Pages

Tuesday, May 29, 2012

Upinzani wahoji mabilioni ya NSSF yaliyokopeshwa Kiwira

17th July 2009
  Yasema inawekeza pasipo na tija

Kambi ya Upinzani bungeni, imehoji mkopo uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa Sh. Bilioni 8.4 kwa Kampuni ya Makaa ya Mawe na Nguvu ya Umeme – Kiwira utarudishwa lini, huku wanachama wanaostahili kulipwa mafao yao wakisaga soli za viatu kufuatilia.
Hoja hiyo ilitolewa na Msemaji wa Kambi hiyo, Salim Abdallah Khalfani, kwa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, wakati akichangia maoni ya Makadirio ya Matumizi katika wizara hiyo.
Alisema kambi hiyo ina wasiwasi wa kutokuwepo ushahidi wowote wa dhamana iliyowekwa iwapo mkopaji atashindwa kurejesha.
Ameir alisema mkopo huo ulitarajiwa kulipwa baada ya miezi sita lakini hadi Machi 26, mwaka huu, ulikuwa haujalipwa.
“Isitoshe, Mkataba huo katika kifungu 10.5 unasema kuwa mkopo huo umedhaminiwa na serikali kwa asilimia 100 pamoja na Benki ya CRDB. Hii inashangaza kwani fedha zenyewe ni za wafanyakazi wa Tanzania, na serirkali yao inadhamini kwa asilimia 100,” alisema.
Ameir alisema Kambi hiyo inaitaka serikali kuhakikisha inachukua hatua za haraka za kiutawala ili kuhakikisha shirika hilo linaendeshwa kama sheria inavyotaka.
Alisema mbali na matatizo hayo ya udhibiti wa fedha za wanachama pia NSSF imetamkwa kuwa ni miongoni mwa taasisi zenye utunzaji mbovu wa kumbukumbu za wafanyakazi ambapo mikataba ya ajira, nakala za vyeti, barua za ajira, taarifa za kupandishwa vyeo, uhamisho na ongezeko la mishahara wakati wa ukaguzi havikuwepo.
Aidha, alisema shirika hilo halizingatii sheria ya ajira ambapo wakati wa ukaguzi iligundulika kuwepo kwa uvunjwaji wa sheria za ajira kwa kutoa ajira bila kufuata taratibu zilizowekwa.
Katika hatua nnyingine, Kambi hiyo ilisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika ukaguzi wake kwenye Shirika hilo iligundua matumizi ya hovyo hovyo ya fedha za wanachama.
Alisema NSSF ilikopesha jumla ya Sh. 1,525,368,525 kwa kampuni ya M/S Medtech toka Aprili 2003 na mkopo ulitakiwa kurejeshwe Desemba 2004, hadi sasa pesa za wanachama hazijarudishwa.
“Kwa ujumla ripoti imebaini kuwa NSSF imekuwa inawekeza sehemu zisizo na tija kwa wanachama,” alisema.
Aliongeza kuwa taarifa hiyo inasema kuwa NSSF ni miongoni mwa taasisi zenye masurufu yanayofikia jumla ya Sh. 22,231,219 ambayo hayajarejeshwa na kwamba imenunua hisa au kuwekeza katika mashirika kadhaa lakini hakuna gawio inayopata.
Alisema fedha zilizowekezwa na NSSF kwenye mabano ni Tanzania Oxygen Ltd (sh. 13,200,000), Tanzania Housing Bank (sh. 495,280,000) na kwamba 1st Adili Bank Corp Litd ilipewa mkopo wenye utata wa sh 3,152,024,742.
Kampuni zingine ambazo NSSF imewekeza bila kupata gawio kwa kipindi chote ni CDC Mbeya Cement (sh. 1,152,024,742), Ubungo Plaza (sh. 9,817,038,702), TANR Share (sh.1,000,000,000), HEPZ Quality Group Share (sh. 47,156,025,113) na PPL pension Properties (sh. 3,500,00). Jumla ya uwekezaji usio na tija ni sh. 62,789,093,299.
Alisema mifano hiyo ni michache inayoashiria udhaifu mkubwa katika upangaji wa miradi na uwekezaji wa NSSF na kwamba inapaswa suala hilo kuchukuliwa kwa uzito maalumu ili kunusuru fedha za wanachama.
CHANZO: NIPASHE

NSSF, Dowans, Muhimbili na Tanesco, zanyooshewa kidole

29th April 2009
Shirika la Umeme (Tanesco).

Mashirika kadhaa ya umma na taasisi nyeti za serikali yamepuuza mapendekezo ya ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yaliyotakiwa kufanyiwa kazi, kwani kasoro zilizogundulika na kutakiwa kurekebishwa zimeendelea kuwepo mwaka mmoja baadaye.
Kasoro hizo ni uvunjaji wa kanuni za matumizi ya fedha za walipa kodi ambazo katika kipindi cha ukaguzi kilichopita zilitakiwa kufanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2007/08 iliyowasilishwa bungeni juzi, baadhi ya taasisi hizo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Taifa (NSSF), Shirika la Umeme (Tanesco), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na taasisi nyingine nyeti za serikali.
Kwa hospitali ya Muhimbili, kwa mfano, ripoti inaonyesha kwamba kuna jengo binafsi lililojengwa katika eneo la hospitali ambalo mkataba unaonyesha kwamba lilitakiwa kuwa mali ya hospitali kuanzia mwaka 1992, lakini limeendelea kuwa mali ya mtu huyo, H.A Kiluvia.
Imeelezwa kuwa jengo hilo kwa sasa kuna benki ya National Microfinance Bank (NMB) na duka la dawa.
“Mkataba umeshamalizika lakini jengo bado liko kwenye himaya ya H. A. Kiluvia kinyume na makubaliano ya mkataba (licha ya mapendekezo yetu ya mwaka 2006/07),” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Ofisi ya CAG pia ilipendekeza, katika ripoti yake iliyopita, kusitishwa kwa mkataba wa Kampuni ya Kuhudumia Makontena Bandarini (TICTS) kutokana na kuongezewa kipindi kingine cha miaka 15 kinyume cha sheria, lakini mkataba bado haujavunjwa hadi ripoti hiyo inaandikwa.
Ripoti inaonyesha kwamba ofisi ya CAG ilipofuatilia mapendekezo hayo yaliyotolewa mwaka 22 06/07, haikupata majibu, hali inayoonekana kwamba hakuna utekelezaji kwa upande wa serikali.
Kadhalika, CAG anasema katika ripoti yake kwamba Tanesco ilishauriwa kuidai kampuni ya M/s Dowans Holdings tozo (liquidated damage) kutokana na kampuni hiyo kukiuka mkataba kwa kushindwa kuzalisha umeme wote wa megawati 100 kama mkataba unavyoonyesha.
Ripoti inaonyesha kwamba ofisi ya CAG haikupata majibu kuhusu utekelezaji wa mapendekezo hayo.
Ofisi ya CAG pia ilipendekeza kwa Hazina kukusanya madeni yatokanayo na mauzo na ubinafsishaji wa mashirika ya umma kutoka kwa wawekezaji.
Ilipendekeza pia kwamba hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wawekezaji walioshindwa kutekeleza majukumu yao ya mikataba ya uwekezaji.
Pia ilipendekeza kwamba mashirika na taasisi za umma ambazo bado zinajiendesha kwa hasara zichukuliwe na serikali au kuuzwa tena.
Hata hivyo, ripoti inasema kwamba mapendekezo hayo hayajafanyiwa kazi hadi ripoti mpya ilipokuwa ikiandaliwa.
Kuhusu NSSF, ofisi ya CAG ilipendekeza isiendelee kukopesha na kwamba kiasi cha mikopo kilichoripotiwa ni kikubwa kuliko inavyotakiwa.
Hata hivyo ripoti inaonyesha kwamba ushauri haukuzingatiwa.

CHANZO: NIPASHE

Benki kupiga mnada Mgodi wa Kiwira

12th March 2011

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja

Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira ambao uligeuzwa kuwa kitega uchumi cha kujipatia fedha za kukopa kutoka taasisi mbalimbali za fedha nchini hivi sasa madeni hayo yameanza kuutokea puani ambapo Benki ya CRDB imeandika barua kwa serikali ikielezea kusudio lake la kutaka kuupiga mnada mgodi huo.
Mgodi huo ambao hadi sasa upo chini ya mwekezaji wa kampuni ya Kiwira Coal and Power Limited (KCPL) licha ya serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja, kutoa taarifa kuwa umerejeshwa serikalini, hadi sasa unadaiwa madeni na taasisi mbalimbali za fedha zaidi ya Sh.28,869,938,996.
Taasisi za fedha ambazo zinaudai mgodi huo ambazo zilikopwa na mwekezaji ni pamoja na CRDB deni lote pamoja na riba ni Sh.bilioni 4.077, Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Sh.bilioni 9.497 na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sh. bilioni 15.294.
Madeni hayo kwa mgodi huo yalibainika wakati Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi wa NSSF, Yakubu Kidula, alipokuwa akitoa taarifa juu ya pendekezo la NSSF la kuchukua kampuni ya Kiwira Coal and POWER Limited kwa wabunge wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAOC).
Alisema kutokana na hali hiyo, Benki ya CRDB imechukua hatua ya kuiandikia barua serikali ikielezea kusudio la kutaka kuupiga mnada mgodi huo kwa kushindwa kulipa deni hilo ambalo mwekezaji huyo alikopa Dola milioni saba kwa lengo zitumike kuzalisha umeme megawati 50.
Kidula alisema hata hivyo, NSSF wameiomba Benki ya CRDB isitishe uamuzi wake wa kutaka kuupiga mnada mgodi huo kwasababu NSSF inakusudia kuwa mwekezaji mpya wa mgodi ambapo itachukua jukumu la kulipa madeni yote yanayodaiwa na taasisi zote zinazoudai mgodi huo.
Kwamujibu wa barua ya CRDB yenye kumbu Na. 3390/654316/4113 ya 28 Julai 2009 ambayo NIPASHE imepata nakala, aliandikiwa Ngeleja, ikitaka serikali kulipa deni hilo lililokopwa na mwekezaji wa kampuni ya Kiwira Coal and Power Project (KCPL) kwa ndiye mdhamini mkuu wa mkopo huo.
Hata hivyo Septemba 5 , 2009 Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, katika barua yake yenye kumbu Na.CDA 48/171/01 aliijibu Benki ya CRDB kwa kueleza kuwa wizara yake ingefanya kazi kwa kushirikiana na wakopeshaji ili kuhakikisha kuwa suala hilo linatatuliwa mapema iwezekanavyo.
Februa mwaka jana, CRDB ilimkumbusha Waziri wa Nishati na Madini kuhusiana na kushindwa kwa kampuni ya KCPL kulipa deni lake na kueleza kuwa hatua iliyobaki ni kwa wakopeshaji kuuza mgodi wa KCPL kwa mnunuzi yeyote ili kurudisha fedha walizoikopesha KPCL.
Pamoja na mfululizo wa barua zilizoandikwa na CRDB, wizara iliendelea kukaa kimya ambapo Disemba mwaka jana (2010) Benki ya CRDB iliandika barua ngingine kwa Waziri yenye kumbu Na. 3390/654316/4113 ikimtaarifu kwamba wakopeshaji hawana njia nyingine zaidi ya kuuza Mgodi wa Kiwira.
CHANZO: NIPASHE

Mafao chini ya NSSF ni ukombozi wa wengi, wanachama zindukeni

13th December 2009
Maoni ya katuni

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni moja ya mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ambalo limepania kujenga maisha bora ya wanachama wake sasa na baadaye. Kudhihirisha hilo, shirika limejikita katika kutoa kinga kwa wanachama wake zaidi ya 460,000 hivi sasa kutokana na majanga ya kiuchumi na kijamii ambayo husababishwa na kupungua kwa kipato.
Mwishoni mwa wiki, uongozi wa juu NSSF uliandaa mkutano mjini Zanzibar ambao uliwashirikisha wahariri toka vyombo vikuu vya habari nchini kuwaelimisha pamoja na mambo mengine huduma zitolewazo na mfuko na namna shirika lilivyojipanga kuboresha maisha ya wanachama wake siku za usoni.
Akitoa mada katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu NSSF, Dk.Ramadhan Dau aliwahakikishia wanachama kwamba mfuko uko imara kwa miaka 20 ijayo, hivyo wasiwe na wasiwasi na wale ambao hawajajiunga kufanya hivyo hima.
Alisema kwa sasa NSSF ina vitenga uchumi vyenye thamani ya sh. bil.848.8 kwa mapato ya bil.58.3/- ilipofika Juni mwaka huu, ikilinganishwa na vitega uchumi vya bil.670.3/- kwa pato la bil.43.9/- mwaka uliotangulia. Malengo mwaka 2009/2010 ni kuwekeza vitega uchumi vya tril.1,078.2/- kwa pato la bil.89.7/-
NSSF imeongeza idadi ya mafao toka matano ya awali na kufikia saba hivi sasa. Mafao ya muda mrefu ni pensheni ya uzeeni, mafao ya mkupuo maalum, pensheni ya ulemavu na pensheni ya urithi. Yale ya muda mfupi ni mafao ya matibabu, mafao ya uzazi, mafao ya kuumia kazini na mafao ya mazishi.
Mafao yote haya, hakika, yamelenga kumpa ahueni ya maisha mwanachama pindi atakapokuwa hajiwezi kutokana na majanga ya kiuchumi na kijamii. Pamoja na ukweli huo, kama alivyoeleza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, bado wapo wanaosita kuchangamkia mafao hayo hasa fao la matibabu pamoja na kwamba ni wanachama wakihofia kukatwa pensheni. “Huduma hiyo ni bure hakuna makato”, alisistiza Mkurugenzi wa Matekelezo NSSF, Crescentus Magori katika mada yake.
Pamoja na ukweli kwamba fao la matibabu ni bure lakini ni idadi ndogo sana ya wanachama waliojitokeza kupata huduma hiyo. “Zilitengwa sh. bil.3/- mwaka 2004 lakini hadi sasa ni mil. 100 tu zilizotumika. Watu bado hawaamini…ni wachache sana wamejitokeza kuliko ilivyotegemewa”, alisema Dk.Dau.
Hata sisi tunajiuliza, kwanini walengwa wanasita kutibiwa bure kupitia fao hilo la matibabu? Je, ni elimu haijawafikia vema kuhusu fao hilo au ni kitu gani. Utafiti wa kina yafaa ufanywe kujua tatizo liko wapi.
Lakini hata hivyo, huduma hiyo ni nzuri na muhimu hasa ikizingatiwa kuwa ni ya bure kwa wanachama wa mfuko huo.
Pia NSSF imeonesha mfano wa kuigwa kwa kuongeza kiwango cha pensheni kwa wanachama kuanzia Septemba mwaka huu kutoka sh.33,200/- hadi 52,000. Hii ni katika jitihada zake za kuwajali wanachama wake.
Ni mfuko uliojiwekea malengo hadi miaka 50 ijayo. Lakini ili ufike huko, yapo mambo mengi yamewekewa mkakati ikiwa ni pamoja na kutaka yawepo maboresho ya sheria zinazolinda mifuko ili iweze kuendelea, kuimarika na hatimaye idumu.
Kwa mfano, Dk.Dau anasema, waliojiajiri wenyewe, sheria haiwalazimishi kujiunga na NSSF. Hawa nao mfuko unataka wajiunge. Au mtu akiacha kazi asipewe fedha zake hadi atimize muda wa kustaafu. Kwa sasa mtu anaruhusiwa kuchukua fedha zake kabla ya kustaafu. Utaratibu huu unatishia maisha ya mfuko wa hifadhi.
Wengine wanataka kuchangia lakini wanachagua fao mojawapo. Kisheria ni lazima wanaojiajiri wenyewe wachangie mafao yote saba, jambo ambalo hawalikubali.
Tunaamini kwamba mamlaka husika zimeshafikishiwa mapendekezo hayo kuona uwezekano wa kuyafanyia kazi ili NSSF na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa wanachama wake.
Siyo siri kwamba mafao ya NSSF yanagusa makundi muhimu ndani ya jamii yetu ambayo ni wazee, walemavu, wanawake na watoto, wafanyakazi na kadhalika, hivyo serikali inapaswa kuunga mkono juhudi zake zilizolenga kujenga maisha ya wanachama wake sasa na baadaye.
Ni imani yetu kwamba waajiri na wafanyakazi wote katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta binafsi, wizara, idara zilizoajiri wafanyakazi ambao wako chini ya mikataba maalum, mashirika ya umma, mtu binafsi aliyejiajiri mwenyewe, watazinduka na kuchangamkia kujiunga na NSSF kunufaika na mafao yatolewayo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Mishahara mipya hailipiki - waajiri

22nd April 2010
  Wasema wafanyakazi wengi watapunguzwa
  Wadai Waziri Juma Kapuya amekurupuka
Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya.

Waajiri katika sekta binafsi na wanasiasa wameilalamikia serikali kupandisha kima cha chini cha mishahara ya sekta binafsi kwa asilimia 100 na wameonyesha wasiwasi wao kwamba kiasi hicho kitakua vigumu kulipa.
Walitoa malalamiko hayo kufuatia tangazo la juzi la Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya (pichani).
Mjini Arusha, baadhi ya waajiri, wameeleza kushtushwa na hatua ya serikali kupandisha mishahara ya wafanyakazi wa sekta binafsi kwa asilimia 100 wakidai kuwa hatua hiyo itawafanya wapunguze wafanyakazi kwa kuwa hawatakubali kupata hasara.
Wamesema hatua hiyo itawafanya washindwe kumudu kulipa mishahara kwa idadi kubwa ya wafanyakazi walionao kwani hakuna ambaye anapenda kupata hasara.
“Ongezeko hili la mishahara litaenda sambamba na ongezeko la mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), hali ambayo itawafanya waajiri walio wengi waingie gharama mara mbili,” alisema Wilson Leguna kutoka kampuni ya Insignia Ltd iliyopo mtaa wa viwanda mjini hapa.
Alisema mwajiri yeyote anataka kupata faida zaidi kwa kupunguza matumizi, hivyo, nyongeza ya mishahara itawapa wakati mgumu.
“Kuongeza mishahara ni kuongeza matumizi, hivyo hali hiyo itawafanya waajiri wengi katika sekta ya biashara kupandisha bei ya bidhaa zao ili kufidia matumizi katika malipo ya mishahara,” alisema.
Hata hivyo, alisema waajiri kama hao hawawezi kupandisha ghafla bei ya bidhaa zao hasa ikizingatiwa kwamba wakati huu ni wa ushindani wa kibiashara. Meneja Mkuu wa kiwanda cha magodoro, TanFoam, Riaz Somji, alisema ameshtushwa na habari ya kupandishwa kwa mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia 100. Hata hivyo, Somji anayemiliki kiwanda hicho chenye wafanyakazi wapatao 120 alikataa kutoa maoni kuhusu nyongeza, kwa maelezo kuwa anayepaswa kufanya hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wake, Bala Subiramania, ambaye yupo safarini.
Alisema menejimenti ya kiwanda hicho itakaa hivi karibuni kutafakari suala hilo. Mwajiri mwingine, mwenye asili ya Kiasia, alisema hakuwa na taarifa yoyote ya nia ya serikali kupandisha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.
Jijini Tanga, baadhi ya waajiri walisema serikali ilipaswa kutafuta mbinu mbadala ili kupata suluhu ya kutatua matatizo ya wafanyakazi badala ya kuwakomoa waajiri wa sekta binafsi.
Baadhi ya waajiri kutoka makampuni ya ulinzi, viwandani, hospitali binafsi na waajiri wa majumbani, wakiongea kwa sharti la kutotaka kutajwa majina yao kwa madai yataleta uchonganishi na watumishi wao, walisema kuwa Serikali ilipaswa kupandisha kwanza kima cha mishahara kwa watumishi wake.
Walisema serikali ilipaswa kutafuta maoni kwanza kutoka kwa waajiri wa sekta binafsi kabla ya kuamua kutoa tangazo hilo kwani litaleta uchochezi na chuki baina ya watumishi wa sekta binafsi na waajiri wao.
Jijini Dar es Salaam, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema mshahara huo ni ‘kiini macho’ na kwamba serikali haina dhamira ya dhati kuhusu ilichosema.
Chadema imesema kama serikali ingekuwa na dhamira ya kweli ingeanza yenyewe kutangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake kabla ya ile ya sekta binafsi.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mnyika, alisema jana kuwa tamko hilo la serikali ni la kisiasa tu kujaribu kuzima mgomo kwa kuwa bado haijatangaza viwango vya mishahara kwa watumishi wake.
Alisema Waziri Kapuya amekurupuka kutoa tamko kuzima shinikizo la kumtaka ajiuzulu, kama alivyoshauriwa na wadau mbalimbali.
Alisema serikali bado pia haijatoa notisi kwenye gazeti la serikali kwa kuwa notisi namba 223 ya mwaka 2007 ilivurugwa, kwa hiyo hata watumishi wa sekta binafsi wasichekelee kwa kuwa kuna dalili zote kuwa tamko hilo ni mchanga wa macho.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa Chama cha Wananchi (CUF), Ashura Mustafa, alisema serikali bado haijatatua matatizo ya wafanyakazi na badala yake imeingiza siasa katika mgogoro huo mkubwa.
Alisema kumekuwa na utendaji mbovu katika idara nyingi za serikali na chanzo kikubwa ni kwa serikali kutowajali wafanyakazi wake ipasavyo.
Alisema watumishi wengi wa umma wanashindwa kuhudumia wananchi hadi watoe rushwa kutokana na uduni wa mishahara.
Alishauri kima cha chini kiwe sawa kwa sekta zote na kwamba hali hiyo inaweza kusaidia ufanisi kuonekana sehemu za kazi.
Mwenyekiti wa PPT Maendeleo, Peter Mziray, alisema kama ni suala la kuongeza mshahara serikali ndiyo inayopaswa kuanza na sekta binafsi inafuata.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samweli Ruhuza, alionyesha wasiwasi kwamba watumishi wa umma watabaki kwenye hali ngumu na hivyo wanaweza kupungua kwa asilimia kubwa kwa kutimkia sekta binafsi.
Ruhuzu alisema sekta binafsi inajiendesha kulingana na uwekezaji, hivyo mwajiri wake atakapofanya vizuri katika kuzalisha kipato ndipo hupatiwa mshahara mzuri.
Alisema kuwa serikali inatakiwa kuangalia suala hilo kwa kina zaidi kwani mtumishi wa umma hulipwa kulingana na cheo chake tofauti na sekta binafsi.
Alisema kuwa suala hilo litasababisha wataalamu wa utumishi wa umma kuondoka serikalini na kuelekea sekta binafsi kwa ajili ya kufuata maslahi.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, alisema suala la serikali kutangaza ongezeko la mshahara katika sekta binafsi bado limekuwa ni kitendawili kutokana na kwamba jambo hilo halijatolewa ufafanuzi wa kutosha.
Mrema alisema alipokuwa akitizama taarifa ya habari kuhusiana na tangazo la serikali, alishangaa kumuona Profesa Kapuya akisita kutaja kiasi cha fedha kilichoongezeka.
Alisema Kapuya alitakiwa kutoa ufafanuzi wa kina kwa mfano, kueleza mtumishi wa ndani atalipwa kiasi gani na kadhalika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Agrey Mlinuka, alisema chama chake kitatoa tamko kuhusu ongezeko hilo ambalo limetangazwa na serikali kitakapopata taarifa rasmi ya serikali.
Imeandikwa na John Ngunge, Arusha, Lulu George, Tanga, Joseph Mwendapole na Beatrice Shayo, Dar.
CHANZO: NIPASHE

Wanachama wa NSSF Mwanza wachota bil. 5/-

22nd March 2010
Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF)

Wanachama 2,820 wa Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF) mkoani Mwanza, wamelipwa mafao yao yanayofikia Sh. bilioni 5.1 katika kipindi cha miezi minane.
Wanachama hao walilipwa kati ya Julai, mwaka jana na Februari, mwaka huu kufuatia maombi yao waliyotuma kwenye mfuko huko kwa kipindi hicho.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Meneja Mkuu wa (NSSF) mkoa wa Mwanza, Sostenes Nguma, katika maadhimisho ya Wiki ya NSSF yanayoendelea kote nchini.
Alisema katika kipindi hicho, NSSF mkoa wa Mwanza ulikusanya zaidi ya Sh. bilioni 11.3 kutoka kwa wanachama wake ambayo ni sawa ya asilimia 92.6 ya lengo la kukusanya zaidi ya Sh. bilioni l. 12.2.
Nguma alisema kudorora kwa hali ya uchumi wa dunia kumechangia Mfuko huo kutofikia malengo waliyojiwekea kwani makusanyo mengi katika mwaka huu hutokana na sekta ya madini, wafanyabiashara na wavuvi.
Kuhusu fao la matibabu linalotolewa na Mfuko huo, Nguma alisema hutolewa bure kwa wanachama waliotimiza masharti na si kweli kwamba hukatwa mafao yao.
Alisema katika Wiki ya NSSF, mfuko huo umekuwa ukijihusisha katika masuala ya kijamii ambapo kwa mwaka huu umepanda miti 1,000 ya matunda, kivuli na maua katika Shule ya Sekondari Nyamagana.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyamagana, Eromena Mallya, aliishukuru NSSF kwa kuchagua shule yake na kupanda miti hiyo na kuahidi kuitunza kwa hali na mali.
“Tunaushukuru Mfuko kwa kuiona shule yangu inafaa kuwa mfano kati ya sekondari 36 zilizo wilayani Nyamagana, watutembelee mara kwa mara na wataona namna tunavyoianza ikiwa ni sehemu ya utunzaji wa mazingira,” alisema Mallya.
CHANZO: NIPASHE

Wastaafu Elimu Kibaha wagomea mafao ya PPF

3rd June 2010
Rais Jakaya Kikwete

Wafanyakazi waliostaafu wa Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani, wamegoma kupokea mafao yao kutoka Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF), kwa madai kwamba fedha zilizotolewa na mfuko huo ni kidogo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa wastaafu hao, Ally Gombati, alisema wafanyakazi walioamua kugomea mafao hayo ni wale waliostaafu kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka huu.
Alisema wameyakataa mafao hayo kupinga mfumo unaotumiwa na PPF ya kuwalipa wafanyakazi waliostaafu malipo kidogo tofauti na mifuko mingine ambayo inalipa wanachama wake kiwango ambacho kinamfanya mstaafu kuishi kwa muda mrefu.
"Tumeamua kueleza bayana kuwa hatuwezi kuchukua pesa za mafao hadi hapo PPF watakapofanya marekebisho na kulipa kama ilivyo mifuko mingine," alisema Gombati.
Alisema katika shirika hilo, kuna wafanyakazi wengi waliostaafu lakini baadhi ya wengine waliokuwa wanachama wa mifuko mingine ya jamii ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya (NSSF) ambao walilipwa kiasi kikubwa cha fedha hadi kufikia Sh. milioni 25 lakini wao waliambulia Shilingi milioni tano tu.
"Kitu hiki hakiwezekani kwani hawa wafanyakazi wenzetu tulikuwa na cheo kimoja lakini wamepewa mafao yanayowawezesha kuanza maisha mapya bila kutetereka, iweje sisi tuliojiunga na mfuko huo tuondoke masikini wa kutupwa," alihoji Mwenyekiti huyo.
Pamoja na hayo, Gombati alisema baada ya kuchukua hatua hiyo, walikwenda makao makuu ya mfuko huo kueleza msimamo huo lakini hawakupata ufumbuzi.
Aidha, wastaafu hao, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati mgogoro kati yao na mfuko huo ili hata watu wanaotarajia kustaafu kwa kipindi hiki waweze kulipwa mafao kulingana na muda waliolitumikia taifa.
Hata hivyo, juhudi za kumpata msemaji wa mfuko huo hazikuzaa matunda jana.
CHANZO: NIPASHE

NSSF wajitoa kuzalisha umeme

3rd February 2011
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesema umeanza mchakato wa kuzalisha megwati 300 za umeme na kuziingiza katika grid ya taifa ifikapo Desemba mwaka huu, ili kusaidia kuondoa matatizo ya umeme yanayoikumba nchi kwa sasa.
Mpango huo ulitangazwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, jijini Arusha.
Dk. Dau bila kutoa ufafanuzi kuhusu mahali ambapo umeme huo utazalishwa, alisema tayari mfuko wake umeshateua mtaalamu mshauri kwa ajili ya kutekelezwa kwa mradi huo, ambao pia hakutaja gharama zake.
Hatua hiyo imekuja wakati nchi ikikabiliwa na matatizo ya umeme na kulilazimisha Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza mgawo mara kwa mara.
Dk. Dau alikuwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa NSSF unaofanyika jijini hapa na kuhudhuriwa pia na wawakilishi wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda na Burundi.

Aidha, Dk. Dau alisema kuwa mfuko wake unaangalia uwezekano wa kutandaza bomba la gesi kutoka Mnazi Bay hadi Dar es Salaam na Mwanza.
Madhumuni ni kusambaza gesi inayozalishwa hapa nchini katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” alisema Dk. Dau bila kutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na mradi huo.
Kuhusu wanachama wa mfuko huo, Dk. Dau alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wameongezeka kutoka 380,000 mwaka 2005/06 hadi 506,216 mwaka 2009/10 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 33.
Alisema ifikapo Juni mwaka huu wanachama wanategemewa kufikia 518,410.
Kwa upande wa makusanyo, alisema yameongezeka kutoka Sh. bilioni 126.96 hadi Sh. bilioni 315.31 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 148.
Mategemeo yetu ni kukusanya kiasi cha Sh. bilioni 404.58 ifikapo Juni mwaka huu,” alisema.
Akizungumzia uwekezaji, Dk. Dau alisema shirika limeendelea kuwekeza raslimali katika miradi ya muda mfupi na mrefu. Kutoka mwaka 2005/6 hadi 2009/10 uwekezaji wa Mfuko uliongezeka kutoka Sh. 424.89 bilioni hadi Sh. trilioni 1.03.
Alisema uwekezaji huu umesaidia kuongeza ajira na kuboresha thamani ya shirika.
Kuhusu ulipaji wa mafao, alsema Oktoba mwaka jana, NSSF ilipandisha pensheni kwa asilimia 52 ambapo kutokana na mabadiliko hayo kiwango cha chini cha pensheni kwa wastaafu kimeongezeka kutoka Sh. 52,000 hadi Sh. 80,000 kwa mwezi.
Katika hatua nyingine, Dk. Dau alisema tathmini inayoishia Juni 2009, imeonyesha kuwa NSSF inaweza kujiendesha, hata kama shirika litaacha kukusanya michango na bila kupata mapato yo yote kutoka katika vitega uchumi vyake, bado linaweza kuendelea kutoa mafao yote saba na kukidhi gharama za uendeshaji kwa muda wa miaka saba.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, aliipongeza NSSF kwa kujizatiti kuanza ujenzi wa daraja la Kigamboni na mipango ya kuzalisha megawati 300 za umeme na kuziweka katika gridi ya taifa pamoja na kusafirisha gesi asilia.
Hii ni mipango mizuri na ni endelevu kwa ustawi na maendeleo ya taifa. Ujenzi wa daraja la Kigamboni ambao kwa muda mrefu wananchi walitarajia kuwa litajengwa sasa watapata faraja kusikia kuwa utaanza wakati wowote,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme ni jambo la muhimu zaidi na ni muafaka kwa uchumi wa taifa kwani upungufu wa umeme/kukatika mara kwa mara kwa umeme kunaathiri sana mitambo ya uzalishaji wa bidhaa viwandani, tija na ufanisi katika maofisi kupungua na hivyo kuleta athari kwa taifa,” alisema.
Lakini athari kubwa zaidi ni ile ya kukimbiza vitega uchumi kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza wa ndani na nje ya nchi na hivyo kusababisha ajira kwa wananchi kukosekana,” alisema, na kuongeza:
Jitihada hizi zinazofanyika na NSSF zitapunguza sana kama si kuondoa kabisa kero hizi.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF, Abubakar Rajabu, aliiomba serikali kutoa uamuzi wa kuukubalia mfuko huo kujenga majengo ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nje ya nchi ili kuokoa fedha za serikali kwa kupanga ofisi.
CHANZO: NIPASHE

Majambazi yavamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu NSSF

18th April 2010
  Kiasi kikubwa cha fedha chaibwa
Dk. Ramadhan Dau

Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi, jana walivamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau na kuiba kiasi kikubwa cha fedha.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo watu hao walibomoa ukuta unaozunguka nyumba hiyo na kuingia ndani.
Akizungumza na Nipashe Jumapili, Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Elias Kalinga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema hata hivyo, watu hao hawakumjeruhi mtu na hawakuchukua kitu chochote zaidi ya fedha ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye masanduku maalum ya kuhifadhia fedha.
"Ni kweli tukio hilo limetokea majira ya saa 9 (juzi) usiku ambapo majambazi hao ambao bado hatujajua idadi yao, waliingia ndani baada ya kubomoa ukuta wa nyumba hiyo," alisema Kalinga.
Aidha, Kamanda huyo wa Polisi alisema baada ya kuingia ndani waliwakamata walinzi wawili wa nyumba hiyo waliokuwa na silaha aina ya shotgun na kuwafunga kamba kabla ya kuingia chumbani na kuiba fedha hizo ambazo kiasi bado hakijajulikana.
Alisema baada ya kuwafunga kamba walinzi hao waliingia chumbani kwa mwenye nyumba (Dk. Dau) na kubomoa sanduku la kuifadhia fedha na kuondoka na fedha hizo.
Alisema wakati tukio hilo linatokea, Dk. Dau hakuwepo nyumbani hapo pamoja na familia yake na walibaki walinzi hao.
Aidha, Kamanda Kalinga alisema kutokana na mazingira ya tukio hilo kuwa ya kutatanisha, Jeshi la Polisi linawashikilia walinzi wa nyumba hiyo, Deus Mtatilo (52) pamoja na Yusuph Bakari (59) waliokuwepo siku ya tukio hilo.
Alisema mazingira ya tukio hilo yanonyesha kuwa na ulakini kutokana na ukweli kuwa walinzi hao walikuwa na silaha za moto ambazo hawakuzitumia wakati wa tukio na pia hakukuwepo kwa milio yoyote ya risasi. Alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

NSSF kuanza ujenzi wa Kigamboni mwaka huu

23rd March 2011
Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limesisitiza kuwa ujenzi wa daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam unatarajia kuanza muda wowote mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau, alitoa kauli hiyo jana kwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Dk. Dau aliwaambia wajumbe wa Kamati hiyo kuwa NSSF ina fedha za kutosha kukamilisha mradi huo ambao kwa sasa unafikia Dola za Marekani milioni 120.
Kwa upande wa utalii Kamati ya Hesabu za Serikali PAC, wajumbe wake walichachamaa na kutaka maelezo ni kwa nini wawekezaji katika mahoteli wanajenga kwa kutumia makuti.Wabunge wa Kamati hiyo walisema kitendo cha wawekezaji hao kujenga kwa kutumia makuti ni dalili ya wizi na hujuma kwa Serikali.
Walisema vifaa vingi vya wawekezaji vinasamehewa kodi hivyo hawana sababu ya kutumia makuti ambayo ni ya bei nafuu lakini sio ya kudumu na hatari kwa wateja kwa kuwa yanaweza kuungua muda wowote.Wabunge hao walitaka kupatiwa maelezo ni kwa nini baadhi ya mahoteli ya Kitalii yanajibadilisha majina baada ya kumaliza mkataba wa kufanya biashara kwa kuwa wanalenga kukwepa kulipa kodi.
Kamati hiyo pia ilimhoji Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutokana na kushuka kwa mapato ya serikali ambayo yeye anahusika kuyakusanya.
Akijibu hojahizo za Wabunge hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi, alikiri kuwepo tatizo hilo, lakini akasema tatizo halipo kwa wizara yake pekee bali kuna wadau wengi wanaohusika.
CHANZO: NIPASHE

Sawa NSSF, wengine waige

4th February 2011
Chapa
Maoni
Maoni ya katuni

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umetangaza kwamba umeanza mchakato wa kuzalisha megawati 300 za umeme ifikapo Desemba, mwaka huu. Hatua ya mfuko huo ina lengo la kusaidia kukabiliana na matatizo ya umeme yanayoikumba nchi kwa sasa na kulilazimisha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kugawa nishati hiyo kwa mgawo.
Mpango huo ulitangazwa jijini Arusha juzi na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, ingawa hakutoa ufafanuzi kuhusu mahali ambapo umeme huo utazalishwa na gharama za mradi huo.
Aidha, Dk. Dau alisema kuwa mfuko wake unaangalia uwezekano wa kutandaza bomba la gesi kutoka Mnazi Bay hadi Dar es Salaam na Mwanza.
Hatua ya mfumo huo kubuni mradi wa kufua umeme huo imekuja wakati nchi ikiwa katika matatizo makubwa ya ukosefu wa umeme wa uhakika.
Tatizo la umeme nchini ni la muda mrefu kiasi cha kuilazimisha tanesco kuingia katika mikataba na kampuni nyingi za kigeni za kufua umeme wa dharura ikiwemo Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Aggreko na Richmond/Dowans kwa kutaja baadhi.
Hata hivyo, baadhi ya mikataba hiyo hadi sasa inalalamikiwa kwamba imegharimu fedha nyingi za walipakodi na kwamba imewanufaisha vigogo na watu wachache.
Kwa mfano, mchakato wa kuipatia mkataba wa Richmond ulibainika kuwa ulitawaliwa na mazingira ya rushwa kutokana na kampuni hiyo kupewa tenda ya kufua umeme wa dharura wa megawati 100 bila kuwa na uwezo, na baadaye kuirithisha mkataba huo kampuni ya Dowans Tanzania Limited kinyemela.
Dowans licha ya kurithi mkataba wa Richmond bila kupitia utaratibu wa kisheria, iliishitaki Tanesco katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) kwa kusitisha mkataba wake baada ya Bunge kuazimia usitishwe.
Mkataba wa Richmond uliitikisa nchi baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri wawili Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi kulazimika kujiuzulu Februari mwaka 2008, baada ya kuhusishwa na kashfa hiyo.
Licha ya migongano ambayo imekuwa ikijitokeza kati ya serikali na makampuni ya kigeni ya kufua umeme, nchi inakabiliwa na utatizo la kutokuwa na umeme wa uhakika.
Nchi inahitaji angalao megawati 1,000, lakini imekuwa ikishindikana kutokana na sababu mbalimbali hususan kukauka mara kwa mara kwa mabwawa ya kuzalisha umeme kutokana na ukame.
Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakichangia kukosekana kwa mvua za uhakika na hivyo kuchangia uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.
Tunaipongeza NSSF kwa kuliona tatizo hilo ambalo ni janga la kitaifa na kuamua kujitosa katika mchakato wa kuzalisha umeme.
Kwa kuwa NSSF ina mtaji wa kutosha, bila shaka itafanikiwa kuutekeleza mchakato huo na kuzalisha umeme huo ifikapo Desemba mwaka jana.
Mfuko huo umetangaza kuutekeleza mradi huo wakati hali imeanza kuwa mbaya kwa uchumi wanchi. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, jana alisema kuwa mgawo wa umeme unaoendelea utaathiri uchumi katika robo ya mwisho wa mwaka huu wa fedja .
Itakumbukwa kwamba Tanesco ilipandisha gharama za umeme kwa asilimia 18.5 Desemba mwaka jana, hatua ambayo imelalamikiwa na wananchi wengi kwamba itawaumiza kutokana na gharama za maisha kupanda maradufu.
Hatua hiyo pia imelalamikiwa na vyama vya wafanyabiashara kwamba itawaathiri wao na wawekezaji.
Ni vizuri NSSF ikajipanga kwa ajili ya kufanikiwa lengo hilo katika muda uliopangwa kwa kutilia maanani kwamba mfuko huo unaendesha miradi mingi nchini.
Hatua hiyo hainabudi kuwa changamoto kwa mashirika mengine nchini yenye mitaji ya kutosha kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika miradi ya kufua umeme badala ya kusubiri Tanesco kufanya hivyo.
Huu ndio wakati kwa serikali kujipanga upya kubuni namna ya kupata vyanzo vingine vya nishati ya uhakika.

