Monday, April 15, 2013

Kanuni zinazohusika na Biashara ya Filamu


Baadhi ya wasanii wa filamu Tanzania
 A.UTANGULIZI
 
Tasnia ya filamu, kama ilivyo muziki wa kizazi kipya, ni miongoni mwa fani zilizofanya mapinduzi makubwa katika miaka ya hivi karibuni hapa nchini. 
 
Pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili tasnia hii, biashara ya utengenezaji,usambazaji na uoneshaji wa picha jongevu (filamu ama sinema kama wengi tulivyozoea) imezidi kukua kwa kasi sambamba na fursa za ajira kwa mamia ya vijana, ongezeko la vipato kwa wahusika, mapato kwa serikali na faida nyinginezo.
 
B. CHANGAMOTO KATIKA TASNIA YA FILAMU
Kama tulivyodokeza hapo juu, taaluma ama biashara hii ya filamu Tanzania imenufaisha wengi lakini wakati huo huo kumekuwepo na matatizo lukuki ambayo yamelazimisha uhitaji wa mabadiliko ya lazima katika sera, sheria, taratibu na miundo-mbinu ya kitaasisi inayohusiana na tasnia hii. 
 
Mathalani, baadhi ya changamoto zilizo dhahiri ni kuendelea kuwepo kwa mitizamo hasi miongoni mwa Watanzania walio wengi kuwa wasanii wa hapa nyumbani hawana ubunifu, umahiri na uwezo wa kuburudisha ipasavyo kama wenzao wa Hollywood (Marekani), Bollywood (India) ama Nollywood (Nigeria) na  kwingineko ama soko la filamu ni kubwa zaidi na la siku nyingi.
 
Matatizo mengine yanayoikabili tasnia ya filamu nchini na ambayo hayajapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu ni uwepo wa mikataba mibovu baina ya wasanii kwa upande mmoja na waandaaji, watengenezaji ama wasambazaji kwa upande mwingine, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kwa wasanii walio wengi kuendelea kuishi maisha ya kubahatisha huku wakiwatajirisha wenzao wachache kupitia migongo ya juhudi na umaarufu wao katiki skrini.
 
Mwiba mwingine katika kuongeza maumivu ya soko lisilodhibitiwa na unakilishaji usioidhinishwa na wizi unaoendelea kufanywa waziwazi kwa kazi za sanaa za filamu na muziki hapa nchini. 
 
Zaidi ya hayo, hakujafanyika juhudi madhubuti kupitia serikali, asasi zisizo za kiserikali, taasisi binafsi na hata miongoni mwa wasanii wenyewe kuweka msimamo wa dhati katika uboreshaji wa bajeti, teknolojia na uhamasishaji katika kile wanachokifanya, kwa faida yao na taifa zima.
 
SHERIA, KANUNI NA TAASISI ZINAZOHUSIKA NA FILAMU
Baada ya kutambulisha maendeleo yaliyojiri, fursa zilizopo na changamoto zinaoikabili tasnia ya filamu nchini, turejee sasa katika mada iliyokudiwa kuwasilishwa hapa leo-kuuelimisha umma na kuwakukumbusha wahusika wa tasnia ya filamu kuhusiana na sheria na taratibu muhimu zilizopo na zinazopaswa kuzingatiwa katika masuala ya leseni, utengenezaji, usambazaji ama uonyeshaji wa picha jongevu (filamu na sinema).
 
Kanuni Kuu na zilizo muhimu zaidi zinazohusika na Tasnia ya Filamu Tanzania zinatambulika kisheria kama ‘Kanuni za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza za Mwaka 2011’. Kanuni hizi zimeandaliwa na kuchapishwa kupitia Tangazo la Serikali Namba 156 la mwaka 2011. 
 
Muhimu kuzingatia ni kwamba Kanuni za zilizopo za filamu ziliandaliwa na kuchapishwa na Waziri mwenye Mamlaka ya kusimamia Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza (Sura ya 230 ya Sheria za Nchi), Toleo la mwaka 2002).
 
Katika hili ni vema pia kwa msanii na yeyote yule anayehusika na biashara ya filamu nchini kutofikiria kuwa Kanuni hizi (tangazo namba 156 la mwaka 2011) ndizo pekee zinazoongoza tasnia hii. 
 
Mathalani, Chini ya Sheria hii ya Filamu na Michezo ya Kuigiza (hujulikama kimombo kama Films and Stage Plays Act) kumetolewa Kanuni mbalimbali tangu sheria hii ilipotungwa na Bunge mwaka 1976 na ni jukumu basi la mhusika mwenyewe kufuatilia ili kuelewa ni kanuni zipi zinaendelea kutumika na kwa mambo gani anayohusika nayo.
 
Uelewa wa mambo haya ni muhimu kwa sa sababu utakufanya wewe msanii ama unayehusika na biashara hii kufanya maamuzi kwa kujiamini katika kusimamia maslahi yako na pia kuelewa wajibu wako kwa mujibu wa Sheria za nchi.
 
Kwa mfano, zaidi ya Tangazo namba 156 la mwaka 2011, kumekuwepo pia na Kanuni nyingine chini ya Sheria hii ambazo zimechapishwa kupitia Matangazo ya Serikali namba 435 la mwaka 1995, 315 la mwaka 1999 na Tangazo la Serikali namba 73 la mwaka 2004.
 
