Wednesday, January 2, 2013

Changamoto za hifadhi za jamii Tanzania




Na Christian Gaya: Majira 01 January 2012


Mfumo wa pensheni wa hifadhi ya jamii mpaka sasa una wanachama ambao wako chini ya milioni 45 ya watanzania wote. Ambapo idadi ya nguvu kazi ya watanzania wote inakisiwa kuwa ni milioni 20.94 kati ya hawa ni asilimia 6.5 ya nguvu kazi ndiyo wako chini ya mpango wa hifadhi ya jamii nchini. Na kila mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii uko chini ya wizara tofauti mfano Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lipo chini ya wizara ya kazi na maendeleo ya vijana, shirika la pensheni kwa ajili ya mashirika ya umma (PPF), Mfuko wa Pensheni wa hifadhi ya jamii kwa ajili ya Watumishi wa Umma (PSPF) na Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi wa Serikali (GEPF) yote mitatu ipo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Wakati Mfuko wa Bima wa Taifa yaani (NHIF) upo chini ya Wizara ya Afya na wakati huo huo mfuko wa pensheni ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya wafanyakazi wa serikali za mitaa yaani (LAPF) wenyewe upo chini ya wizara ya Serikali za Mitaa. Na kabla ya ya mwaka 2008 hayakuwa na chombo chochote cha  kusimamia na wala kudhibiti mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii kama yanavyosimamiwa na SSRA yaani msimamizi na mdhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mashaka na wasiwasi ulikuwa mwingi sana juu ya uendelefu wa mashirika haya ya hifadhi ya jamii hasa juu ya mgawanyo wa masoko kulingana na sheria tofauti zilizotungwa.

Hapakuwa na usawa wa mgawanyo wa soko huru wa wateja kama inavyoonyesha hapo juu mfano kila mfuko ulipangiwa sekta yake ya kuwahudumia  kisheria na hii ilifanya baadhi ya mifuko kuwa na wateja wachache na hivyo kupungua kwa mapato yatokanayo na michango ya wafanyakazi wachagiaji ya kuendeshea mifuko na kuweza kulipa mafao ya muda mfupi na ya muda mrefu.

Na kila mfuko wa hifadhi ya jamii unatoa mafao yake tofauti, na hata kama yanafanana kila moja ina taratibu na kanuni zake. Hivyo hayafuati utaratibu wa mafao kama yalivyoainishwa na shirika la kazi la dunia (ILO) chini ya kifungu cha 102 cha mwaka 1952. Ambapo imeanisha mafao yafuatayo: pensheni ya uzee, pensheni ya ulemavu, pensheni ya urithi, haya ni yakiwa kama mafao ya muda mrefu na mafao ya muda mfupi ni kama vile uzazi, bima ya afya, msaada wa mazishi, kuumia kazini na magonjwa yatokanayo na kazi, mafao ya uzazi, mafao ya wasiokuwa na kazi, na msaada wa kujikimu kwa wale wenye watoto chini ya umri wa miaka 18 kisheria.

Malipo ya mafao kwa wanachama hayaendi na mfumuko wa bei. Inakuwa nafuu kupata shilingi ya leo kuliko shilingi ya kesho. Kwa sababu kama ulitakiwa kupata mifuko ishirini ya saruji unapata mifuko kumi tu kwa sababu thamani ya fedha ambayo ndiyo mafao yako yanakuwa yameliwa na mfumuko wa bei wa wakati huo.



Hata riba inayotolewa na mifuko hii ni ndogo sana ukilinganisha na michango mwanachama anayochangia. Wakati huo huo michango ya mwanachama huo ndiyo inayowekezwa kwenye vitega uchumi mbalimbali kama vile kwenye hisa, vipande, na hatifungani. Na baadhi ya idadi kubwa ya michango huwekezwa kwenye miradi ya nyumba na makazi mbalimbali na faida inayopatikana ndiyo mwanachama hugawiwa kwenye akaunti ya kila mwanachama.

Na changamoto nyingine ni pale mifuko wanapokosa sehemu endelefu za uwekezaji hasa kwenye sehemu za muda mfupi na za muda mrefu kama vile kwenye majengo, hisa, vipande, na hatifungani

Kumekuweko na ongezeko kidogo sana la kuelewa juu ya mfumo wa hifadhi ya jamii hasa juu ya mafao yanayotolewa, jinsi ya kujiunga kuwa wanachama, vitega uchumi na shughuli mbalimbali za sekta.

Taasisi za hifadhi ya jamii ya jamii nchini Tanzania zimekuwa zikiwekeza orodha ya fedha kwa faida kwenye mikopo, nyumba za kupangisha, hatifunganishi, kuweka akiba benki zote hizi zimechangia maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.

Kumekuweko na ongezeko kidogo sana la kuelewa juu ya mfumo wa hifadhi ya jamii hasa juu ya mafao yanayotolewa, haki na wajibu wa mwanachama jinsi ya kujiunga kuwa wanachama, vitega uchumi na shughuli mbalimbali za sekta hii ya hifadhi jamii.
Sekta ya hifadhi ya jamii isiyo kuwa rasmi hasa kwa makundi ya kusaidiana yamekuwa yakijipanga vizuri zaidi kwa sasa ukilinganisha na hapo siku za nyuma.
 


Mapungufu yaliyomo kwenye mfumo huu wa hifadhi ya jamii ambayo yanahitajika kutatuliwa na sera hii ya hifadhi ya jamii yakisimamiwa na mdhitibi na msimamizi wa hifadhi ya jamii (SSRA). Idadi kubwa ya watu waliomo katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii ni wale tu ambao wameajiriwa kwenye sekta iliyo rasmi, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu kutoka katika sekta isiyokuwa kuwa rasmi inazidi kupungua kila siku kuwa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii badala ya kuongezeka.

Na hata wafanyakazi kutoka katika sekta isiyo rasmi wakiandikishwa kuwa wanachama wa mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii inakuwa ni vigumu sana hasa jinsi ya kuwapata, kuwaandikisha, kukusanya michango, jinsi ya kuwahamasisha na kuwaelemisha juu ya mafao yatolewayo na faida zake pamoja na haki na wajibu wa mwanachama. Na idadi kubwa ya watu ambao wako sekta rasmi hawana utamaduni wa kuweka akiba. 

Hata hivyo inaonyesha kuwa idadi kubwa ya mafao yanayotolewa na mifuko hii ya hifadhi ya jamii nchini 
Tanzania yako chini ya kiwango cha shirika la kazi la dunia (ILO) yaani kwa idadi ya mafao, ubora wa 
mafao, na kutokwenda na ukali wa maisha ya kila siku.

Hivyo mpaka sasa haya mashirika ya hifadhi ya jamii kila moja ina wizara yake inayoisimamia na kuwa utaratibu na kanuni tofauti za uendeshaji wa mifuko hii. Matokeo yake ni kwamba kiwango cha michango, mfumo wa mafao, na sifa za kupata mafao na hata mipango na vipa umbele vinatofautiana kabisa kwa kila mfuko.

Mpaka sasa hakuna utaratibu ulioanzishwa wa kuruhusu haki za mafao ya mwanachama kuhamishwa kutoka mfuko mmoja hadi mwingine. Matokeo yake wafanyakazi wamekuwa wakipoteza baadhi ya haki zao za mafao wakati wakihama kutoka sehemu moja ya mwajiri hadi mwajiri mwingine. Pia hii imechangia sana kuongezeka kwa tabia ya kuondoa michango ya pensheni kabla haijakomaa kiwango cha kuwa tayari kama mafao ya kustaafu. 

Huduma za wanachama zimekuwa haziridhishi kwa wateja. Mwanachama anaonekana kama siyo mfalme wa mifuko hii ya hifadhi ya jamii. Imekuwa ikichukua muda mrefu mwanachama kupata mafao yake. Mara nyingi malalamiko ya wanachama yamekuwa hayasikilizwi ipasavyo. Mafao yamekuwa yakilipwa pungufu. Na ushirikishwaji wa wanachama kama wabia wao kwenye mikakati, mipango na miradi umekuwa ukisua sua sana.  

No comments :

Post a Comment