CHANZO: NIPASHE

JK atoa changamoto kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii

24th March 2011
Chapa
Maoni
Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA), kuyaangalia kwa makini malalamiko ya wafanyakazi kuhusu tofauti kubwa ya utoaji wa mafao ya mkupuo na pensheni ya uzeeni, iliyopo kati ya mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii na mwingine.
Mifuko hiyo, ni pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Pensheni ya Wafanyakazi wa Serikali Kuu (GEPF), Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni nchini (PPF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya SSRA pamoja na nembo ya mamlaka hiyo, inayosimamia mifuko hiyo.
Alisema kutokana na tofauti hizo, wafanyakazi wenye viwango sawa vya mishahara na muda sawa wa utumishi wanapostaafu, mmoja anapata mafao hadi mara tatu zaidi ya mwenzake aliye mfuko mwingine, na kusema: “Hili ni jambo la kuliangalia kwa makini sana.”
Hata hivyo, aliipongeza SSRA kwa uamuzi wake wa kuajiri Mshauri Mwelekezi anayeshughulikia suala hilo ili kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuwapo kwa uwiano mzuri wa mafao kati ya mfuko na mfuko, na kushauri uamuzi utakaofikiwa, uzingatie afya ya mifuko na pia tathmini ihakikishe serikali inapunguziwa mzigo.
Pia aliitaka SSRA kuangalia malalamiko ya wastaafu kwamba, mafao ya pensheni hayazingatii mfumuko wa bei, viwango vya riba katika masoko na ukuaji wa uchumi, hali ambayo alisema inasababisha wengi wao kupata pensheni isiyokidhi maisha yao ya kawaida.
Alisema uanzishwaji wa mfuko wa pensheni ya wazee, ni jambo lisiloepukika hivi sasa nchini kwani inasikitisha kusikia kuwa ni asilimia nne tu ya wazee ndiyo wanaopata pensheni.
Aliitaka SSRA kwa kushirikiana na wadau, kuandaa mkakati wa kutekeleza jambo hilo akisema kuanzisha pensheni ya wazee, serikali itafanikiwa kupunguza kiwango cha umaskini kwa zaidi ya asilimia 10.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SSRA, Siraju Kaboyonga, alisema wafanyakazi wengi nchini, bado hawajatambua ipasavyo umuhimu wa hifadhi ya jamii, hali ambayo alisema inachangia kuwakatisha tamaa baadhi ya wanachama watarajiwa kuhiari kujiunga katika mifuko hiyo.
CHANZO: NIPASHE

Serikali yakiri mafao ya wastaafu hayatoshi

16th February 2011
Chapa
Maoni

Serikali imekiri kuwa mafao yanayotolewa hivi sasa na mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii nchini bado ni madogo kulinganisha na hali ya maisha.
Vile vile, imesema imejipanga kuifanyia marekebisho makubwa mifuko hiyo ili iweze kutoa mafao makubwa zaidi kwa wanachama wake tofauti na mafao wanayoyapata sasa.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano baina ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na waandishi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Kamishna Msaidizi wa Kazi (Hifadhi ya Jamii), Daudi Kaali, alisema mafao yanayotolewa sasa ni duni mahitaji halisi ya wakati huu hivyo kuna haja ya kufanya marekebisho.
Alisema ingawa hali iko hivyo, baadhi ya mifuko imekuwa ikijitahidi kuongeza mafao kila inapoona inafaa na alitoa mfano wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambao hivi karibuni uliongeza mafano kwa wanachama wake kutoka shilingi 52,000 kwa mwezi hadi 80,000.
Alisema baadhi ya mifuko mingine nayo imeongeza mafao hayo kutoka shilingi 21,000 hadi 40,000.
Kaali alisema mamlaka ya SSRA kusimamia mabadiliko ya mifuko hiyo ili iweze kutoa mafao manono yatakayowawezesha wastaafu kuishi maisha mazuri zaidi.
Alisema vile vile mifuko ya hifadhi ya jamii inawajibu wa kusaidia watu wa makundi yasiyojiweza kama wanavyochangia katika maeneo mengine.
Naye Mkurugenzi wa Mipangop na Utafiti wa SSRA, Ansgar Mushi alisema mafao yanayotolewa yanapaswa kulingana na thamani ya pesa ya wakati uliopo.
Alisema mifuko ya hifadhi ya jamii iwekeze kokote inakotaka lakini inatakiwa mafao inayotoa yawe na maana kubwa kwa maisha ya wanachama wao.
Alisema hivi sasa asilimia 3.5 tu ya watanzania ndio wako katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba SSRA imejipanga angalau kuongeza idadi hiyo hadi kufikia asilimia 20 kwa muda mfupi ujao.
Tunapaswa kutoka hapo tulipo kwenda hadi asilimia 20, twende 50 hadi asilimia 100 maana hifadhi ya jamii ni haki ya msingi na inahusu haki za binadamu, kwa kuwa kuishi ni haki ya binadamu lazima vyombo vya umma kama SSRA imwezeshe mtu kuishi maisha mazuri,” alisema.
Alisema utafiti uliofanywa na Shirika la Kazi Duniani miaka michache iliyopita unaonyesha kuwa asilimia 35 ya watu wanaofanyakazi hapa nchini ni maskini na wanapostaafu wanaishi maisha ya shida.
Alisema mifuko ya hifadhi ya jamii iboreshwe ili iweze kutoa mafao ya kuwanufaisha wastaafu.
SSRA inawajibu wa kuhakikisha mfumo huu unawajumisha watanzania wengi na hata mafao yanayotolewa yawe ya viwango vya kimataifa na watu wapate huduma zinazolingana hivi sasa tofauti ya mafao ni kubwa sana baina ya makundi katika jamii,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya SSRA, Siraju kaboyonga alisema tatizo la ucheleweshaji wa mafao katika mifuko ya jamii inasababishwa na ukosefu wa utunzaji mzuri wa kumbukumbu.
Alisema kuna wakati wanachama wamekuwa wakiulizwa barua za ajira zao kabla ya kupata mafao yao jambo linalowawea gumu kwani wengi wao waliajiriwa miaka mingi iliyopita.
Mimi niliajiriwa Benki Ku ya Tanzania (BoT), mwaka 1974 leo hii ukiniambia nilete barua ya mwajiri wangu ndipo unipe mafao yangu utakuwa unanitesa maana sina, utunzaji wa kumbukumbu ni changamoto kubwa katika utoaji wa mafao ya wanachama,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