Tukirejea katika Kanuni za Filamu na Michezo ya kuigiza ya mwaka 2011, baadhi ya mambo muhimu yaliyomo humo ni matumizi ya maneno ya Kisheria. Chini ya Sheria hii neno muhimu sana kulifahamu ni ‘Picha Jongevu’.
 
Msamiati huu si maarufu sana mitaani lakini chini ya Sheria hii una maana ya ‘mpangilio wa picha zinazoonekana na zilizorekodiwa katika kifaa chochote kwa mfumo wa digitali, seluloidi au kwa namna yoyote ambayo picha hiyo inaweza kujongea na inajumuisha picha zilizoko katika filamu, video, katuni na picha zinazofanana na hizo’. 
 
Ndiyo kusema basi picha, sauti na mitiririko iliyomo katika filamu zilizozoeleka za akina hayati Kanumba, Wema Sepetu na nyinginezo ni ‘picha jongevu’ na ambazo uandaaji, utengenezwaji, usambazaji, uuzwaji na uonyeshwaji wake ulipaswa ama unapaswa kuzingatia kanuni tunazozifafanua hapa.
 
Jambo jingine muhimu ni kuhusiana na eneo la Kijiografia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo Sheria hii inahusika. Kanuni namba 2 iko wazi kabisa kwamba Sheria hii hutumika Tanzania Bara tu. 
 
Hivyo, basi, mtengenezaji wa filamu ama ‘picha jongevu’ aliyeko Tanzania Bara na ambaye anataka kurekodi akiwa Tanzania Visiwani (Zanzibar ama Pemba) tukio fulani ndani ya filamu hiyo atapaswa kuzifahamu Sheria zinazohusiana na filamu zinazotumika huko ili kwamba asije akafanya jambo ambalo ni halali chini ya Sheria za Bara lakini likawa ni haramu chini ya Sheria za Zanzibar kwa sababu, kama tulivyoona, iwapo anashtakiwa huko, haitarajiwi kwamba atatumia Kanuni hizi kujitetea huko.
 
Ukweli huu ni ule ule kwa Msanii kutoka Zanzibara anayekusudia kufanya hivyo Tanzania Bara. Ni muhimu basi kwa wasanii na wafanyabiashara wa filamu nchini na hasa wanaofanya biashara pande zote za Muungano kuzifahamu vilivyo sheria zinazohukika kote.
 
Jambo la tatu muhimu kulielewa ni taasisi zilizopewa dhamana katika masuala mbalimbali ambayo msanii ama mfanyabiashara wa filamu anapaswa kuzifahamu kwa sababu aghalabu atapaswa kufika katika ofisi husika ama kufanya mawasiliano nazo katiika masuala muhimu kama utoaji wa leseni na vibali, kupata miongozo, uwasilishaji malalamiko, utatuzi wa migogoro, ukataji wa rufaa na kadhalika. Chini ya Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 1976 na Kanuni zake za mwaka 2011 taasisi muhimu zaidi ni pamoja na Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza;
 
Bodi Kuu ya Ukaguzi wa Filamu  na Michezo ya Kuigiza na Waziri mwenye dhamana ya mambo yanayohusiana na Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza.
 
Kwa utaratibu wa sasa. Waziri anayehusika na mambo haya ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa mujibu wa Tangazo la Serikali namba 494A la mwaka 2010 (Angalia Tangazo la Serikali liitwalo‘The Ministers (Discharge of Ministeria Functions), Notice, 2010 lililotolewa Chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Wajibu wa Mawaziri (Sura ya 299).
 
Taasisi, Asasi na Wadau wengine muhimu katika usimamizi na utekelezwaji wa Sheria na Kanuni za filamu ni pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (COSOTA),Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Utamaduni Tanzania, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo(TaSUBa), ZIFF (Zanzibar), Bodi ya Filamu Zanzibar, Ofisi ya Rais, Wizara za Serikali na kadhalika.
 
Kulingana na maelezo hapo juu ni mambo mawili yanweza kuzua maswali kuhusiana na Kanuni hizi.
 
Mosi, Kanuni namba 2 ya Kanuni za filamu inaainisha kuwa Kanuni hizi zitatumika Tanzania Bara tu lakini katika Jedwali la Tano lililotengenezwa kupitia Kanuni namba 51, Bodi ya Filamu Zanzibar  na ZIFF (Zanzibar) mi miongoni mwa  asasi 17 zilizotamulishwa kuwa zitashirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania. Hili linaweza lisilete mgongano kwa sababu linazungumzia ‘kushirikiana’.
 
Pili, inaweza kuzua swali kubwa kwamba hakuna asasi yoyoye ya vyombo vya habari iliyotajwa katika jedwali hili miongoni mwa asasi hizo za ushirikiano.
 
*Juma lijalo tutamalizia kwa kuangalia taratibu husika kama uombaji vibali, ada na masharti ya utengenezaj, uonyeshaji na usambazaji filamu Tanzania. 
 
Kumbuka kuwa maelezo haya ni ya ujumla tukulingana na ufinyu wa nafasi hii ukilinganisha na wingi wa kanuni husika na kwa kuzingatia kwamba maelezo haya lengo lake ni kutoa elimu ya msingi na si kuwa mbadala wa ushauri wa kitaalam wa kisheria, jambo ambalo ni la hatari na lisiloshauriwa kwa mhusika kulifanya kwa sababu uelewa wa sheria huhitaji elimu ya kina, uzoefu wa muda mrefu na umakini wa hali ya juu.
*Denis Maringo ni Mwanasheria aliyeko Dar es Salaam. dnmaring
 
 
 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment