haionekani kufurahia utaratibu uliowekwa kwa shinikizo la wafadhili la kuweka wazi  ripoti hizi za CAG. Ndiyo maana imeushinikiza Uongozi wa Bunge kufuta utaratibu uliokuwapo wa Bunge kujadili ripoti hizo moja kwa moja na kuiwajibisha Serikali.

Jambo ambalo wananchi watajifunza baada ya kujua kilichomo katika Ripoti ya CAG iliyozinduliwa katikati ya wiki ni ukweli kwamba kimsingi Serikali haijakubali kubadilika na kufuata njia nyoofu ya uadilifu na uwajibikaji.

Bado watumishi wake katika ngazi za juu wanafuja fedha mithili ya mabaharia walevi na imekataa katakata kuzingatia ushauri ambao CAG alikuwa akitoa kupitia ripoti zake za kila mwaka.

Kwa mfano, CAG amegundua kwamba Serikali imepuuza kabisa ushauri wake wa kuitaka ipunguze misamaha ya kodi isiyo ya lazima. Ripoti ya sasa inasema misamaha hiyo bada

Ni ushahidi kwamba baadhi ya viongozi serikalini wanafaidika na misamaha hiyo. Ebu fikiria mantiki ya Serikali kusamehe makampuni ya madini Sh140 bilioni au sababu za kusamehe kampuni na watu binafsi kodi ya Sh304 bilioni.

CAG alipendekeza wabunge wasiwe wajumbe wa bodi za mashirika ya umma, lakini idadi yao katika mashirika hayo ndiyo kwanza inazidi kuongezeka. Wakiwa katika bodi hizo hawawezi kuyasimamia mashirika yake ipasavyo kwa sababu ya wao  kuwa na masilahi binafsi. Kwa mfano, Ripoti ya sasa ya CAG imegundua kwamba Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali Kuu (PSPF) umepata hasara ya Sh6.487 trilioni.

Kwa mshangao wa CAG, Uongozi wa Bunge pengine kwa shinikizo la Serikali umevunja Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na kuunganisha shughuli zake na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC).
CAG ameonya, na tunafikiri yuko sahihi kwamba PAC itazidiwa na haitaweza kumudu majukumu ya kusimamia mashirika ya umma zaidi ya 300, wizara zote na taasisi zake.

No comments :

Post a Comment