Mifuko ya hifadhi ya jamii yaaswa kuboresha mafao ya wanachama

13th July 2011
Chapa
Maoni
Hifadhi ya jamii (NSSF)
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe), kimeitaka mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSF) na ya watumishi wa serikali za mitaa (LAPF) kuboresha mafao ya wanachama wao ili wanapostaafu wapate mafao yatakayowawezesha kujikwamua kiuchumi tofauti na ilivyo sasa.
Katibu wa Tughe mkoa wa Mara, Watson Lushakuzi, alitoa kauli hiyo katika taarifa yake ya utekelezaji wa kazi wa chama hicho katika kipindi cha miaka mitano iliyopita iliyowasilishwa kwenye mkutano mkuu wa Tughe mkoa.
Lushakuzi alisema mafao yanayotolewa kwa watumishi wa mifuko hiyo ni kidogo sana jambo linalowafanya wastaafu kuendelea kukabiliwa na hali ya umaskini licha ya kutumikia utumishi wao kwa zaidi ya miaka 30.
Alitolea mfano wa watumishi wengi waliostaafu miaka ya hivi karibuni wakiwa wamejiunga na mifuko hiyo wamejikuta wakiambualia kiasi cha kati ya Sh. 700,000 na milioni 1.2 huku wenzao wa Mfuko wa Utumishi wa Umma (PSPF) wakivuna mamilioni ya shilingi wanapostaafu.
Ameishauri mifuko hiyo ya NSSF, LAPF, PPF na GEPF kuboresha huduma ya mifuko kwa wanachama wake kama ilivyofanyika kwa Mfuko wa Watumishi wa Umma (PSPF) badala ya kuegemea zaidi kutumia fedha za wanachama kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo ile ya ujenzi wa majengo ya kibiashara, madaraja na vivuko.
Katibu huyo wa Tughe mkoani Mara ambaye pia ni mwanachama wa NSSF, alisema licha ya makato yanayofanywa na mifuko hiyo, bado huduma wanazotakiwa kupewa wanachama hazitolewi kabisa ikiwa ni pamoja na matibabu, mafao ya ulemavu, huduma za mazishi huku wastaafu wakikosa pesheni ya kila mwezi.
CHANZO: NIPASHE

SSRA yaanisha changamoto mifuko ya hifadhi ya jamii

8th October 2011
Chapa
Maoni
Muundo wa kisheria wa mifuko ya hifadhi jamii nchini ni moja changamoto zinazoikabili Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA).
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam juzi na Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, alipozungumza na wahariri wakuu wa vyombo vya habari kuhusu kazi za Mamlaka hiyo katika kusimamia mifuko ya jamii nchini.
Alisema hali ilivyo sasa mifuko hiyo kisheria inaripoti kwa wizara tofauti, akitaja kuwa Mfuko wa Pensheni Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF) na GEPF iko chini ya Wizara ya Fedha; Mfuko wa Bima Afya (NHIF) uko chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) chini ya Wizara ya Kazi na Ajira na Mfuko wa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF) uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na za Serikali Mitaa (Tamisemi).
Kadhalika, Isaka alisema kila mfuko una sera yake ya uwekezaji, wigo finyu wa hifadhi ya jamii kwa Watanzania yote kwa pamoja ikiwa imesajili asilimia mbili tu ya Watanzania wote.
Mifuko hiyo ina jumla ya wanachama 853,531 kati ya Watanzania milioni 42.
Mkurugenzi huyo alitaja changamoto nyingine kuwa ni mfumo ulipo sasa unabana wanachama kwani hauruhusu kuhamia mfuko mwingine; fofauti kwenye ukokotoaji wa mafao, tofauti kubwa ya mafao kati ya mifuko; ukosefu wa takwimu sahihi; gharama kubwa za uendeshaji wa mifuko, uelewa mdogo wa hifadhi ya jamii kwa watunga sera, waajiri na waajiriwa na umma kwa ujumla.
Isaka alisema ukosefu wa pensheni ya wazee ni changamoto kubwa kwani ni asilimia nne tu ya wazee ndio wanaopata mafao hayo.
Alisema mamlaka hiyo mpya kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepata mtathmini ambaye anapitia tathimini zote za mifuko, hali ambayo itawasaidia kujua thamani halisi ya mifuko yote nchini.
Alisema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, SSRA watatoa taarifa na miongozo mbalimbali ili kusimamia vema sekta ya mifuko ya jamii nchini.
Isaka alisema SSRA inatarajia kuwa na wiki ya hifadhi ya jamii ambayo itafanyika Novemba mwaka huu ambayo mifuko yote ya hifadhi ya jamii itapata fursa ya kueleza umma shughuli wanazofanya ili Watanzania waijue.

CHANZO: NIPASHE

Ujenzi wa daraja la Kigamboni sasa kuanza mwakani

9th November 2011
Chapa
Maoni
Hatimaye ujenzi wa daraja la Kigamboni lililokuwa likisubiriwa na wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam, unatarajia kuanza mapema mwakani.
Daraja hilo linatarajia kujengwa eneo la Kurasini ambapo litaunganisha mji wa Kigamboni na sehemu zingine za jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika maonyesho ya wiki Mashirika ya Hifadhi za Jamii, yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Ofisa Mkuu wa miradi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), John Ndazi, alisema tenda zilizotangazwa kwa ajili ya kupata kampuni itakayojenga daraja hilo zitafunguliwa mwezi ujao.
Ndazi alisema baada ya kupata kampuni moja, kazi ya ujenzi itaanza mapema mwaka ujao ambao utagharimu dola za Marekani milioni 130. Alisema serikali itatoa asilimia 40 ya fedha hizo na NSSF itatoa asilimia 60 na kwamba baada ya ujenzi wake kukamilika, magari yatakayokuwa yanapita katika daraja hilo yatakuwa yanalipia.
“Magari yote yatakuwa yanalipia wakati yanapita katika daraja hilo kwa kipindi cha miaka 25 na baada ya hapo daraja litakuwa mali ya serikali,” alisema. Daraja hilo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya NSSF ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu na wananchi wengi lakini kwa bahati mbaya uanzishwaji wake umekuwa kitendawili.
Aidha, NSSF imesema inatarajia kujenga nyumba 18,000 za bei nafuu ambazo itaziuza kwa wanachama wake.
Maonyesho hayo ya wiki ya mifuko ya hifadhi yalifunguliwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka na kuhudhuriwa na wananchi mbalimbali.
CHANZO: NIPASHE

Ujenzi daraja la Kigamboni wanukia

21st November 2011
Chapa
Maoni
Wakandarasi saba ambao wamefanikiwa kupita katika mchakato wa awali wa kumpata mkandarasi atakayeshinda zabuni ya ujenzi wa daraja la Kigamboni tayari wamefanya ukaguzi katika eneo hilo. 
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martini Ntemo, alisema wakandarasi hao wametembelea eneo hilo mapema wiki hii kwa ajili ya kufanya tathmini ya ujenzi.

Alisema kabla ya mchakato huo wa kuwapata wazabuni walijitokeza wakandarasi 16 walichambuliwa na ndipo walipopatikana hao saba ambao wanashindanishwa.

Ntemo alisema lengo la ziara hiyo ni  kuwapatia maelezo ya kitaalam wakandarasi hao kuhusu maudhui ya mradi husika na changamoto zake kabla ya kuwasilisha makisio yao kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. 

Alisema ujenzi wa daraja hilo unatarajia kuanza mwanzoni mwa mwaka 2012 na kwamba tayari zimeshatengwa bilioni 130 kwa ajili ya zoezi hilo.

Hata hivyo, alisema daraja  hilo ambalo ni la kisasa zaidi kujengwa hapa nchini ambapo litakuwa na barabara tatu kila upande yaani kuwa na uwezo wa kuruhusu magari sita kupita kwa wakati mmoja. 

“Daraja hilo linatarajiwa kuwa na urefu wa mita 600 na litakapokamilika litakuwa ni kiungo muhimu kati ya Jiji la Dar es Salaam na Kigamboni na pia litachangia kupunguza msongamano wa magari hapa jijini," alisema Ntemo 

Alisema Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF tayari limeshatoa Sh bilioni 100  kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa daraja hilo kwa kushirikiana na Wizara hiyo ambapo watachangia asilimia 40.

Aidha, alisema mchango huo wa NSSF  ni moja ya maagizo ambayo aliyatoa Waziri wa Ujenzi, Dk John  Magufuli  Mwezi Machi mwaka huu ambapo aliwataka kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa usafiri kwa wakazi wa maeneo ya Kigamboni unaimarishwa na hivyo kuondoa kero ya usafiri.

 Ntemo alisema NSSF itachangia  asilimia 60 na Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itachangia asilimia 40 zilizobakia. 
 
