Tuesday, February 5, 2013

Kwa nini michango ya pensheni isitumike kummilikisha nyumba mwanachama

Na Christian Gaya Majira 05 February 2013
Nyumba ina mchango mkubwa kwa upande wa uchumi, kijamii na kisiasa, na alama au muonyesho wa maendeleo na ustawi wa jamii katika nchi yeyote ile. Hivyo basi ni kitega uchumi ambacho kinachangia katika kupunguza kama siyo kuondoa umaskini kabisa, nyumba ni kitega uchumi ambacho kinachangia kuongezea ajira, kinaongezea mapato, kinaboresha afya na kuongeza ufanisi kwa nguvu kazi

Nyumba kwa mwenye nayo au anaye miliki ni rasilimali ambayo inawezekana kubadilishana na kitu chochote kwa vile kina thamani yake na ikatumika kwa vile ina thamani yake inayotambulika. Kijamii nyumba inachangia kuhamasisha na kuboresha nafsi ya mtu, utu, usalama na kutambuliwa mbele za watu. Kisiasa, nyumba bora inapunguza vitishia vya kisiasa vinavyotokana na kugandamizwa na kuchanganyikiwa hasa kwa watu wanaoishi kwa mazingira hatarishi na makazi yasiyokuwa rasmi

Kutokana na upeo wa michango au mafao ya pensheni, umilikaji wa nyumba ni sehemu ya upangaji mzuri wa jinsi ya kustaafu. Kumiliki nyumba wakati wa kustaafu inawalinda wastaafu kutokana na mahitaji ya mtiririko wa fedha mkononi-mahitaji ya mapato au fedha mkononi kwa ajili ya kuitumia kwa kulipia kodi ya nyumba inakuwa tayari imeshapungua.

Pamoja na hayo tena inawalinda wastaafu kutokana na maamuzi mabaya ya uwekezaji, na faida mbaya inayotokana na uwekezaji ikiwemo na mfumuko wa bei ambao hauendi na ukali wa maisha wa wakati huo. Vile vile inamwandaa mstaafu na maisha yenye heshima usoni mwa jamii na yenye utu mzuri wa hali ya maisha. Umilikaji wa nyumbani kwa kweli huchangia kiasi kikubwa kwa wastaafu kwa ajili ya kuwaandaa maisha ya ulimwengu wa kustaafu na katika kuwatengenezea staili ya miaka yao ya mwanzoni kabla hawajastaafu.

Kuna haja kubwa kabisa msimamizi na mdhibiti wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii yaani (SSRA) kubuni mikakati ya kuhamasisha uhitaji wa nyumba ili kuwezesha wanachama wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii kununua nyumba za gharama nafuu. Kwa mfano Singapore wanachama wa hifadhi ya jamii wanaruhusiwa kutumia asilimia 75 ya akiba yao ya michango ya pensheni kwa ajili kukopeshewa nyumba au kwa ajili ya kununulia nyumba maalumu anayohitaji.

Wakati Mauritius na Africa kusini mifuko ya pensheni ya hifadhi za jamii kama vile Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Pensheni kwa ajili ya Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Pensheni wa Hifadhi ya jamii kwa ajili ya Watumishi wa Umma (PSPF) na Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi wa Serikali (GEPF), Mfuko wa Bima wa Taifa yaani (NHIF), mfuko wa pensheni ya Hifadhi ya jamii kwa ajili ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa yaani (LAPF). Pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa Zanzibar (ZSSF) yanaruhusu kutoa mikopo moja kwa moja kwa wanachama na hata vilevile wanachama wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii kutumia sehemu ya theruthi mbili (2/3) ya mafao yao ya baadaye kama amana ya kumpatia mikopo benki na kupata mkopo wa nyumba kutoka taasisi za nyumba au mashirika ya nyumba ya nchi hizo kama vile Shirika la Nyumba la Taifa (THC) la Tanzania.

Na mafao yaliyosalia yanaachwa kama yalivyo bila kuguswa mpaka wanachama atakapofikia wakati wa kustaafu kwa hiyari au kwa lazima. Wanachama waliokopa wanalipa riba kwa muda wote na kuhurusiwa kuingilia mafao kulipa deni halisi alilokopa wakati utakapofika muda wake wa kawaida wa kustaafu. Kwa Afrika kusini viongozi wa hifadhi ya jamii wanapandisha mkopo wa nyumba kwa kutumia soko la mtaji kwa kutoa amana ya pensheni ili kumwezesha mwanachama wa hifadhi ya jamii kumiliki nyumba

Tanzania hairuhusu wanachama wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii kuingilia michango yao ya akiba ya pensheni kwa ajili amana ya kujipatia nyumba ya mkopo. Kwa maana hiyo kuna baadhi ya taasisi au mashirika ambayo yafanya kuwa siyo ya ushindani hasa pale yanapokuja na masharti magumu yanayofanya kwa mtu asisitahili kabisa kupata nyumba ya mkopo. Pamoja na hayo idadi kubwa ya wanachama wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii wanakopo kutoka katika taasisi hizo bado idadi kubwa ya wanachama mpaka sasa hawafikiwi. Wakati njia ya kutumia akiba ya michango ya pensheni ambayo huchangiwa na mwanachama na mwajiri wake ilikuwa ndiyo njia pekee ya mbadala ya kumwezesha mwanachama kupata mkopo wa nyumba. 

Katika kutambua umuhimu wa ungezeko wa uzalishaji nyumba kwa ajili ya kuhudumia watu wanaongezeka kila siku, serikali mara kwa mara  imekuwa ikiaangalia uwezekano wa kuwa na ufumbuzi  wa aina mbalimbali na hata vilevile kushawishi ushiriki wa sekta za watu binafsi ili kufikia lengo hili la nyumba. Uwezekano wa kupata mikopo ya fedha kwa waendelezaji na wanunuzi kumekuwa ni mojawapo ya sababu zilizochangia kuwa na uhaba wa nyumba.

Baada ya kutambua kwa thamani ya uchumi ya sekta hii muhimu ya pensheni ya hifadhi ya jamii iliyokuwa nayo mpaka sasa, mwaka 2008 serikali iliunda chombo cha kusimamia na kuthibiti mifumo hii ya hifadhi ya jamii. Muda umefika sasa kwa serikali kuchukua maamuzi ya makusudi ya kuchukulia sekta hii ya hifadhi ya jamii kama chombo ambacho  kinachoweza kuwa na mchango mkubwa wa kutoa mikopo kwa ajili sekta
ya nyumba

Chombo cha kusimamia na kuthibiti sekta ya pensheni ya hifadhi ya jamii yaani SSRA kimetoa miongozo ya uwekezaji pamoja na kuruhusiwa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii kujihusisha na uwekezaji wa rasilimali pamoja na nyumba/makazi mpaka kikomo cha asilimia 30% ya jumla ya fedha zote za mfuko. Na mifuko inaweza kujenga au kununua rasilimali isiyohamishika. Isipokuwa  michango au mafao ya pensheni haiwezi kutolewa kwa ajili ya kumwezesha mwanachama kupat mikopo ya nyumba au haiwezi kutumika kama amana ya kupata nyumba ya mkopo au dhamana ya kupata mkopo wa nyumba kwa ajili ya faida au manufaa ya mwanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii



No comments :

Post a Comment