CHANZO: NIPASHE

Mkataba wa ujenzi daraja la Kigamboni wasainiwa

10th January 2012
Chapa
Maoni
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ramadhani Dau, akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Shi Yuan kutoka kampuni ya ujenzi ya China Railways Constructin Engineering Group, kwa pamoja wakiweka saini ya mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigamboni na maungio yake jijini Dar es Salaam jana. Kazi hiyo ya ujenzi inatarajiwa kuchukua miezi 36.(PICHA: OMAR FUNGO)
Hatimaye ujenzi wa daraja la Kigamboni unatarajiwa kuanza hivi karibuni, baada ya jana Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na mkarandasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo, kutia saini mkataba wa makubaliano.

Ujenzi huo utatekelezwa na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group Co. Ltd kwa kushirikiana na China Major Bridge Co. Ltd na utagharimu Sh. 214,639,445,523.80 kwa kipindi cha miaka mitatu.
MAGUFULI: TUFANYE KAZI, TUACHE SIASA
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alimtaka mkandarasi kukamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo hata kabla ya muda uliowekwa, lakini azingatie ubora wa kazi.
“Sioni sababu ya kusubiri muda huo kwa sababu pesa zipo; nataka mradi huu ukamilike kabla ya muda uliopangwa ili Rais Jakaya Kikwete auzindue kabla hajamaliza muda wake,” alisema.
Dk. Mgufuli, aliwaasa viongozi na wananchi kwa ujumla kuacha siasa kwenye masuala yanayohusu maendeleo kwa kuwa siasa inakwamisha mipango mbalimbali.
“Watanzania sasa wamechoka na maneno wanataka utekelezaji, tufanyekazi tuache siasa, zitatupotezea muda na zitatupeleka pabaya,” alisema Dk. Magufuli.
Aliongeza: “Ifike mahali tuache kusimamia siasa tupambane kuwaletea Watanzania maendeleo.”
Kuhusu miradi mingine, alisema serikali inatekeleza miradi mingi ya ujenzi wa barabara na madaraja na kwamba makandarasi wamekuwa wakituma maombi kila siku.
Alisema serikali imejipanga kupanua barabara ya Morogoro kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze na ya kutoka Arusha-Himo, mkoani Kilimanjaro; pamoja na ile ya mabasi ya mwendokasi kutoka Kimara hadi Kivukoni, jijini Dar es Salaam.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, alisema daraja hilo litakuwa la njia sita za lami za magari na njia za waenda kwa miguu.
Aliishukuru serikali kwa kukubali kuchangia asilimia 40 ya gharama za ujenzi na kuahidi kwamba shirika lake litaendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali yenye manufaa kwa taifa.
AJIRA 2,000 KUZALISHWA
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema mradi huo utazalisha ajira za muda mfupi zaidi ya 2,000 na kuwataka wananchi hususani vijana kuzichangamkia na kuhakikisha wanafanyakazi kwa bidii na uadilifu.
Hata hivyo, aliwaonya watu wenye tabia za wizi kutothubutu kwenda kwenye mradi huo kwa kuwa ataimarisha ulinzi kwenye eneo hilo: “Hata ikiwezekana tutaweka kituo cha polisi pale, vijana wa Dar es Salaam changamkieni ajira hizi, lakini msiwe wazembe au wadokozi.”
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya wataalam wanaosimamia ujenzi huo, alisema kamati yake itafanyakazi kwa uadilifu ili kuhakikisha kuwa daraja hilo linajengwa kwa ubora wa kimataifa.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali akiwemo Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, ambaye alisema mradi huo utazalisha pia ajira za kudumu takribani 1,000.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Hubert Mrango, Wenyeviti wa Bodi mbalimbali ikiwemo ya makandarasi, wahandisi, wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi na maofisa wengine waandamizi kutoka Wizara ya Ujenzi na NSSF.
CHANZO: NIPASHE

Balozi Seif aitaka NSSF kuongeza wanachama

3rd February 2012
Chapa
Maoni
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd
Mfuko wa Hifadhi za Jamii nchini (NSSF), umetakiwa kuhakikisha unaongeza  idadi ya wanachama wake,  ili kuongeza idadi iliopo zaidi.

Changamoto hiyo ilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, katika sherehe za ufunguzi wa kongamano la pili la wadau wa mfuko huo wa kimataifa.
Balozi Idd alisema NSSF na mifuko mingine imeelekeza nguvu zake kwa kupata wanachama kutoka sekta rasmi tu na ndio maana wanachama waliopo hawafiki milioni moja.
Alisema hiyo ni kasoro kubwa inayohitajika kurekebishwa mara moja na kuna haja kwa uongozi wake kuchukua juhudi za makusudi kuongeza wanachama kutoka sekta kama kilimo ambayo Watanzania wengi zaidi wanajishughulisha nayo kuliko sekta nyingine.
Alisema zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo na kundi hilo ni muhimu sana kwa mfuko huo kama sekta hiyo itaandaliwa utaratibu mzuri.
Alisema mafanikio yaliyofikiwa na NSSF ni makubwa katika uwekezaji wa vitega uchumi vya ndani ya nchi, kwa misingi hiyo mafanikio hayo yanapaswa kwenda sambamba na kuyafanya mafao ya wanachama wake kuwa bora zaidi na makubwa zaidi.
Pia alitoa changamoto kwa mifuko yote ya hifadhi za jamii nchini kujitahidi kuyafanya mafao na malipo mengine kwa wanachama wao kuwa mazuri zaidi.
Balozi Idd aliisifu NSSF kuwa na mradi wa nyumba za bei nafuu jijini Dar es Salaam na kusema kuwa mradi huo unapaswa kuendelezwa nchini kote kwani gharama za ujenzi za nyumba kwa wanachama wa kawaida au hata mtu wa kawaida ni kubwa mno.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia inao mpango wa aina hiyo kutokana na hali hiyo inaialika NSSF kwenda Zanzibar kushirikiana na ZSSF kuwekeza katika mpango huo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau, alisema  mafaniko mengi ya mfuko huo nchini ni kwa kubuni miradi mingi ya maendeleo na kuongeza kiwango cha pensheni ambacho kimepanda kutoka Sh. 52,000 hadi Sh. 80,000.
CHANZO: NIPASHE

Wanachama waitaka NSSF ianzishe benki

11th March 2012
Chapa
Maoni
Baadhi ya Wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wameuomba mfuko huo kuanzisha benki ambayo itatumika kuwakopesha wanachama wake fedha za kuendeshea miradi mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kutumia dhamana ya akiba zao ndani ya mfuko huo.
Ombi hilo lilitolewa jana na walimu wa Shule za sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania zilizopo mkoani Mbeya wakati wa semina ya mafunzo iliyoandaliwa na NSSF mkoani hapa.
Wakichangia maoni yao katika semina hiyo, baadhi ya walimu hao walisema kutokana na umri wa kuishi wa watanzania pungua, wanachama wengi wa mfuko huo hawafikii hatua ya kustaafu na kulipwa mafao yao, hali ambayo inasababisha amana zao ndani ya mfuko kuliwa na watu wengine wasiostahili.
“Ikiwa kwa sasa mfuko wa NSSF una wanachama zaidi ya 500, ambao wanachangia kila mwezi, kwa nini isiwe benki badala ya shirika la umma ili benki hiyo itumike kuwakopesha wanachama wake kwa dhamana za akiba zao?” alihoji mmoja wa walimu hao ambaye hakutaja jina lake.
Mwalimu huyo alisema kwa sasa kati ya wanachama mia moja wa NSSF, wale wanaofikia umri wa kustaafu na kulipwa mafao yao hawafiki 10, akidai kuwa umri wa kuishi kwa watanzania umepungua na ndio sababu anapendekeza kuwa NSSF ingefungua benki ambayo ingewakopesha wanachama wake ili na wao waweze kufaidi fedha zao wangali hai.
Akijibu hoja hiyo Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Hamis Fakii, alisema suala la NSSF kufungua benki haliwezekani kwa kuwa kila taasisi ina majukumu yake.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI